Loading...

Risasi zarindima makao makuu CUF.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF, Julius Mtatiro, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, kuhusu mambo mbalimbali ya kisiasa nchini.
JESHI la Polisi limelazimika kufyatua risasi hewani kuwatawanya wafuasi wa CUF wanaodaiwa wapambe wa aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba, baada ya jana kufika kwenye ofisi za chama hicho zilizopo Buguruni jijini Dar es Salaam wakipinga kusimamishwa uanachama kwake.

Aidha, huku wafuasi hao wakitawanywa na polisi, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imesema itawakutanisha Prof. Lipumba na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, kwa lengo la kuzungumza kilichotokea hadi kufikiwa uamuzi wa kufutwa na kusimamishwa uanachama kwa baadhi ya viongozi wa chama hicho akiwamo mtaalamu huyo wa uchumi. 

Hii ni mara ya pili vurugu kutokea zikihusisha wafuasi wa CUF baada ya Agosti 21, mwaka huu kuvunjika kwa mkutano wa uchaguzi wa nafasi za Mwenyekiti na Makamu wake baada ya wanaodaiwa kuwa wafuasi wa Prof, Lipumba kuzusha vurugu wakitaka arejeshwe katika nafasi yake ya Uenyekiti aliyojiuzulu mwaka jana.

Wafuasi hao wa Prof. Lipumba walifika kwenye ofisi hizo majira ya saa 4:00 asubuhi kabla ya kufanyika kwa mkutano baina ya viongozi wa chama hicho na waandishi wa habari wakitaka kufanyike maridhiano kati ya Prof. Lipumba na uongozi wa chama hicho ambacho wiki iliyopita kilitangaza kumsimamisha uanachama mtaalamu huyo wa uchumi.

Baadhi ya mashuhuda wa tukio la polisi kuwatawanya wanachama hao kwa risasi jana waliliambia Nipashe kuwa majira ya saa 4:00 asubuhi, waliona gari la polisi linaingia katika ofisi hizo na baada ya muda mfupi waliona anatoka kijana mmoja aliyekuwa ameingia ndani ya ofisi hizo akitolewa na polisi kwa nguvu na kukimbilia katikati ya wafanyabiashara wa soko la Buguruni.

Mussa Abdallah, mmoja wa mashuhuda hao, alisema kijana huyo alitoka ndani ya ofisi hizo huku akikimbizwa na askari hao huku baadhi ya wafuasi hao wanaodaiwa wa Prof. Lipumba wakionekana kuwa wageni kwa wenyeji wa maeneo hayo.

Abdallah alisema wafuasi hao waliokuwa wamezagaa kwenye maeneo ya karibu na ofisi hizo, walikuwa wamevaa nguo za kawaida.

Alisema baada ya polisi kutoka nje wakimkimbiza kijana huyo kutoka ndani ya geti la ofisi za chama hicho, walipiga risasi mfululizo juu na kusababisha mshtuko kwa wakazi wa maeneo hayo ambao walianza kukimbia ovyo kujiokoa huku baadhi wakitelekeza biashara zao.

Mmoja wa mama lishe anayefanya biashara zake karibu na ofisi hizo ambaye hakupenda jina lake litajwe katika gazeti, alisema kuwa baada ya polisi kupiga risasi, alilazimika kukimbia na kuacha chakula chake.

"Kiukweli 'mtiti' uliokuwapo hapa huwezi kubaki na hata kama ni wewe usingebaki. Kwanza, kabla ya hapo tuliona polisi wamekuja wakaingia ndani na baada ya muda kidogo tunaona kijana mmoja anatoka anakimbilia katikati ya watu na ndipo polisi wakapiga risasi. Baada ya risasi hizo, hatukujua kilichoendelea maana kila mtu alikimbia kujiokoa," alisema.

Nipashe ilishuhudia gari la polisi likiwa limepiga kambi nje ya geti la ofisi za CUF huku askari wawili waliokuwa wamevaa nguo za kiraia wakiwa na silaha wakionekana kuimarisha ulinzi kwenye ofisi hizo.

Wakati hayo yanaendelea katika ofisi za CUF, watu wapatao 50 waliodai ni wanachama wa chama hicho, walikuwa wamesimama kwenye kona ya barabara ya kuelekea kwenye ofisi za chama hicho na walipofuatwa na gazeti hili, walikiri kuwa waliamua kufika kwenye ofisi za chama hicho kwa lengo la kutafuta ufumbuzi wa mvutano unaoendelea baina Profesa Lipumba na uongozi wa chama hicho.

"Ndiyo, sisi ni wawakilishi wa wanachama wa CUF na wengine wametoka nje ya Dar es Salaam, tumekwenda pale tena kwa nia nzuri, lengo letu tunataka uongozi utoe tamko juu ya sintofahamu inayoendelea hivi sasa na kikubwa zaidi tunataka maridhiano yafanyike kati ya Profesa Lipumba na uongozi wa chama," alisema Amini Juma Abdalla, mmoja wa watu hao.

