Loading...

Wasira azidi kumkomalia Bulaya.

Aliyekuwa Mbunge wa Bunda (CCM), Stephen Wasira.
KESI ya kupinga matokeo ya ubunge katika jimbo la Bunda Mjini, iliyofunguliwa na wapigakura wanne wa jimbo hilo, jana ilianza tena kunguruma katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza.


Wapigakura hao, Magambo Masatu na wenzake watatu, walifungua kesi hiyo mahakamani kupinga ushindi wa Ester Bulaya wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) dhidi ya aliyekuwa Mbunge wa Bunda (CCM), Stephen Wasira, katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

Kesi hiyo namba moja ya mwaka 2015, inasikilizwa na Jaji Lameck Mlacha wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza.

Kesi hiyo ambayo inagusa hisia za Watanzania wengi, hususani wa Kanda ya Ziwa, awali ilitupiliwa mbali baada ya kuona haiona mashiko kabla ya Mahakama ya Rufani Tanzania kuirejesha.

Shauri hilo lilianza kusikilizwa saa 3:30 asubuhi huku pande zote mbili zikionekana kutoa hoja kali ambazo zilimlazimu Jaji Mlacha kuahirisha kesi hiyo.

Wakili wa Bulaya, Tindu Lissu, alidai kuwa wapeleka maombi hao hawakuainisha vifungu vya kisheria ambavyo vinaipa mahakama nafasi ya kuyapokea.

Lissu alidai kuwa walalamikaji pia hawajaonesha vitendo vya rushwa vilivyofanywa na mfuasi wa mlalamikiwa (Bulaya) na kwamba kutokana na kukosewa huko, mahakama inapaswa kutupilia mbali ombi hilo.

“Mheshimiwa Jaji, vitendo vya rushwa ambavyo vinatajwa na walalamikaji havijaoneshwa kisheria kama wangefanya vitendo hivyo mbunge (Ester Bulaya) au wakala wake na vikadhibitika matokeo ya ubunge kisheria yanapaswa kutenguliwa,” alidai Lissu.

Kutokana na hali hiyo, alidai kuwa mahakama haina budi kutupilia mbali maombi hayo kwa kuwa walalamikaji wamekosea vifungu vya kufungulia kesi na mgombea ubunge (Wassira) alinyimwa haki ya kuhesabu kura na kuhakiki kura kwenye vituo ambavyo hawajavionesha katika maombi yao.

Wakili wa walalamikaji, Constatine Mtalemwa, akijibu hoja za pingamizi zilizowasilishwa na Lissu, alidai kuwa hazina mashiko.

Mtalemwa alidai kuwa katika vifungu vinavyosemwa na mjibu maombi namba moja, havijaonyeshwa na kuipa mahakama kuvisikiliza kisheria na kwamba wateja wake wanapaswa kusikilizwa.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Jaji Mlacha aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 25, mwaka huu, ili kupitia vifungu vyote kisheria na kuangalia kama maombi ya walalamikaji yana mashiko kisheria.

Source: Nipashe
ZeroDegree.
Wasira azidi kumkomalia Bulaya. Wasira azidi kumkomalia Bulaya. Reviewed by Zero Degree on 8/18/2016 08:00:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.