Loading...

Raisi Magufuli asali katika kanisa la Anglikana.

BAADA ya kuomba Mungu kwenye dhehebu lake la Roma, kuingia Kanisa Kuu la Azania la KKKT na (GRC), Rais John Magufuli jana aliungana na waumini wa Kanisa la Anglikana la Mtakatifu Albano jijini Dar es Salaam kusali ibada ya Jumapili, kuadhimisha Siku ya Bwana ya 19 baada ya Penteko.

Akizungumza na waumini wa kanisa hilo baada ya kumalizika kwa ibada, Rais aliyeongozana na mkewe, Janeth, aliwashukuru viongozi na waumini wa Kanisa la Anglikana na madhehebu mengine ya dini nchini kwa kuendelea kuliombea taifa na kudumisha amani na utulivu.

Rais alisema viongozi wa dini wanafanya kazi kubwa na muhimu katika taifa na kwamba Watanzania wote bila kujali dini zao, itikadi za kisiasa, makundi na kanda zao, wana wajibu wa kuungana na viongozi hao ili nia hiyo njema iendelee kufanikiwa.

“Ninawashukuru kwa sababu mmeendelea kuliombea taifa, ninawashukuru kwa sababu siku zote mmekuwa mkipiga magoti na kumtanguliza Mungu mbele, ninawashukuru kwa sababu mnaendelea kuombea amani ya nchi yetu na upendo udumu ndani yetu sisi sote,” alisema.

"Makanisa yote, madhehebu, dini zote na vyama vyote, upendo tukiujenga ndiyo tutaiendeleza vizuri Tanzania yetu,” alieleza zaidi Rais Magufuli.

Kwa upande wake, Padre Jackson Sostenes aliyeongoza ibada hiyo, alimshukuru Rais Magufuli kwa kuungana na waumini wa kanisa hilo katika ibada ya Jumapili na kuahidi kwamba viongozi na waumini wa kanisa hilo wataendelea kumuombea na kuliombea taifa.

Katika ibada hiyo, Rais Magufuli alitoa Sh. milioni moja kwa ajili ya kuchangia vikundi vya kwaya ya kanisa hilo.

Rais Magufuli alihudhuria ibada ya Pasaka Kanisa la KKKT la Azania Front jijini Dar Es Salaam Machi 27, mwaka huu.

Aidha, Juni 5 Rais Magufuli alisali katika Kanisa la Maombezi (GRC) Ubungo-Kibangu, jijini Dar es Salaam Juni 5 na kuahidi kutengeneza njia inayokwenda katika kanisa hilo linaloongozwa na Mchungaji Anthony Lusekelo, kutokea Barabara ya Nelson Mandela. 

Kabla na baada ya kuingia katika madhehebu hayo, Rais Magufuli amesali katika parokia za Roma katika miji mbalimbali, ikiwamo Mtakatifu Petro, Oysterbay jijini na Chato mkoani Geita.

ZeroDegree.
Raisi Magufuli asali katika kanisa la Anglikana. Raisi  Magufuli asali katika kanisa la Anglikana. Reviewed by Zero Degree on 9/26/2016 01:30:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.