Loading...

Wabunge watoro kutumbuliwa.

UONGOZI wa Bunge umesema utoro kwa watunga sheria ni tatizo sugu na utalazimika kuzifanyia marekebisho kanuni zake ili kuwabana wabunge wenye tabia hizo na ikiwezekana kuwavua nyadhifa hiyo.



Spika wa Bunge, Job Ndugai aliyasema hayo katika mahojiano maalum na moja ya vituo vya runinga vya jijini Dar es Salaam jana.


Spika wa Bunge, Job Ndugai
Ndugai alisema tabia ya utoro kwa wabunge ni tatizo sugu si kwa Bunge la Tanzania tu, bali hata mabunge ya nchi jirani. 

“Ni tatizo sugu na kubwa, kanuni zinasema mbunge asipokuwapo bungeni kwa mikutano mitatu mfululizo, anaweza kuchukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kupoteza ubunge wake. Mikutano mitatu tafsiri yake ni robo tatu ya mwaka asipokuwapo angalau siku moja," alisema. 


“Mbunge mtoro, anakuja siku moja anakuwa amevuka kanuni, huwezi kumchukulia hatua. Kwanza inabidi tuitazame kanuni yetu ili kuikazia na pia tujifunze utoro unaletwa na jambo gani."

Aliwataka wabunge kuhudhuria vikao vya bunge ili kutimiza jukumu lao la kuwasemea wananchi kero zao.

Alisema kutokuwapo kwao bungeni pamoja na kitendo cha kususia vikao si tatizo kwa wabunge wa wa upinzani tu, bali hata kwa wabunge wa CCM, hivyo kuna haja kanuni inayohusu utoro ifanyiwe marekebisho ili kukomesha wenye tabia hiyo.

Ndugai pia alikiri kuwa posho za wabunge haziridhishi huku akidokeza kuwa huenda ni sababu mojawapo ya mahudhurio hafifu ya wabunge kwenye vikao vya bunge.

MWAKA 2020


Akizungumzia uamuzi wa serikali kupiga marufuku mikutano ya kisiasa hadi mwaka 2020, Ndugai aliuunga mkono na kusisitiza siasa zihamie bungeni kwa kuwa uchaguzi umeshamalizika.

“Hata nchi za wenzetu kama Marekani, unaona wakati wa uchaguzi wataitana majina ya kila aina, lakini ukiisha hakuna maandamano, mikutano ya kisiasa wala kuitana majina yasiyofaa," alisema Ndugai.

"Kuendelea na kampeni zisizoisha, hakuwezi kujenga nchi. Kwa ujumla, maelekezo ambayo yametolewa tuyafuate.”
Ndugai pia alisema kuna tabia ya vijembe, dharau na kejeli zinazofanywa na wabunge wa pande zote ambazo hazimfurahishi na kwamba katika bunge lijalo kanuni zitafanya kazi kwa wabunge wenye tabia hiyo.

"Tutarajie bunge imara, lisilokuwa na matusi, vijembe, kejeli na nitajitahidi sana tuweze kuwa na Bunge lenye kuelewana. Tufike mahali tuendeshe bunge kwa kanuni na kama zina matatizo, basi tuzirekebishe," alisema.

Kiongozi huyo wa Bunge alisisitiza kurudisha nidhamu ya bunge kwa wabunge wote wa upinzani na hata wale wa CCM hasa kwenye matumizi ya lugha zisizo na staha, vijembe, matusi na matusi.

Alisema kwa sasa uongozi wa bunge hilo utajielekeza kwenye kanuni kuchukua hatua na Watanzania watarajie kuona Bunge lenye nidhamu.

KUHAMIA DODOMA

Kuhusu kuhamia Dodoma, Spika huyo alisema uongozi wa bunge hilo unamuunga mkono Rais John Magufuli na watahakikisha watumishi wa bunge walio Dar es Salaam wanafungasha virago na kuelekea Dodoma kufikia mwezi ujao, na kwamba ofisi za Dar es Salaam zinakuwa na watumishi wasiozidi watano ambao watakuwa wakiratibu shughuli za wabunge kwenda nje na matibabu.

“Ofisi ya bunge kuanzia Septemba watumishi wote ni Dodoma, tuna ofisi za kutosha na watumishi wa bunge wengi wana makazi Dodoma, kwa hiyo ni watu wanaoishi Dodoma. Suala la malipo kwa sasa hatalipwa mtu, kinachotakiwa ni kwenda Dodoma kwanza,” alisema Ndugai.

Source: Nipashe
ZeroDegree.
Wabunge watoro kutumbuliwa. Wabunge watoro kutumbuliwa. Reviewed by Zero Degree on 8/15/2016 08:45:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.