Loading...

Maelezo ya awali kesi ya Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu [ CHADEMA ], kuanza kutolewa Agosti 29.

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imepanga kusikiliza maelezo ya awali ya kesi ya uchochezi, inayomkabili Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu na wenzake, Agosti 29, mwaka huu.

Hatua hiyo ilifikiwa jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Respicius Mwijage, baada ya upande wa Jamhuri kudai upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.

Upande wa Jamhuri, ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu Bernad Kongola, akisaidiana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi, ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika lakini mshtakiwa wa kwanza, Jabir Idrisa, bado hajapatikana.

Kongola alidai kwa kuwa mshtakiwa huyo hajapatikana na upande wa Jamhuri uliomba tarehe ya kuwasomea washtakiwa maelezo ya awali.

Hakimu Mwijage alisema kesi hiyo itasikilizwa maelezo ya awali Julai 29, mwaka huu na dhamana za washtakiwa zinaendelea.

Hakimu alitoa amri hiyo baada ya Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba, anayesikiliza kesi hiyo kuwa na udhuru wa kikazi.

Mbali na Idrisa na Lissu, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni wahariri wa gazeti la Mawio ambalo linadaiwa kuchapisha habari ya uchochezi yenye kichwa cha habari ‘Machafuko yaja Zanzibar’. Wahariri hao ni Simon Mkina, Jabir Idrisa na mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehboob.

Ilidaiwa kuwa washtakiwa walichapisha bila kuwasilisha hati ya kiapo kwa Msajili wa Magazeti.

Washtakiwa hao wanadaiwa kutenda makosa hayo Januari 14, mwaka huu,jijini Dar es Salaam.

Katika kesi ya msingi, ilidaiwa kuwa Lissu na wenzake wanakabiliwa na kosa la kuchapisha taarifa za uchochezi Januari 14, mwaka huu, jijini Dar es Salaam, kuchapisha habari hizo ili kuleta chuki kwa wananchi wa Zanzibar.

Ilidaiwa kuwa Lissu na wenzake bila ya kuwa na mamlaka yoyote yale, waliwatishia na kuwatia hofu wananchi wa Zanzibar ili wasiweze kuingia kwenye marudio ya uchaguzi mkuu.

Credits: IPPMedia
ZeroDegree.
Maelezo ya awali kesi ya Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu [ CHADEMA ], kuanza kutolewa Agosti 29. Maelezo ya awali kesi ya Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu  [ CHADEMA ], kuanza kutolewa Agosti 29. Reviewed by Zero Degree on 8/03/2016 08:55:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.