Loading...

James Rodriguez atishiwa kuuawa na watu wasiojulikana nchini Colombia.


KUNA mambo ya kutaniana lakini sio kifo. Hali sio nzuri kwa staa Real Madrid, James Rodriguez baada ya kutishiwa kuuawa na watu wasiojulikana nchini kwao Colombia kufuatia kitendo chake cha kujitoa katika kikosi cha timu ya taifa.

Rodriguez alijitoa katika pambano muhimu la kufuzu fainali za Kombe la Dunia nchini Russia 2018 dhidi ya Uruguay kutokana na kuwa majeruhi, lakini kuna mashabiki wanaamini staa huyo amejilegeza tu.



Shirikisho la Soka la Colombia lilitangaza kuwa staa huyo atalikosa pambano gumu dhidi ya Uruguay baada ya kulikosa lile la Paraguay Jumamosi ambalo walishinda 1-0, lakini kocha Nestor Pekerman alikuwa ana matumaini kuwa Rodriguez angerudi katika pambano dhidi ya Uruguay.

Hata hivyo, aliumia kiazi chake cha mguu wakati akipasha moto misuli yake kabla ya pambano la Real Madrid dhidi ya Eibar, lakini alijiunga na kikosi cha timu yake ya taifa akisikilizia majeraha yake. 

Mama wa James, Pilar Rubio ameripoti Polisi kuwa mwanae ametumiwa meseji mbaya ya kifo na mashabiki wenye hasira huku wakieneza ujumbe kwamba, ‘James ni fedheha ya taifa’ na ujumbe huo umekuwa ukizunguka sana.

Ujumbe huo umeandika “Nasafiri kwenda nyumbani kwako nikiwa na silaha, sema kwaheri kwa wote unaowapenda,” ulisema ujumbe huo ukiwa kando yake ukiwa na picha ya bastola pamoja na risasi ikiashiria ukweli ndani yake. Ujumbe mwingine wenye kutishia maisha ya Rodriguez uliandikwa “Kesho nitawaona watu wote hawa wakilia kwa sababu nimemuua mchezaji mpuuzi.” 

Ujumbe huo pia uliwekwa nembo maalumu ya kundi la Legion Holk ambalo ni kundi la wahuni linalojulikana sana kwa kuwashambulia watu maarufu. Mama wa James pia ametumiwa meseji mbalimbali za vitisho vya kuuwa kwa mwanae, ambaye aling’ara katika michuano ya kombe la dunia nchini Brazil 2014 kiasi cha kununuliwa na Real Madrid kwa dau la pauni 60 milioni akitokea Monaco ya Ufaransa.



“Hawa watu wana nini jamani? Wana kichaa? Wamenitumia ujumbe wakisema itakuwa vizuri nikimuona mwanangu amekufa,” alilalamika mama wa staa huyo. Polisi nchini Colombia hawajavichukulia vitisho hivyo kama vya kawaida kufuatia historia chafu ya mauaji nchini humo. 

Mwaka 1994, siku tano baada ya kutolewa katika fainali za kombe la dunia nchini Marekani, staa wa soka wa nchi hiyo, Andres Escobar, 27 aliuawa na shabiki wa soka kwa madai ya kuifungisha na kuitoa nchi hiyo katika michuano hiyo.

Escobar alijifunga bao hilo Juni 22, 1994 katika pambano muhimu la makundi dhidi ya Marekani, ambapo Marekani ilishinda 2-1 kwa bao la ushindi la kujifunga kwa Escobar na baadhi ya mashabiki walikerwa na bao hilo kufuatia matumaini makubwa waliyokuwa nayo kwa timu yao ya taifa ambayo ilitolewa hatua ya makundi kwa kichapo hicho.

Aliuawa Julai Mosi, 1994 ikiwa ni siku tano tu baada ya kutolewa kwa Colombia katika michuano hiyo baada ya kikosi hicho kurudi nyumbani ambapo, alikwenda katika klabu ya usiku ya El Poblado mjini Medellín na kupigwa risasi katika eneo la maegesho ya magari.

Colombia kama zilivyo kwa nchi nyingine za Amerika Kusini imekuwa na vitendo vya uhalifu vya huku mashabiki wengi wakiwa wehu wa soka.

ZeroDegree.
James Rodriguez atishiwa kuuawa na watu wasiojulikana nchini Colombia. James Rodriguez atishiwa kuuawa na watu wasiojulikana nchini Colombia. Reviewed by Zero Degree on 10/12/2016 09:35:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.