Loading...

Bandari Dar yapaisha mapato TRA.

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi TRA, Richard Kayombo.
SIKU moja baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira, kueleza kushitushwa na kupungua kwa mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam, Mamlaka ya Mapato (TRA) imeeleza kuwa makusanyo ya kodi katika bandari hiyo, yanaongezeka kwa kasi.


Ongezeko la makusanyo katika Bandari ya Dar es Salaam ni sehemu ya makusanyo ya kodi, yaliyowezesha TRA kuweza kukusanya Sh trilioni 1.158 katika makusanyo ya mwezi Agosti mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi TRA, Richard Kayombo alisema kuwa mapato hayo ni kutokana na makusanyo kutoka maeneo yote ya kodi. Katika kile kinachodhihirisha kuwa makusanyo katika Bandari ya Dar es Salaam yameongezeka licha ya kuwepo kwa propaganda nyingi kuwa upungufu wa mizigo bandarini umeshusha kodi za serikali,

Kayombo alisema; “licha ya mizigo kupungua bandari ya Dar es Salaam lakini makusanyo ya kodi katika bandari hiyo yameongezeka mara dufu.”

Kayombo alisema TRA imefanikiwa kukusanya kiasi cha Sh trilioni 1.158 katika makusanyo ya mwezi Agosti mwaka huu na kusema kuwa makusanyo hayo yanatokana na mikakati madhubuti waliyojiwekea.

Alisema makusanyo hayo yameiwezesha mamlaka hiyo kuvuka lengo la makusanyo iliyojiwekea ya kukusanya Sh trilioni 1.152 ambayo ni sawa na asilimia 100.57. ambapo mwezi kama huo mwaka jana ilikusanya Sh bilioni 923.

“Tumekusanya kodi hii kutokana na mikakati madhubuti tuliyojiwekea, na mapato haya yanatokana na kodi mbalimbali ambazo zimekuwa zikikusanywa kwa ushirikiano mkubwa baina ya wafanya biashara na Mamlaka,” alisema Kayombo.

Alisema TRA katika kuhakikisha kuwa inakusanya kodi zote stahiki vizuri, imejiwekea mikakati mbalimbali ya kuongeza wigo wa vyanzo vya mapato pamoja na kukusanya mapato kikamilifu.

Alisema miongoni mwa mikakati hiyo ni pamoja na kulifanya eneo la Kariakoo kuwa Mkoa Maalumu wa Kodi kutokana na eneo hilo kuwa kitovu cha biashara hapa nchini na kuhakikisha kila mfanyabiashara anakuwa na Mashine ya Kielektroniki ya Kodi (EFDs) na kuitumia ipasavyo.

Katika kuhakikisha hilo linafanya kazi, Kayombo alisema mawakala wote wa EFDs tayari wamefungua ofisi ya pamoja katika jengo la Al-Falah Towers lililopo mtaa wa Msimbazi Kariakoo ili kurahisisha upatikanaji wa mashine hizo na kutatua changamoto zinazowakabili wafanyabiashara katika matumizi ya mashine hizo.

Katika hatua nyingine, Kayombo alitoa mwito kwa wananchi na wafanyabiashara kujitokeza kuhakiki taarifa zao za usajili wa Namba ya Mlipakodi (TIN) kabla ya Oktoba 15, mwaka huu katika vituo vilivyopangwa na kwamba muda huo hautaongezwa.

“Pamoja na kuhakiki taarifa zao, wafanyabiashara wote ambao hawana TIN nchini wanaombwa kufika katika ofisi ya TRA iliyoko karibu nao ili kujisajili kuepuka kukumbwa na msako unaondelea hivi sasa nchi nzima pamoja na uhamasishaji,” alisema Kayombo.

Aliwataka wamiliki wa vituo vya mafuta kutekeleza agizo la Serikali la kufunga mashine za EFDs kabla au ifikapo Septemba 30, mwaka huu kwani kinyume na hapo ukaguzi utaanza kufanyika kuanzia Oktoba mosi na kusema hatua za kisheria zitachukuliwa kwa wale wote watakaobainika kukiuka agizo hilo.

Alisema katika kuhakikisha kwamba Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) inakusanywa kwa wakati, TRA inawakumbusha walipakodi wote waliosajiliwa VAT kuwasilisha ritani ya kila mwezi kulingana na taratibu zilizowekwa.

Juzi; Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira ilisema inakusudia kuwakutanisha wadau wa Bandari ya Dar es Salaam ili kujadili namna ya kurejesha mizigo ambayo kwa sasa imepungua bandarini. Mwenyekiti wa Kamati hiyo Dk Dalali Kafumu alisema; “Nafikiria ni vizuri tukaenda kwenye mazungumzo ili tuweze kurekebisha. Tuweze kuambiwa ukweli na tupate majibu.

“Sisi tutaitisha mkutano wa pamoja haraka kweli, nchi iko katika hali ambayo si ya kawaida, wakati mwingine kuna mambo mengi sana tunamdanganya Rais (John Magufuli), kwa hiyo tutaitisha mkutano,” alisema Kafumu.

Source: Habari Leo
ZeroDegree.
Bandari Dar yapaisha mapato TRA. Bandari Dar yapaisha mapato TRA. Reviewed by Zero Degree on 9/05/2016 12:15:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.