Loading...

Yanga, Azam FC mechi ya kisasi leo

MABINGWA wa soka nchini Yanga wakiwa na rekodi nzuri ya kuifunga Azam FC katika mechi ya Ngao ya Jamii leo wanakutana tena kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kama alama ya kuanza msimu mpya wa Ligi Kuu Bara 2016/17.

Yanga ambayo mwishoni mwa wiki imetupwa nje katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika, itashuka uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya kushinda katika misimu mitatu mfululizo kuwania ngao hiyo.

Ikiwa na makocha tofauti Yanga iliichapa Azam FC bao 1-0 mwaka 2013 halafu ikashinda mabao 3-0 mwaka uliofuata na mwaka jana walishinda tena kwa njia ya penalti 8-7 baada ya kutoka suluhu katika dakika 90 za kawaida.

Endapo leo Yanga itatwaa taji hilo itakuwa ni mara ya sita, kwani ukiacha mara hizo tatu ilizoifunga Azam pia iliwahi kutwaa mwaka 2001 kwa kuwafunga Simba mabao 2-1 na 2010 ilipoichapa tena Simba mabao 3-1 kwa njia ya penalti.

Yanga pia ndiyo inayoongoza kwa kutwaa taji hilo na Ngao ya Jamii mara nyingi zaidi, imeshinda mara tano na kuipa wakati mgumu Azam kumaliza 'uteja' kutoka kwa mabingwa hao.

Kocha wa Yanga, Hans van der Pluijm aliliambia gazeti hili kuwa mechi za kimataifa zimewaimarisha wachezaji wake na leo wamejipanga kushinda ili kuanza vyema msimu mpya.

Zeben Hernandes, kocha mkuu wa Azam alisema kwamba amezitumia mechi za Kombe la Shirikisho Afrika kuipeleleza Yanga na leo wataikabili kwa mbinu tofauti ili kupata ushindi.

Katika mechi ya leo Yanga itawakosa wachezaji wake nyota watano ambao ni pamoja na kipa Ally Mustafa ‘Barthez’, mabeki Juma Abdul, Andrew Vincent ‘Dante’, Kelvin Yondani na kiungo Obrey Chirwa ambao ni majeruhi.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Selestine Mwesigwa alisema jana kuwa sehemu ya mapato ya mchezo huo yatapelekwa kununua madawati ili kuunga mkono agizo la Rais John Magufuli.

Source: IPPMedia

ZeroDegree.
Yanga, Azam FC mechi ya kisasi leo Yanga, Azam FC mechi ya kisasi leo Reviewed by Zero Degree on 8/17/2016 11:15:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.