Loading...

Kanisa kujenga hospitali 10 nchini.

KANISA la Agape WUEMA Sanctuary linatarajia kujenga hospitali 10 nchini, nne zikiwa za rufaa katika mikoa mbalimbali kwa lengo la kuisaidia Serikali kuhakikisha inatoa huduma bora za afya kwa wananchi.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kibaha mwishoni mwa wiki, Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, Martin Bwila, alisema kwa sasa wanaendelea kutafuta viwanja na maeneo kwa ajili ya kuanzisha ujenzi huo kwa kushirikiana na wafadhili kutoka Marekani.

Askofu Bwila alisema kuwa lengo la kujenga hospitali hizo ni kushirikiana na Serikali kumaliza changamoto zinawakabili wananchi katika eneo la huduma muhimu ikiwa ni pamoja na za afya.

"Mbali na kanisa hilo kutoa huduma za kiroho pia linatoa huduma za kijamii kama vile afya elimu, uchumi na makazi ili walengwa waweze kupata huduma bora zinazokidhi mahitaji," alisema Askofu Bwila.

Alisema kuwa kanisa lake litahakikisha linamuunga mkono Rais John Magufuli kwa kuanzisha miradi mbalimbali ili kuifanya Tanzania mpya inayoongozwa na kiongozi anaye mpenda Mungu.

"Matarajio yetu ni kuanzisha miradi mikubwa nchini na kuifanya Tanzania kuwa nchi yenye viwanda na uchumi unaokuwa kama Rais alivyosema kuwa tunataka kufikia uchumi wa kati. Ujenzi tutakaoufanya ni pamoja na wa Bandari ya Majini na nchi Kavu," alisema Askofu Bwila.

Askofu Bwila ambaye pia ni Makamu Askofu Mkuu wa Afrika Mashariki katika kanisa hilo, alisema kuwa kwa sasa Tanzania imeweza kuaminika na kutunukiwa cheti maalumu kuwa nchi ya 68 duniani kwa uadilifu na uchapakazi.

Alisema kwa sasa wapo kwenye mchakato wa kuwasiliana na wizara mbalimbali kwa ajili ya kupata vibali ili kufanya shughuli hizo kisheria.

Alisema wanaomba ardhi kwa ajili ya uwekezaji huo na kwamba hadi sasa wana ekari 14,000 katika maeneo mbalimbali nchini, ambayo ni pamoja na Dodoma ambako itajengwa hospitali ya rufaa," alisema.

Naye Mwenyekiti wa Kanisa hilo mkoani Pwani, Askofu Ezra Meena, alisema kuwa wamejipanga kuanza maandalizi ya ujenzi yanayotarajiwa kuanza mwishoni mwa mwaka huu, ikiwa ni pamoja na nyumba za watumishi na huduma za kijamii.

Askofu Meena alisema kuwa mbali ya huduma hizo za kijamii pia watahakikisha wanawawezesha watu kiuchumi hasa wale wanaoishi kwenye mazingira magumu.

Alisema kwa upande wa elimu watahakikisha kuwa wanajenga shule kuanzia ngazi ya awali hadi elimu ya juu, lengo likiwa kuhakikisha elimu bora kwa watoto. Alisema huduma zitatolewa bila kujali dhehebu la anayehudumiwa.

Credits: Habari Leo
ZeroDegree.
Kanisa kujenga hospitali 10 nchini. Kanisa kujenga hospitali 10 nchini. Reviewed by Zero Degree on 9/26/2016 08:57:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.