Aliongeza kuwa kijana aliyeingia ndani ya ofisi hizo na kutoka huku akifukuzwa na askari polisi, walituma kuwawakilisha kwa uongozi wa chama hicho kuhusu maombi yao hayo na kwamba kabla ya kufika kwa uongozi, polisi waliingia ndani na kumtoa.

KAULI YA UONGOZI CUF

Katika mkutano na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi wa CUF, Julius Mtatiro, alipoulizwa juu ya ujio wa askari kwenye ofisi hizo, alisema hatambui uwapo wao na kwamba kuwepo kwao huenda ilikuwa sehemu ya utekelezaji wa majukumu yao ya ulinzi wa raia na mali zao.

"Ndiyo nasikia taarifa kutoka kwako kuwa polisi wako nje na kwamba wamepiga risasi, mimi nilikuwa ndani sijasikia chochote na labda inawezekana wako katika kazi zao za kawaida. Lakini nikwambie kwamba ofisi yetu inalindwa na askari wetu wa chama," alisema Mtatiro.

Awali katika mkutano huo na waandishi wa habari, Mtatiro alizungumzia kauli mbalimbali zilizozungumwa na Rais John Magufuli juzi visiwani Zanzibar ikiwamo ya kumtaka Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, kuacha kusaini posho za aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif kutokana na kitendo cha wawili hao kutopeana mikono wakati wa mazishi ya aliyekuwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mzee Aboud Jumbe hivi karibuni.

Mtatiro alisema stahiki zote anazopewa Maalim Seif zipo kisheria kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano na Katiba ya Zanzibar.

Alisema stahiki anazopewa kiongozi huyo zinatokana na kuwa kiongozi mstaafu wa nchi.

"Stahiki hizo si za hisani inayotoka mfukoni mwa kiongozi yeyote, ni fedha za Watanzania zinazotokana na makusanyo ya kodi zinazolipwa na wananchi," alisema Mtatiro.

LIPUMBA, MAALIM SEIF USO KWA USO

Katika hatua nyingine, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imewataka kufika katika ofisi zake Prof. Lipumba na Maalim Seif ili itoe uamuzi kuhusu malalamiko yaliyotolewa na Profesa Lipumba dhidi ya Katibu Mkuu huyo wa CUF.

Imeelezwa kuwa viongozi hao watatinga kwenye ofisi hizo zilizopo jijini Dar es Salaam siku yoyote kuanzia leo ili kusikiliza uamuzi wa madai yaliyowasilishwa Agosti 29, mwaka huu ofisini hapo na Prof. Lipumba.

Katika barua yake kwa Msajili wa Vyama vya Siasa aliyoiwasilisha kwa mikono yake siku hiyo, Profesa Lipumba alilalamika kung’olewa uenyekiti wa CUF huku ofisi hiyo nayo iliandika barua kwenda kwa Katibu Mkuu wa CUF (Maalim Seif) ikitaka aeleze hatua alizopitia hadi kufikia uamuzi wa kumvua uenyekiti na kumsimamisha uanachama msomi huyo.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano katika ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Monica Laurent, katika mahojiano na Nipashe jijini Dar es Salaam jana, alisema kuwa juzi ofisi hiyo ilipokea barua kutoka kwa Maalim Seif, iliyomjibu Msajili wa Vyama na kisha kikao cha ndani kukaa na kuijadili barua hiyo.

Laurent alisema uongozi wa CUF ulijibu barua hiyo kwa wakati na kwamba kinachosubiriwa ni kuzikutanisha pande zote zinazohusika katika mvutano huo.

Alisema ofisi hiyo haiingilii masuala ya ndani ya vyama vya siasa, lakini vyama vinatakiwa kufuata taratibu, kanuni na katiba zake katika kujiendesha na kufanya uamuzi wa masuala mbaliambali.

Katika madai yake, Profesa Lipumba anasema yeye ndiye mwenyekiti halali wa CUF licha ya Baraza Kuu la Taifa la chama hicho kutangaza kumsimamisha uanachama pamoja wenzake 10 akiwamo Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara, Magdalena Sakaya.

Uamuzi huo ulichukuliwa siku chache baada ya Mkutano Mkuu Maalumu wa CUF kuvunjika jijini Dar es Salaam kutokana na vurugu za wafuasi waliodaiwa kuwa wa Profesa Lipumba.

Wafuasi hao walilazimisha kuingia ukumbini ulimokuwa unafanyika mkutano huo, Agosti 21, mwaka huu na kupinga uamuzi waliouita wa kura za kutengenezwa za kuridhia kuondoka kwa mwenyekiti wao aliyejiuzulu katika nafasi yake mwaka jana.

Source:Nipashe
ZeroDegree.
Risasi zarindima makao makuu CUF. Risasi zarindima makao makuu CUF. Reviewed by Zero Degree on 9/05/2016 08:45:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.