Loading...

Magufuli aibua ‘dili’ chafu CCM.

Rais John Magufuli.

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais John Magufuli, ameshitukia ‘dili chafu’ zinazofanywa kwenye majengo, viwanja na mali mbalimbali zinazomilikiwa na Jumuiya za chama hicho na kuahidi ‘kula sahani moja’ na wahusika ili kuokoa fedha zinazoliwa na baadhi ya watu kila uchao.



Magufuli alisema ni aibu kuona chama kikubwa kama CCM kikitembeza bakuli kwa wafadhili na wafanyabiashara wakubwa kila unapokaribia uchaguzi wakati chenyewe kina vyanzo vingi vya kujiingizia mapato ambayo hivi sasa yanaishia mikononi mwa watu wachache.

Rais Magufuli aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana, wakati akizungumza na viongozi na wanachama wa chama hicho muda mfupi baada ya kutembelea ofisi yake iliyopo Makao Makuu ya Chama hicho, Lumumba.

Rais Magufuli alisema wapo viongozi ndani ya CCM ambao wamegawana vyumba vya majengo mali ya chama hicho na wengine wakikodisha kwa bei ya juu huku fedha kidogo tu ndizo zinazobaki na kupelekwa CCM.

Aliyataja majengo hayo kuwa ni lile la Umoja wa Vijana UV-CCM, Lumumba ambapo baadhi ya viongozi wake wamegawana vyumba, Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) ambao walikuwa na jengo la hoteli na kuingia ubia na mfanyabiashara mmoja huku akihoji fedha zinazopatikana zinakwenda kwa nani.

Rais Magufuli alihoji pia fedha zinazotokana na vitega uchumi vya Jumuiya ya Wazazi CCM zinaingia kwenye mfuko wa watu gani.

Hivi sasa, baadhi ya viongozi wakuu wa jumuiya hizo ni Sadifa Juma ambaye ni mwenyekiti wa UV-CCM, Sophia Simba (Mwenyekiti UWT) na Abdallah Bulembo anayeshikilia uenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi. Wote hao, na wenzao, wanatarajiwa kuwa na kibaria cha ziada katika kuhakikisha kuwa jumuiya zao zinaandaa majibu ya kutosha kuhusiana na maswali ya mwenytekiti wao, Rais Magufuli.

Aidha, mbali na majengo mbalimbali ya jumuiya hizo za CCM, Magufuli alihoji pia fedha zinazotokana na viwanja zaidi ya 400 vinavyomilikiwa na chama hicho, huku akitolea mfano viwanja vya CCM Kirumba jijini Mwanza na Majimaji Songea ambavyo vimezungukwa na fremu za maduka ya kukodisha lakini fedha za pango kwa viwanja hivyo zimekuwa zikimegwa na baadhi ya wana- CCM ambao ameapa ‘kulala nao mbele’.

Mwenyekiti huyo mpya aliyetwaa kiti cha uongozi wa chama Julai 23 kutoka kwa mtangulizi wake, Rais mstafu Jakaya Kikwete, alifika kwenye ofisi ndogo za CCM Makao Makuu jijini Dar es Salaam hizo jana saa 5:01 asubuhi akitokea Mwanza na kupokelewa na viongozi na wana CCM ambao walikusanyika kwa wingi ofisini hapo kwa lengo la kumpokea na kusikiliza hotuba yake.

Mara baada ya kuwasili hapo, Magufuli alipokewa na mawaziri, wabunge na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Tulia Ackson, kisha aliingia ndani ya jengo la chama na kuonyeshwa ofisi yake.

Katika hotuba yake iliyotumia takribani dakika 55, Magufuli alitangaza kukifumua upya chama hicho kwa lengo la kukiondoa mikononi mwa wala rushwa, mafisadi na wenye uchu wa madaraka kiasi cha kutumia fedha kupata vyeo.

AFAFANUA KUHUSU MALI ZA CCM. 

