Loading...

Wahudumu wa mabasi ya mwendo kasi wagoma, ..wadai mishahara ni midogo.

MWEZI mmoja baada ya madereva wa mabasi ya mwendo kasi kugoma wakilalamikia mishahara midogo, wahudumu 142 wa mradi huo, wamegoma tena wakishinikiza kulipwa ujira wao wa miezi miwili na mikataba ya kazi.

Wahudumu hao wamedai kuwa uongozi wa mabasi hayo uliahidi kuwalipa kabla ya kuanza kutoa huduma.

Wahudumu hao ni wale wanaojishughulisha na kazi ya kuwaelekeza abiria matumizi ya kadi pamoja na tiketi, kuwaongoza jinsi ya kupanda mabasi na wanaofanya usafi wa vituo na mabasi.

Wakati wahudumu hao walikutwa na Nipashe katika ofisi za Udart Jangwani jijini Dar es Salaam juzi wakisuburi hatma yao, Mkurugenzi Mtendaji wake, David Mgwasa, alikanusha kuwapo kwa mgomo huo.

Wakizungumza na Nipashe, wahudumu hao walisema wamelazimika kugoma kutokana na maelezo yasiyoridhisha kutoka kwa uongozi kuhusu hatma ya malipo na mikataba yao ya kazi.

Mwakilishi wa kampuni ya Steward, Erick Mhagama, akizungumza kwa niaba ya wahudumu wenzake, alisema wakati mradi huo wa mabasi haujaanza, walikubaliana na uongozi mara utakapoanza watasaini mkataba wa ajira.

“Mradi ulipoanza tulianza kazi tena tunafanya usiku na mchana, lakini malipo yetu yamekuwa ni ya kusuasua,” alisema.
Alisema walikubaliana kila mhudumu atalipwa Sh. 10,000 kwa siku.

“Fedha tunazodai kwa kila mhudumu ni Sh. 670,000, tumeamua kugoma ili uongozi utupe haki yetu," alisema.

Aliongeza, “Leo asubuhi tumeonana na Mgwassa ambaye ametueleza ameandaa malipo na kumtaka Mhasibu Mkuu atupe nakala yake ili tuipitie kila mtu aangalie kama kilichojazwa ni sahihi,” alisema.

Mhudumu mwingine, Elayson Zakaria, alisema wamefikia hatua ya kugoma kutokana na kauli za viongozi kutolewa bila kutekelezwa.

Hata hivyo, Mgwassa alisema hakuna mgomo wowote na kwamba alichofanya ni uhakiki wa watu kama wapo kazini na si vinginevyo.

ZeroDegree.
Wahudumu wa mabasi ya mwendo kasi wagoma, ..wadai mishahara ni midogo. Wahudumu wa mabasi ya mwendo kasi wagoma, ..wadai mishahara ni midogo. Reviewed by Zero Degree on 8/05/2016 09:41:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.