Loading...

JWTZ wabuni mashine ya kumenya mpunga.

Mashine iliyobuniwa na Mzinga itasaidia kupunguza adha za mpunga mwingi kuingia kwenye pumba hadi kulazimika kupepeta kama wanavyofanya akinamama hawa.
MIKAKATI ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuiwezesha Tanzania kuwa nchi ya viwanda na hatimaye iwe na uchumi wa kati ifikapo 2025. Ili kufikia hatua hiyo, lengo ni kuwa na viwanda vikubwa, vya kati na vidogo vikiwemo vitakavyosaidia kuongeza thamani ya mazao ya kilimo. Katika kuunga mkono juhudi hizo, Shirika la Mzinga la Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) lililopo kwenye Kikosi cha Mazao, Morogoro, limebuni mashine ya kumenya mpunga na kuuweka mchele kwenye madaraja.

Fundi Mchundo, Idara ya Uhandisi katika shirika hilo, Idd Ndui anasema Mzinga imeboresha mashine ya kumenya mpunga na kuongeza mashine ya kuweka mchele katika madaraja ili kuongeza thamani ya zao hilo. Anasema kuuweka mchele kwenye madaraja kutaongeza thamani kwenye mchele sanjari na kuongeza bei ya chakula hicho na hivyo kuwa na kilimo cha mpunga chenye tija.

“Ukiangalia katika bei iliyoko sokoni mchele wa daraja la kwanza unaweza kuuzwa kwa bei kubwa, kwa sababu hiyo kama mkulima anapata soko kwenye ‘supermarket’ au kwa wafanyabiashara wanaouza mchele nje ya nchi anaweza kupata bei nzuri ya kuuza mchele wake na kufidia mchele ambao uko kwenye daraja la pili na la tatu ambao pia ana uwezo wa kuuchanganya na kuuza kwa bei nzuri,” anasema Ndui.

Anasema ikiwa ni tofauti na mashine nyingi za kukobolea mpunga ambazo zinatumia ‘meno ya chuma’ kwa kuwa ubunifu wao umelenga kuumenya badala ya kukoboa, jambo ambalo linafanya mchele ambao haujavunjika kuwa mwingi ukilinganisha na ule uliovunjika.

“Mashine za zamani za kukobolea mpunga ambazo zilikuwa na meno ya chuma ambayo ndiyo yanayotumika pia kukoboa mahindi, mpunga ulikuwa unavunjika sana na wote ulikuwa unaishia kwenye pumba. “Baada ya kuiboresha mashine hii mchele unaotoka bila kukatika unakuwa ni mwingi ukilinganisha na ule uliokatika, hii inatokana na mfumo wa mashine tunazozitengeneza kumenya ganda la mchele bila kuvunjika,” anasema Ndui.

“Kama mkulima atakoboa mpunga wake, basi katika kilo 20 alizokoboa, kilo 18 zinakuwa ni mchele ulio mzima na kilo mbili ni ule uliovunjika, hivyo asilimia 95 ya mchele uliokobolewa unakuwa umenyooka, na hapo atakuwa wameongeza thamani ya mchele wao,” anasema. Ndui anasema mashine hiyo imeongezea mfumo wa kupanga madaraja ya mchele kati ya daraja la kwanza hadi la tatu.

Anasema mwaka 2014, Shirika la Mzinga lilifanya maboresho katika mashine hiyo kwa kuongezea mfumo wa kunyanyua mpunga kutoka chini na kupeleka juu ili kumrahisishia kazi mwendesha mashine. “Hii mashine ni ndefu kwa kwenda juu, mpaka kwenye sehemu ya kuwekea mpunga, lakini baada ya kubuni huu mfumo wa kuweza kubeba mpunga kwenye kibebeo cha chini kabisa na kupandisha kwa juu, hii itasaidia kumpunguzia kazi mtu anayeendesha mashine hiyo,” anasema Ndui.

Anasema, maboresho hayo pia yamepunguza idadi ya watu wanaotakiwa kuendesha mashine hiyo na pia kumsaidia akiwa peke yake kuweza kufanya kazi kwa muda mrefu. “Inapunguza idadi ya watu ambao wanaendesha mashine hiyo kwa sababu awali ilikuwa ni lazima kuwepo na mtu wa kubeba mpunga kutokea chini, mwingine wa kupokea na anayepokea mpunga baada ya kumenywa, hivyo kwa sasa mtu mmoja anaweza kuendesha mashine hiyo tena kwa muda mrefu,” anasema Ndui.

“Hii mashine tuliyoibuni ni kwamba inaweza kuongeza thamani ya zao la mpunga na kufanya mkulima apate faida zaidi kwa kutumia nguvu kidogo kwa sababu ya nyenzo tulizoweka ni rafiki kwake,” anasema. Anasema mpaka sasa Shirika la Mzinga limeuza mashine tatu tofauti hapa nchini na kuwa mashine ambayo imekamilika mpaka kuweka madaraja imeuzwa moja nchini Malawi.

Anasema kwa mashine ambayo wameifunga katika shirika hilo kama mfano imekuwa ikiwanufaisha wakulima wa mpunga kutoka kwenye vijiji vinavyozunguka shirika hilo. “Kwenye shirika tuna mashine moja ambayo imekuwa ikisaidia kuboresha thamani ya mazao ya wakulima wa mpunga katika vijiji vinavyotuzunguka,” anasema Ndui. Mikakati ya baadaye Ndui anasema kwa sasa mashine hiyo ikiwa kamili (yaani na mashine ya kuweka mchele katika madaraja), imekuwa ikitumia umeme na kwamba lengo ni kuiboresha zaidi ili kuweza kutumia mafuta ili kutoa fursa ya kutumika vijijini ambako hakuna umeme.

“Kwa mashine ya kumenya mpunga inaweza kutumika eneo lolote hata kusiko na umeme, lakini ikiwa kamili pamoja na mashine ya kuweka mchele katika madaraja, inahitaji umeme kutokana na kuwa na mota nne. “Hata hivyo tuko katika mikakati ya kuhakikisha tunaiboresha zaidi ili iweze kutumia mfuta na hivyo kuweza kutumika hata vijijini ambako hakuna umeme,” anasema Ndui.

Ushauri Ndui anawashauri wananchi na wawekezaji wakubwa na wadogo kuachana na mtindo wa kukoboa mpunga kwa mashine zenye kutumia meno ya chuma kwa sababu mchele mwingi unapotea kwenye pumba.

Ndui anaomba kupitia taasisi za fedha nchini kuwasaidia mkulima mmoja mmoja au vikundi waweze kununua mashine hizo zitakazosaidia kuongeza thamani ya mchele na hivyo kuinua kilimo cha mpunga. “Naishauri Serikali kupitia taasisi za fedha kuwakopesha wakulima kununua mashine kama hizi zinazopatikana Shirika la Mzinga kwani mashine iliyokamilika tunaiuza kwa Sh milioni 13,” anasema.

ZeroDegree.
JWTZ wabuni mashine ya kumenya mpunga. JWTZ wabuni mashine ya kumenya mpunga. Reviewed by Zero Degree on 9/01/2016 02:51:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.