Loading...

Wabunge 11 wasababisha Bunge kumalizika saa 5 ya usiku.

Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson.
BUNGE lililazimika kufanya kazi hadi saa 5:24 usiku wa juzi baada ya wabunge 11 kutaka baadhi ya vifungu kwenye miswada miwili iliyokuwa inajadiliwa vibadilishwe.

Awali, Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola alilishauri Bunge kutupa moja ya miswada hiyo akidai ni hatari kwa maendeleo ya taifa.

Katika kikao cha juzi kilichoongozwa na Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson, Bunge lilikuwa linajadili miswada miwili - Sheria ya Kuanzishwa kwa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali na Sheria ya Kuanzishwa kwa Baraza la Wanataaluma wa Kemia.

Baada ya kurejea saa 11:00 jioni kuendelea na shughuli za Bunge zilizositishwa saa 7:00 kwa ajili ya chakula cha mchana, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alianza kujibu hoja zilizoibuliwa wakati wa mjadala wa miswada hiyo ulioanza Ijumaa, lakini muda wa kawaida wa chombo hicho haukutosha kutokana na wabunge hao 11 kutaka ufafanuzi wa mambo mbalimbali yaliyokuwa kwenye miswada hiyo.

Hali hiyo iliyoulazimu upande wa serikali kuomba kutengua Kanuni ya 28 ya Bunge ili kuongeza muda wa kikao cha Bunge kuhakikisha mjadala wa miswada hiyo inakamilika.

Kanuni ya 28 inataka kikao cha jioni cha Bunge kimalizike saa 1:45 jioni, lakini baada ya ombi hilo la serikali lililotolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Angela Kairuki, Naibu Spika aliridhia hoja hiyo na kusema: "Leo tunakesha."

Ilionekana mapema kuwa kikao hicho kingemalizika usiku mwingi baada ya Lugola kusimama na kulishauri Bunge liutupe Muswada wa Sheria ya Kuanzisha Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa maelezo kuwa katika kifungu chake cha kwanza umetambulishwa kwa jina la muswada wa sheria ya serikali badala ya kuwa muswada wa sheria ya nchi.

Mbunge huyo pia aliwaomba watunga sheria wenzake wamuunge mkono, lakini baada ya kuhojiwa, hoja yake ilitupwa kutokana na kuungwa mkono na wabunge wachache.

Ingawa kulikuwa na wabunge zaidi ya 100 kwenye ukumbi wa Bunge, ni wabunge 11 walioijadili wakiwamo Halima Mdee (Kawe), Dk. Godwin Mollel (Siha), Mwita Waitara (Ukonga), Esther Matiko (Tarime Mjini), Devotha Minja (Viti Maalum) na Lucy Owenya (Viti Maalum) wote kutoka Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliochangia ni Amina Mollel (Viti Maalum), Balozi Adadi Rajab (Muheza), Profesa Anna Tibaijuka (Muleba Kusini) na Andrew Chenge (Bariadi Magharibi).

Wabunge hao walisimama mara kadhaa na kuomba kufanyika kwa marekebisho na kufuta baadhi ya maneno kwenye vifungu na vingine kuvifuta kabisa.

Aidha, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Walemavu), Dk. Possi Abadallah na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju walilazimika kusimama mara kwa mara kutoa ufafanuzi wa baadhi ya vifungu vilivyopendekezwa kufutwa, kuboreshwa au kuingizwa kwenye miswada hiyo.

Kutokana na mvutano huo wa kisheria, muswada wa kuanzisha Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ulipitishwa na Bunge saa 4:10 usiku wakati Sheria ya Kuanzisha Baraza la Wanataaluma wa Kemia ulipita saa 5:18.

Naibu Spika aliahirisha shughuli za Bunge saa 5:24 usiku.

Katika Bunge lililopita, kikao cha Bunge kililazimika kufanyika hadi usiku mwingi wakati wa kujadili sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow lililowang'oa mawaziri kadhaa kwenye Baraza la Mawaziri.

Miongoni mwa mambo ambayo wabunge wa Chadema walitaka yafutwe kwenye miswada hiyo ni wajumbe wa Bodi ya Baraza la Wataalamu wa Kemia kuwekewa kinga ya kutoshtakiwa na kigezo cha kuwa mtumishi wa umma ili uteuliwe kuwa Mkemia Mkuu wa Serikali.

Wakiongozwa na Mdee, wabunge hao pia walipinga kifungu cha adhabu ya kuanzia kifungo cha miaka mitano jela na faini kwa mtu atakayepatikana na hatia ya kukiuka Sheria ya Kuanzishwa kwa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali.

Mdee alipendekeza adhabu iwe kifungo kisichopungua mwaka mmoja, lakini kisizidi miaka mitano pendekezo ambalo lilitupwa na serikali kwa madai kuwa lengo la adhabu kali hiyo ni kudhibiti watu wanaohatarisha taifa kutokana na kuharibu kumbukumbu muhimu, zikiwamo alama za vidole vya makundi ya wagaidi.

Credits: Nipashe
ZeroDegree.
Wabunge 11 wasababisha Bunge kumalizika saa 5 ya usiku. Wabunge 11 wasababisha Bunge kumalizika saa 5 ya usiku. Reviewed by Zero Degree on 9/15/2016 10:05:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.