Loading...

Magufuli agomea ahadi ya Kikwete

Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt. John Pombe Magufuli akimpongeza Mbunge wa zamani wa Kahama James Lembeli mara baada ya kuwasalimia wananchi.

MWAKA mmoja na miezi minne tangu Rais wa nne Jakaya Kikwete kutoa ofa ya kujenga upya nyumba 650 za wakazi wa Kamaha wilayani hapa zilizobomolewa na mvua ya mawe, mrithi wake, John Magufuli, amesema hawezi kutekeleza ahadi hiyo.

Aidha, Rais wa tano Magufuli amesema kama wapo wanacnhi watakaomchukia kwa kutotekeleza ahadi hiyo, acha wamchukie.

Machi 12 mwaka jana, ikiwa ni siku chache tangu mvua ya mawe kunyesha na kuacha mamia wakiwa hawana makazi, Kikwete aliahidi kujenga nyumba za kaya 468 kwa Sh. bilioni 15 na kwamba kazi hiyo ilikuwa ifanywe na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

Lakini jana, Rais Magufuli akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika wilayani Kahama, alisema wananchi wanaosubiri kutimiziwa ahadi ya Rais Kikwete, wanatakiwa kubadilika kifikra.

Magufuli alisema serikali yake haiwezi kukubaliana na ahadi hiyo kutokana na waathirika wa janga hilo kushindwa kufanya jitihada binafsi, badala yake kusubiria kujengewa nyumba na serikali.

“Huo ni ufinyu wa mawazo na uzembe, wanatakiwa wajiongeze ili kutimiza majukumu yao na wala si kufikiria serikali itawajengea nyumba zao,” alisema Rais Magufuli.

Alisema Rais aliyepita alitoa ahadi hiyo kwa wananchi hao, lakini awamu yake haitoweza. Alimtaka kila mtu asimame kwa nafasi yake na sio kutegemea serikali ambayo ina majukumu mengi ya kimaendeleo.

“Suala la kuwajengea nyumba siwezi kuwadanganya, sipo tayari na wala siwezi kuwajengea nyumba,” alisema Rais Magufuli ambaye serikali yake imeanza utekelezaji wa ahadi ya elimu bure kuanzia darasa la awali mpaka kidato cha nne.

"Kama kuna mtu atakayenichukia, anichukie tu kutokana na hilo, ila sitoweza kujenga nyumba hizo, siwezi kuwaficha kabisa wananchi wangu.

"Penye ukweli lazima tuseme na wala siyo kufichana."

DAWA HOSPITALINI

Aidha, Rais Magufuli alisema kutumia fedha kujenga nyumba za watu ambao watalala na familia zao, sio jambo la la kawaida na kuwataka wajenge wenyewe ili pesa ambazo zingetumika kujengea nyumba hizo, ziweze kununulia dawa hospitalini zitakazosaidia kuokoa maisha ya watu.

“Kupanga ni kuchagua ndugu zangu, ahadi aliiyoitoa Kikwete haitatekelezwa.

“Serikali hii ninayoongoza siwezi kuwajengea nyumba kabisa, watoto wanakaa chini mashuleni, nyie mmekaa tu, mwaka mzima mnasubiri mjengewe nyumba na serikali?

“Sipo tayari kujenga nyumba ya Mariam ama Marietha wakati mnahitaji maji na reli.”

Machi 13 mwaka jana, Kikwete aliwatupia lawama watendaji wa serikali kwa namna walivyo legelege katika kuwahudumia waathirika wa mafuriko hayo na kuahidi kuwajengea nyumba mpya za kisasa.

Mafuriko hayo pia yaliharibu hekari 2,332 za mazao mbalimbali ya chakula na biashara, huku visima 53 vya maji ya kunywa vikiwa vimeharibiwa.

47 WALIFARIKI DUNIA

Machi 12, Kikwete alifika kwenye kijiji cha waathirika hao ambako kutokana na mvua hizo, watu 47 walifariki dunia na wengine 112 kujeruhiwa.

Akiwa katika Shule ya Msingi Mwakata ambako wahanga hao walihifadhiwa kwa muda, Kikwete aliwahakikishia kwamba hakuna atakayekufa na njaa baada ya mvua hiyo kuharibu mashamba yao, na kwamba serikali itakuwa nao bega kwa bega mpaka watakaporudi katika makazi yao ya kawaida.

Alisema serikali ingetoa tani 20 za unga wa sembe ili ugawiwe kila kaya kwa ajili ya chakula cha mwezi mzima, huku misaada mingine kutoka kwa wahisani mbalimbali ikiendelea kutolewa.

Alisema serikali ingejenga nyumba katika kaya zote 468 zilizoathiriwa na mvua hizo na zabuni hiyo haitatolewa kwa makampuni binafsi na badala yake JKT itafanya kazi hiyo.

Aliahidi ujenzi huo ambao ulitarajiwa kugharimu Sh. bilioni 15 ungekamilika ndani ya siku tisini, ili wananchi warudi katika makazi yao na kuendelea na shughuli mbalimbali za maendeleo.

Lakini jana Rais Magufuli aliwataka wananchi wa Mwakata kuhakikisha wanafanya kazi za vibarua katika mradi wa reli ya kati pale utakapoanza kujengwa ili kujiimarisha kiuchumi.

Awali akiwa mjini Kahama, Rais Magufuli alipiga marufuku watumishi wa halmashauri kuwatoza ushuru wajasiriamali wadogo na kuwaagiza wajikite zaidi katika kuwasimamia wafanyabiashara wakubwa kulipa kodi.

Mbunge wa Kahama Mjini (CCM), Jumanne Kishimba, alisema wananchi, hasa wajasiriamali wadogo, wamekuwa wakinyanyaswa na maafisa biashara kwa kuwatozwa ushuru kwa nguvu bila kuangalia aina ya biashara wanazofanya.

Rais Magufuli aliwataka wananchi wa wilaya hiyo na Watanzania kwa ujumla, kufanya kazi kwa kujituma badala ya kuitegemea serikali na kuachana na masuala ya siasa ambayo hayawanufaishi.

Rais Magufuli alieleka mkoani Geita ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake iliyoanzia mikoa ya Singida, Tabora na Shinyanga akitokea mjini Dodoma.

Source: Nipashe(IPPMedia)
ZeroDegree.
Magufuli agomea ahadi ya Kikwete  Magufuli agomea ahadi ya Kikwete Reviewed by Zero Degree on 8/01/2016 08:24:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.