Loading...

Manji anogesha mechi ya Yanga na Simba, ..aikabidhi Yanga ekari 712 kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja wa kisasa.

HATIMAYE Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji, amekata mzizi wa fitina baada ya kuikabidhi klabu hiyo eneo la ukubwa wa ekari 712 lililopo kandokando ya Bahari ya Hindi, Kigamboni, jijini Dar es Salaam ili kujenga uwanja wa kisasa wenye hadhi ya kimataifa.

Jiwe la msingi la eneo hilo lilizinduliwa jana na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba ambaye alitamba kuwa zawadi hiyo kwa wana-Yanga ni chachu ya ushindi wa kishindo katika mchezo kati ya timu yao na watani wao wa jadi, Simba, utakaochezwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Akizungumza kabla ya uzinduzi huo, Nchemba alimpongeza Manji kwa uamuzi wake huo akiamini sasa atakuwa amekata kiu ya wana-Yanga ya kuwa na uwanja wao wa kisasa.

Alisema kuna wakati alikutana na kiongozi huyo wa Yanga na kumtaka kufanya kila linalowezekana kuitafutia klabu hiyo eneo la kujenga uwanja Kigamboni na kuachana na mpango wa kuukarabati Uwanja wa Kaunda ambao Serikali imegoma kutoa kibali cha kuuendeleza kwa kuwa upo kwenye mkondo wa maji.

“Nilipokutana na mwenyekiti nilimwambia wakati wenzetu wanawaza kwenda Bunju, sisi twende Kigamboni, nimefurahi amelitimiza hilo, huku vitimu vya ajabu ajabu vikija, vinashangaa shangaa tu bahari na kupigwa mabao,” alisema huku akishangiliwa na viongozi na wapenzi wachache wa klabu hiyo waliohudhuria hafla hiyo ya uzinduzi.

Alisema kwa hali ilivyo kwa sasa kwenye soka, hakuna ujanja wowote wa kuiendesha klabu zaidi ya kuhakikisha inakuwa na nyenzo zote muhimu kama uwanja wa kisasa na vitega uchumi, hivyo zawadi hiyo ya Manji ni vema ikaenziwa na wana-Yanga wote popote walipo.

Akizungumza kabla ya kumkaribisha Waziri Nchemba, Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini ya Yanga, Mama Fatma Karume, alisema baada ya kujulishwa na Manji juu ya mpango wake wa kuwakabidhi eneo hilo kwa ajili ya kujenga uwanja, walifarijika mno wakifahamu hilo litawawezesha kuifanya klabu yao kujiendesha kisasa zaidi, akiahidi mchakato wa ujenzi kuanza punde.

“Tunashukuru hatimaye mwenyekiti wetu ametimiza ahadi yake na hii ni zawadi kubwa mno kwa wana-Yanga sasa tushindwe wenyewe,” alisema Mama Karume aliyekuwa ameongozana na mjumbe mwingine wa bodi hiyo, Jabir Katundu, Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Baraka Deusdedit, wajumbe wa Kamati ya Utendaji na baadhi ya wanachama wao.

Awali akikabidhi eneo hilo, Mkurugenzi wa Village Investment aliyemwakilisha Manji, Konstantinos Vasileiadis, alisema kuwa wametoa zawadi hiyo kwa Yanga kutokana na mapenzi aliyonayo mfanyabiashara huyo kwa klabu hiyo.

“Eneo hili ni kubwa sana, kunaweza kujengwa viwanja vingi tu vyenye ubora wa hali ya juu kama vile vya UIaya pamoja na vitega uchumi,” alisema.

Naye Diwani wa Kata ya Kigamboni, Dotto Mzawa, alisema Yanga wana bahati mno kupata eneo kubwa kama hilo lililopo Gezaulole ambalo pia lipo kando kando ya barabara.

Awali, Yanga ilikuwa katika mpango wa kuujenga upya uwanja wao wa Kaunda uliopo makao makuu ya klabu hiyo yaliyopo kwenye makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam, lakini Serikali iligoma kutoa kibali cha ujenzi kwa kuwa eneo hilo lipo katika mkondo wa maji.

Kwa kufanikiwa kupata eneo hilo la kujenga uwanja, Yanga itakuwa imeipiga bao Simba ambao wamekuwa wakiringia eneo lao lililopo Bunju, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam ambalo hata hivyo si kubwa kama watani wao wa jadi.

Yanga na Simba zinatarajiwa kuvaana Jumamosi katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Taifa, mchezo unaotarajiwa kuwa na upinzani wa hali ya juu.


Credits: Bingwa
ZeroDegree.
Manji anogesha mechi ya Yanga na Simba, ..aikabidhi Yanga ekari 712 kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja wa kisasa. Manji anogesha mechi ya Yanga na Simba, ..aikabidhi Yanga ekari 712 kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja wa kisasa. Reviewed by Zero Degree on 9/29/2016 12:48:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.