Loading...

Kupiga picha wagonjwa wodini marufuku.

SERIKALI mkoani Ruvuma imepiga marufuku upigaji picha kwa wagonjwa waliolazwa wodini katika vituo vya kutolea huduma za afya katika mkoa mzima.

Onyo hilo lilitolewa jana mjini Songea na Mganga Mkuu wa Mkoa huo, Dk Damas Kayera kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Hassan Bendeyeko.

“Kuanzia sasa ni marufuku vitendo vya upigaji picha wodini kwa kutumia kamera au vifaa vyovyote vyenye uwezo wa kupiga picha kama simu za mkononi,” alisema Dk Kayera.

Alisema, wamebaini kuwa katika vituo mbalimbali vya kutolea huduma za afya katika mkoa huo, kumekuwa na tabia ya baadhi ya wananchi kupiga picha wodini pale wanapokuja kuwajulia hali ndugu zao waliolazwa.

Vitendo hivyo vinafanywa ama kwa lengo zuri la kuwajulisha jamaa zao hali ya mgonjwa wao au kwa malengo ambayo sio mazuri ambapo baadhi ya picha zimekuwa zikioneshwa kwenye mitandao ya kijamii zikiwa na ujumbe wa kupotosha.

Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto katika barua yake kwa makatibu tawala wa mikoa Tanzania Bara, inaeleza wizara imetoa tamko la kukataza kupiga picha wodini kwa kuwa inasimamia viwango na miiko ya utoaji huduma za afya.

Waganga wakuu wa mikoa na wakurugenzi wa halmashauri zote nchini wanatakiwa kusimamia utekelezaji wa agizo hilo na kwamba wananchi wanatakiwa kuelimishwa umuhimu wa kuwasilisha malalamiko yao pale inapotokea ukiukwaji katika utoaji wa huduma za afya.

Manispaa ya Songea nayo imeanza kutekeleza agizo la kupiga marufuku upigaji picha wodini kwenye vituo vyake vyote vya kutolea huduma za afya katika manispaa hiyo.

Ofisa Habari wa Manispaa hiyo, Albano Midelo alisema tayari Mkurugenzi Mtendaji wa manispaa hiyo ametoa maagizo kwa Mganga Mkuu wa Manispaa ya Songea kuhakikisha kuwa agizo hilo linatekelezwa kwa vitendo katika hospitali na vituo vya afya.

ZeroDegree.
Kupiga picha wagonjwa wodini marufuku. Kupiga picha wagonjwa wodini marufuku. Reviewed by Zero Degree on 10/17/2016 11:33:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.