Loading...

Papa Francis amtangaza Mama Teresa wa Calcutta kuwa mtakatifu.

Mama Teresa.
Mtawa ambaye huduma zake kwa wagonjwa na jamii masikini katika jiji la Calcutta, India zilimpatia umaarufu duniani na kumjengea taswira ya Upendo wa Kikristo, ametangazwa kuwa mtakatifu katika sherehe iliyoendeshwa na Papa Francis mjini Vatican jana.

Kutangazwa kwake katika hadhi hiyo ya juu katika Ukatoliki, kulifanywa katika ibada ya MIsa Takatifu kwenye viwanja vya Mtakatifu Petro na kuhudhuriwa na waumini wapatao 100,000.

“Kwa heshima ya Utatu Mtakatifu, tunatangaza na kumfanya Mbarikiwa Teresa wa Calcutta kuwa Mtakatifu na tunamjumuisha miongoni mwa watakatifu,” alisema Papa.

Kwa sababu hiyo, kuanzia jana, Mama Teresa ambaye alitangazwa kuwa mwenye heri Oktoba 19, 2003 na marehemu Papa Yohane Paulo II, atajulikana kama Mtakatifu Teresa wa Calcutta.

Sherehe hiyo iilifanyika siku moja kabla ya maadhimisho ya 19 ya kifo chake mjini Calcutta, jiji alilolitumikia karibu miongo minne akiwahudumia masikini.

Hata hivyo, baadhi ya wasaidizi waliokuwa pamoja naye, wamejitokeza na kueleza jinsi baadhi ya watu hao masikini walivyodhulumiwa hata kutelekezwa hadi kufa.

Lakini pia wakosoaji wengine wanadai Mama Teresa aliyefariki dunia mwaka 1997 akiwa na umri wa miaka 87, alitumia udhaifu wa watu hao kujaribu kuwabadili dini, hasa watu masikini wa madhehebu ya Hindu, kuwa Wakristo.

Akiwa amezaliwa Macedonia wakati ikijulikana kama Albania Agosti 26, 1910, kazi zake za misheni zilimwezesha kunyakua Tuzo ya Amani ya Nobel na alianzisha Shirika la Masista Wamisionari wa Upendo kuwasaidia walala hoi katika mtaa wa mabanda wa Calcutta.

Wachambuzi wa mambo wanasema maisha yake yanaenda sambamba na maono ya Papa Francis kuhusu kanisa linalojikakamua kuwasaidai watu masikini.

“Tunahisi kupandishwa ngazi kwake na kuwa mtakatifu kutachochea watu zaidi kujitolea kuwasaidia wasiojiweza katika jamii,” alisema Askofu Thomas D’Souza anayesimamia shughuli za kimishenari mjini humo.

Lakini pia mamilioni ya waumini wa Kanisa hilo kote duniani wameeleza furaha yao kwamba hatimaye mchango wake wa kuwasaidia watu maskini umetambuliwa.

Sherehe za ibada maalum pamoja na matukio mengine zilifanyika kote India kusherehekea hatua ya kutangazwa kuwa Mtakatifu Mama Theresa.

Mamia ya waumini walikusanyika makao makuu ya taasisi yake ya misheni katika mji huo wa Calcutta mashariki mwa India.

Rais wa India, Pranab Mukherjee, amemtaja mtawa huyo kuwa ni masiha wa watu masikini na nguzo ya kuwasaidia waliodhaifu na wanaoishi katika mateso.

Mkazi wa mji huo, Gutam Lewis alisema bado anamkumbuka, hasa baada ya kumsaidia kukabiliana na ugonjwa wa polio alipofiwa na wazazi wake.

“Mama Teresa alikuwa akinibeba kwenda kanisani kila Jumapili. Pia alihakikisha napata matibabu kwa njia inayofaa.

“Ni kupitia fadhila zake niliweza kukabiliana na maradhi ya polio ambayo yalinishika nikiwa na umri wa miaka miwili,” anasema Lewis, ambaye kwa sasa anafanya kazi ya urubani mjini London, Uingereza.

“Nilihisi usalama wa kutosha nikiwa naye,” anasema rubani huyo mwenye umri wa miaka 39.

Uamuzi wa kumfanya Mama Teresa kuwa mtakatifu ulipitishwa na makao makuu ya Kanisa Kanisa mwaka jana baada ya muujiza wa pili kutokea, ikiwa ni moja ya masharti kwa kila mtu anayestahili kuwa mtakatifu.

Muujiza huo unamhusu mwanamume mmoja raia wa Bengal, aliyekuwa na vidonda ndani ya ubongo ambaye maombi ya marehemu anasema yalichangia kupona kwake.

Hata hivyo, Dk. Aroup Chatterjee, alimtaja marehemu kama “aliyelenga kueneza imani yake kwa njia zozote.”

“Ni vipi mtu anaweza kumwombea mgonjwa anayekaribia kufa bila kumpa msaada wa matibabu anayohitaji?” alihoji msomi huyo ambaye amekuwa mkosoaji wake mkubwa.

Mama Teresa pia alikuwa akikosolewa vikali na mwandishi Christopher Hitchens kutoka Uingereza, aliyemtaja kama ‘aliyeendeleza mateso dhidi ya maskini kwa kisingizio cha kuwasaidia.’

Baadhi ya wakosoaji wake wamedai ufujaji wa fedha licha ya kupokea michango mingi ya kuwasaidia watu maskini.


ZeroDegree.
Papa Francis amtangaza Mama Teresa wa Calcutta kuwa mtakatifu. Papa Francis amtangaza Mama Teresa wa Calcutta kuwa mtakatifu. Reviewed by Zero Degree on 9/05/2016 11:15:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.