Loading...

Klabu ya Arsenal kufanya usajili mwingine wa lala salama.

KWA mara nyingine klabu ya Arsenal imefanya kile ilichokifanya misimu kadhaa iliyopita kwa kukamilisha usajili katika siku za lala salama, ambapo ujio wa Shkodran Mustafi na Lucas Perez ulitarajiwa kukamilika hivi karibuni.

Lucas Perez
Katika siku za kwanza za dirisha la usajili, klabu hiyo iliwanasa Granit Xhaka na Rob Holding, lakini pia, si klabu ngeni machoni pa watu kwa kusajili wachezaji kwenye dakika za lala salama, tena kwa bei ghali.

Shkodran Mustafi
Je, unawajua wachezaji waliosajiliwa na klabu hiyo katika dakika za mwisho kabla dirisha la usajili halijafungwa? Na unatambua ni kwa namna gani walivyong’ara ndani ya klabu hiyo? Hii hapa orodha yao:

MSIMU WA 2015-16

Mohamed Elneny (Januari 14, pauni mil.5)


Arsenal hapa imelamba dume. Elneny, aliyetua Emirates akitokea klabu ya Basel, ameonesha uwezo mzuri kwenye eneo la kiungo, hasa suala la upigaji pasi za uhakika.

Anakumbukwa kuwa bao lake kali la kusawazisha dhidi ya Barcelona kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya lilimpatia zawadi ya bao bora la mwaka ndani ya klabu hiyo, hivyo kiasi cha pauni milioni 5 walichokitoa Arsenal kimewapa faida.

MSIMU WA 2014-15

Danny Welbeck (Septemba 2, pauni mil.16)


Welbeck alitua Arsenal na kuonesha mwanga wa kuwa mpachika mabao mzuri, lakini kitu ambacho kimemzuia fowadi huyo kudhihirisha hilo ni tatizo la majeraha ya mara kwa mara linalomkumba.

Unakumbuka lile bao alilowafunga Manchester United kwenye robo fainali ya Kombe la FA pale Old Trafford? Na ndio mwaka waliokwenda kulitwaa taji lenyewe.

Ni aina ya mabao ambayo yanatuambia kwamba, kama si majeraha ya kila mara, Welbeck angeendelea kuipaisha mno Arsenal, kwani hufanya hivyo kila anapokuwa fiti kucheza.

Gabriel Paulista (Januari 28, pauni mil.11.3)

Paulista alianza kwa kiwango kizuri, lakini woga ulianza kumwandama na akaanza kufanya makosa ya kizembe.

Ameichezea Arsenal mechi 27 za ligi mpaka sasa tangu alipotua Emirates kwa dau la pauni milioni 11 mwaka 2015. Tunamhesabia siku za kuendelea kuangalia faida yake pale Arsenal.

Kim Kallstrom (Januari 31, kwa mkopo)

Kiungo huyo aliichezea timu hiyo jumla ya mechi nne za mashindano yote kati ya Januari msimu huo na ikumbukwe kuwa alitua Arsenal huku akiwa na maumivu ya mgongo yaliyomweka nje ya uwanja kwa msimu mzima.

Hakuwa na msaada pale Arsenal na mkataba wake wa mkopo ulivyomalizika, akaachwa.

Mesut Ozil (Septemba 2, pauni mil.42.5)

Kiungo huyo ambaye kwa jina jingine unaweza kumwita ‘fundi wa pasi za mwisho’ alitua Arsenal kutoka Real Madrid kwa dau la pauni milioni 42.5 na hadi sasa amedhihirisha kuwa alistahili thamani hiyo. Ni uwezo wake tu wa kufanya maajabu katika maeneo magumu ndio unaomfanya apendwe mno pale Emirates.

MSIMU WA 2012-13

Nacho Monreal (Januari 31, pauni mil.8.3)


Monreal amejihakikishia namba yake kwenye kikosi cha kwanza cha Arsenal na kiasi cha pauni milioni 8.3 hakikutoka bure, kwani beki huyo wa kushoto amedhihirisha ubora wake linapokuja suala la kukaba na kupandisha mashambulizi kwa kasi ya juu.

MSIMU WA 2011-12

Joel Campbell (Agosti 19, pauni mil.1)


Mashabiki wa Arsenal walimpenda mno winga huyu msumbufu, lakini Kocha Wenger hakuvutiwa naye kwa asilimia 100.

Campbell aliigharimu klabu hiyo takribani pauni 1 mwaka 2011, lakini alijikuta akitolewa kwa mkopo mara tano na sasa yupo Sporting Lisbon ya Ureno.

Haonekani kama atafanya makubwa ndani ya Arsenal iwapo Wenger ataendelea kuwepo kwenye bechi la ufundi.

Andre Santos (Agosti 31, pauni mil.6)


Mbrazil huyu hakung’ara sana Arsenal alipotua akitokea Fenerbahce, aliichezea timu hiyo mechi 25 tu za ligi na mashabiki walizidi kumchoka, hasa alipoonesha kiwango kibovu dhidi ya Manchester United na kama hiyo haitoshi, akazidi kuwaudhi mashabiki hao kwa kubadilishana jezi na straika wa zamani wa United, Robin van Persie, wakati timu hizo zikienda mapumziko.

Per Mertesacker (Agosti 31, pauni mil.10)

Beki huyu mwenye umbo refu la kimo cha futi 6 na inchi 6 ameonesha ni namna gani Wajerumani wanavyosifika kwa soka la nguvu na akili, hasa kwenye eneo la ulinzi, ambalo Mertesacker anatumika.

Ndani ya mechi 149 za ligi tangu alipotua Emirates mwaka 2011, Mertesacker anatambulika kama mwamba wa Arsenal na kwa sasa wanaukosa mwamba huu kutokana na majeraha aliyoyapata ambayo yatamweka nje hadi Desemba, mwaka huu.

Mikel Arteta (Agosti 31, pauni mil.10)

Kiungo huyu wa zamani wa Everton ameichezea Arsenal kwa miaka mitano (mechi 110 za ligi). Ni wazi kuwa pauni milioni 10 hazikupotea bure, kwani ndani ya miaka yote hiyo ameiongoza Arsenal kutwaa mataji mawili ya FA na Ngao ya Jamii moja.

MSIMU WA 2010-11

Sebastien Squillaci (Agosti 26, pauni mil.4)


Mfaransa huyu alichezea Arsenal mechi 23 za ligi huku akifunga bao moja, lakini makosa ya kizembe yalishindwa kuvumilika na Wenger akaamua kumvuta Mertesacker mwaka huo ili kuondokana na aibu ya kuwa na beki huyu ‘uchochoro’.

Credits: Dimba
ZeroDegree.
Klabu ya Arsenal kufanya usajili mwingine wa lala salama. Klabu ya Arsenal kufanya usajili mwingine wa lala salama. Reviewed by Zero Degree on 8/31/2016 10:25:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.