Magufuli alitangaza kuwafuatilia mafisadi ndani ya CCM ambao wanakiangamiza chama hicho na kukisababishia kuwa ombaomba.

“Lazima niseme ukweli na msema kweli ni mpenzi wa Mungu, si kweli kwamba CCM hapakuwapo na mafisadi… wapo na ndiyo maana wengine walikimbilia upinzani na wengine wamebaki wanajilimbikizia mali za chama. Wanajinufaisha wenyewe na kuwaacha wanachama ambao ni maskini wenzangu wakiwa hawana kitu. Hawa sitawavumilia nikiwa kama Mwenyekiti wa CCM,” alisema.

Alisema CCM katika Mkoa wa Dar es Salaam ina viwanja zaidi ya 400, lakini alisema kwa miaka nenda rudi fedha zinazopatikana haijulikani zinakwenda wapi na nani wanazisimamia.

“Tulikuwa na Sukita (Shirika la Uchumi na Kilimo) fedha zipo wapi, jengo la UVCCM ambayo ni maghorofa makubwa nimeambiwa baadhi ya viongozi wa vijana wamegawana vyumba… je, fedha zinazopatikana zinaenda kwenye mfuko wa nani? Haya ndiyo nitayachambua kituo kwa kituo, koma kwa koma, nukta kwa nukta mpaka kieleweke,” alisema na kuibua shangwe kutoka kwa wanachama waliofika hapo.

“UWT kulikuwa na jengo la hoteli… na vitega uchumi vya wazazi vimeenda wapi? Viwanja vya Mwanza, Songea na maeneo mengine na kila kiwanja kimezungukiwa na maduka yanayoonyesha yanakodishwa Sh. 20,000 au Sh. 30,000… lakini kumbe ni zaidi ya Sh. milioni moja, kuna wana CCM wanamega fedha hizo, nitahakikisha nalala nao mbele,” alisema.

“Haiwezekani kila ikifikia uchaguzi tunaenda kuomba kwa wafanyabiashara. UWT wanaomba, UVCCM wenye maghorofa nao wanaomba, Wazazi wanaomba,” alisema.

Aliongeza, “UWT wanaomba mpaka kwa wale walioondoka CCM, mchana UWT ni CCM, usiku Chadema… nasema uongo UWT (umati ukamjibu… kweliiiii). Nataka chama kwa ajili ya wanachama, chama kwa ajili ya Watanzania ili kiendelee kutawala milele,”

“Hamjiulizi kwa nini nini Redio Uhuru haipati matangazo? Kwa nini kikundi cha TOT wanashinda kuwa ombaomba, hamjiulizi kwa nini CCM chama kikubwa hakina hata TV, lazima tujipange vizuri, tubadilike, tupate changamoto, asiyekubali kubadilika tutajitahidi kumbadilisha, akishindwa tutamuweka pembeni,” alisema.

Aidha, Magufuli alisema anataka chama safi kilichonyooka kwa ajili ya wanachama na Watanzania wote na si kwa matajiri pekee.

KINANA, MAJAWALIWA WANENA

Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdurahman Kinana, alimuahidi Mwenyekiti huyo kuwa baada ya kumuamini yeye na sekretarieti yake na kuwataka waendelee na uongozi, ataenda kwa kasi kama yake ili wawakomboe wanyonge.

Pia alisema baada ya Rais kumchagua pale Dodoma Julai 23, mwaka huu, siku nne mbele alimtaka yeye na sekretarieti yake wakutane naye na miongoni mwa mambo aliyotaka wayashughulikie ni uhakiki wa watumishi wa CCM pamoja na mali za chama.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, aliwaahidi Watanzania kuwa CCM na serikali yake haitawaangusha na itafanya kila liwezekanalo ili maendeleo yapatikane.

Source: Nipashe(IPPMedia)
ZeroDegree.
Magufuli aibua ‘dili’ chafu CCM. Magufuli aibua ‘dili’ chafu CCM. Reviewed by Zero Degree on 8/13/2016 08:00:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.