Loading...

TFF yatoa siku 2 kwa Yanga kueleza sababu za kushindwa kuwasilisha usajili wao.

Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limetoa siku mbili kwa klabu ya Yanga na Coastal Union kueleza sababu za kushindwa kuwasilisha usajili wao.

Mbali na hilo, TFF pia imezitaka timu za African Lyon (Ligi Kuu), Kiluvya United, Mashujaa, Friends Rangers, Abajalo (Daraja la Kwanza), Kitayosa na Mvuvumwa (Daraja la pili) kukamilisha usajili wake ndani ya siku mbili.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu Mkuu wa TFF Selestine Mwesigwa alisema dirisha la usajili kwa timu zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara, Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Daraja la Pili msimu wa mwaka 2016/2017 lilifungwa saa 6.00 usiku wa Jumamosi Agosti 6, 2016 na timu hizo ndizo hazijawasilisha usajili wake.

“Klabu ya Yanga na Coastal Union hazijawasilisha usajili wao, lakini timu nyingine saba zina kasoro kwenye usajili hivyo TFF inasubiri barua za utetezi wa klabu ambazo hazikukamilisha usajili ili utumwe utetezi huo FIFA na endapo itaona una mashiko itatoa maamuzi yake,” alisema Mwesigwa.

Mwesigwa alisema usajili unafanywa kwa njia ya mtandao wa TMS (Transfer Matching System) ambao chombo chake cha kutunza kumbukumbu kipo makao makuu wa Fifa, Uswisi.

Awali, kabla ya kuanza kwa usajili Juni 15, 2016 mwaka huu, TFF iliandaa mafunzo ya usajili kwa klabu zote 64 zinazoshiriki Ligi Kuu, daraja la kwanza na la pili ambapo kila klabu ilitakiwa kupeleka watendaji wawili ili kuongeza ufanisi na kuondoa kasoro ambazo zimekuwa zikijitokeza lakini Yanga na Simba hazikupeleka mtu kwenye mafunzo.

Kwa mujibu wa Mwesigwa, klabu ambazo zilishindwa kufanya usajili huo kwenye mtandao ziliomba msaada TFF na kutoa mfano wa Mkamba Rangers ya ligi daraja la kwanza kutoka Morogoro ilituma mtu TFF kusaidiwa kufanya usajili.

Usajili wa mfumo pepe ni utaratibu wa FIFA na imesaidia kuondoa ujanjaujanja wa viongozi au watendaji katika usajili wa wachezaji. Kuhusu kuomba kusogezewa usajili mbele, Mwesigwa alisema: “huwa kuna gharama na mfano kwenye uhamisho wa Emmanuel Okwi ambaye pasi ya kusafiria ilichelewa kupakia (ku-upload) na kufanya TFF kutozwa faini dola za Marekani 5,000 ambazo ni zaidi ya Sh milioni 10 za Tanzania.”

Mwesigwa alizitahadharisha klabu endapo itatokea dirisha za usajili kufunguliwa zitakabiliwa na faini ya dola za Marekani 500 kwa kila mchezaji na kuongeza kuwa pamoja na faini hiyo ni wajibu wao kuendelea kuwasiliana na FIFA ili kuomba dirisha kufunguliwa.

Klabu za Yanga, Coastal Union, African Lyon, Kiluvya United, Mashujaa, Friends Rangers, Abajalo, Kitayosa na Mvuvumwa ambazo hazikutuma usajili wake zinatakiwa kuandaa utetezi utakaotumwa FIFA yenye mamlaka ya kufungua dirisha la usajili na endapo utetezi huo utakataliwa basi timu husika inabidi ishuke daraja ambalo halimo kwenye usajili wa mfumo wa TMS.

Yanga haijasema sababu za kutopeleka usajili wao baada ya Katibu wake Mkuu, Deusdedit Baraka simu yake kuita bila majibu.


Credits: Habari Leo
ZeroDegree.
TFF yatoa siku 2 kwa Yanga kueleza sababu za kushindwa kuwasilisha usajili wao. TFF yatoa siku 2 kwa Yanga kueleza sababu za kushindwa kuwasilisha usajili wao. Reviewed by Zero Degree on 8/10/2016 09:39:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.