Loading...

Njia 11 za kudhibiti ajali barabarani zapendekezwa.

KATIKA kuadhimisha Wiki ya Nenda kwa Usalama, Chama cha Kutetea Abiria Tanzania (Chakua), kimetoa mapendekezo 11 kwa serikali ambayo yanapaswa kutekelezwa ili kupunguza ajali za barabarani.

Moja ya mapendekezo hayo ni maadhimisho kufanyika mara kwa mara badala ya mara moja kwa mwaka kama ilivyo sasa.

Akizungumza na Nipashe jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Chakua, Francis Mugasa, alisema ili serikali iweze kutokomeza ajali, inapaswa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa kufikia mafanikio na kukuza uchumi.

Alisema Mamlaka za Usimamizi wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra), Bima, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Zimamoto na Uokoaji kwa kushirikiana na Chakua, zifanye ukaguzi endelevu wa vyombo vyenye usajili wa kusafirisha abiria, sambamba na kutoa elimu.

Alisema pia mamlaka za usimamizi abiria kutotumia vyombo ambavyo havijasajiliwa kusafirisha abiria kama vile ‘pick up’ na malori.

“Kwa maana imezoeleka kuona wafuasi wa vyama vya siasa, washabiki wa mpira, wafanya kazi wa taasisi za ujenzi, mazishi, wafuasi wa dini na ngoma kutumia usafiri huo ambao ni hatarishi,” alisema Mugasa.

Alitaja pendekezo lingine kuwa ni serikali inapaswa kupiga marufuku magari ya kusafirishia abiria kusafirisha ndege hai, bidhaa za milipuko kama vile mitungi ya gesi, mkaa na pikipiki.

Alisema Chakua pia inaishauri serikali kukagua mizigo pamoja na kuweka vifaa vya ukaguzi ili kujiridhisha usalama na mizigo yote inayoingia vituo vya mabasi, stesheni za reli na vivuko kwa kuwa utafiti unaonyesha mizigo inakuwa na vitu hatarishi katika vituo vyote vya mabasi.

Alisema serikali pia inapaswa kuunga mkono Chakua katika mpango wa kuweka mfumo wa tiketi wa kielekroniki, kwa kufanya hivyo itaondoa ulanguzi wa tiketi na wapiga debe katika vituo vya mabasi.

Pendekezo lingine ni watoa huduma kutoa risiti zenye vielelezo muhimu na kuboreshwa kwa nyongeza endapo ikitokea dharura ili ajulishwe ndugu wa karibu wa abiria.

Alisema pia kunatakiwa kuwe na utaratibu wa madaraja ya mabasi uliohakikiwa na uendane na namba ya usajili wa gari husika na namba za Chakua, pamoja na vituo vya vyombo ya kusafirisha abiria lazima vikidhi miundombinu ya kuwezesha walemavu kusafiri.

Alisema vyombo vya kusafiria abiria kwa njia ya maji, pia lazima vikidhi masharti ya vifaa vya usalama na kujiokolea na ujazo uendane na uwezo wa chombo.

Mugasa alisema ulipaji fidia kwa waathirika wa ajali, uwe wazi na mamlaka husika itoe elimu kwa wananchi pamoja na kutolewa kwa adhabu kwa abiria wanaokiuka taratibu za usalama barabarani.

ZeroDegree.
Njia 11 za kudhibiti ajali barabarani zapendekezwa. Njia 11 za kudhibiti ajali barabarani zapendekezwa. Reviewed by Zero Degree on 9/27/2016 08:01:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.