Loading...

Mavugo hatihati kuichezea Simba.

Mshambuliaji mpya wa Simba, Laudit Mavugo.
MSHAMBULIAJI mpya wa Simba, Laudit Mavugo, huenda akashindwa kuitumikia timu yake katika mechi ya kwanza ya ufunguzi wa msimu mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania (VPL).


Simba itaanza kampeni ya kuwania ubingwa wa ligi msimu wa 2016/17 kwa kuikaribisha Ndanda FC kutoka Mtwara, mechi itakayopigwa kesho kwenye Uwanja wa Uhuru (Shamba la Bibi), Dar es Salaam.

Mchezaji huyo huenda akakosa kuanza kucheza mechi hiyo kutokana na hati yake ya uhamisho wa kimataifa (ITC) kutopatikana hadi jana jioni.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara, alisema uongozi uko katika hatua ya mwisho ya kukamilisha uhamisho wa mshambuliaji huyo waliyemsajili akitokea kwa mabingwa wa Ligi Kuu Burundi, Vital’ O.

Manara alisema viongozi wa Simba waliokwenda Burundi kushughulikia suala hilo, wametoa taarifa kwamba mazungumzo na klabu yake ya zamani ya Solidarity ambayo ndiyo ina haki na mchezaji huyo yako katika hatua za mwisho.

Kiongozi mwingine wa juu wa klabu hiyo, aliwataka wanachama na mashabiki wa Simba kuwa watulivu kwa sababu uongozi unafanya kila juhudi kuhakikisha usajili wa Mavugo unakamilika na kesho anashuka uwanjani kuitumikia klabu yake.

“Suala la ITC linaendelea kushughulikiwa na mpaka sasa (jana jioni) maombi yote yameshatumwa, huenda likakamilika wakati wowote na tatizo dogo lililokwamisha wameshalifanyia kazi,” alisema kiongozi huyo (jina tunalihifadhi).

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Selestine Mwesigwa, alisema jana kuwa bado Simba ina nafasi ya kumaliza usajili huo na ikapata nafasi ya kumtumia katika mechi ya kesho.

Wakati huo huo, kikosi cha Simba kilichoko chini ya Mcameroon Joseph Omog, jana kiliendelea na mazoezi kwenye Uwanja wa Boko Veterans kwa ajili ya kujiimarisha kuikabili klabu hiyo kutoka mkoani Mtwara.

Katika hatua nyingine, Simba jana iliwasilisha malalamiko TFF kupinga hatua ya Yanga kuruhusiwa kumtumia Hassan Kessy wakati klabu hiyo imeweka pingamizi kuhusiana na beki huyo.


Source: Nipashe
ZeroDegree.
Mavugo hatihati kuichezea Simba. Mavugo hatihati kuichezea Simba. Reviewed by Zero Degree on 8/19/2016 10:22:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.