Loading...

Mbabe wa Pluijm arejea kikosini

BEKI mwenye roho ya paka wa Yanga, Vicent Bossou, amerejea kundini jana akitokea nchini kwao Togo alipokwenda kuitumikia timu yake ya Taifa kwenye mchezo wa kirafiki wa kalenda ya FIFA dhidi ya Msumbiji.

Bossou amerejea kundini Yanga ikiwa ni baada ya siku chache kuiwezesha timu yake ya Taifa ya Togo kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Msumbuji.

Ikumbukwe kuwa beki huyo amekuwa ndiyo muhimili wa Yanga kwa siku za hivi karibuni ambapo ubabe wake uwanjani, lakini pia katika kuwaongoza wenzake, umekuwa na mchango mkubwa kwa timu yake msimu huu.

Kati ya sifa zinazomfanya Bossou kuwa tegemeo Yanga, ni uwezo wa kupambana kwa dakika zote bila kuchoka, kuwaongoza wenzake, hasa katika safu ya ulinzi, kuhamasisha na pia kumpa ukweli kocha wake kama ilivyojionyesha wakati wa mchezo dhidi ya watani wao wa jadi, Simba hivi karibuni.

Katika mchezo huo uliopigwa Oktoba Mosi mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Bossou alijidhihirisha kuwa na sifa za kuwa nahodha wa timu kubwa kama Yanga baada ya mara kadhaa ‘kumkoromea’ Kocha Mkuu wake, Hans van der Pluijm kufanya mabadiliko pale alipoona mambo yanakwenda kombo.

Japo Pluijm alionyesha kuwa na uhakika na kile alichokuwa akikifanya, lakini uthubutu wa Bossou ulionyesha jinsi mchezaji huyo alivyo na ujasiri wa aina yake kwani ni wachezaji wachache wenye uwezo wa kufanya hivyo.

Hata hivyo, beki huyo uhenda akaukosa mchezo wa kesho wa Ligi Kuu Tanzania Bara wakati Yanga itakapoivaa Azam FC mchezo kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam kutokana na kuyakosa mazoezi ya pamoja na wenzake kwa siku kadhaa.

Kukosekana kwa mbabe huyo kesho, huenda kukawa ni pigo kwa kikosi cha Yanga, japo nafasi yake inaweza kuzibwa vema na Kelvin Yondani ambaye ni wazi atasaidiana na Andrew Vincent katika nafasi ya beki wa kati.

Meneja wa Yanga, Hafidhi Saleh, alithibisha kikosi chao kumkosa Bossou na kusema kuwa mchezaji huyo anatajia kuingia nchini jana hivyo hataweza kujumuishwa na mwalimu kwenye kikosi hicho.

Alisema katika kujiandaa na mchezo huo, jana asubuhi walifanya mazoezi katika Uwanja wa Uhuru watakaotumia kwa ajili ya mchezo huo.

Bossou alisajiliwa na Yanga mwaka jana kwa mkataba wa miaka miwili na ameweza kuisadia timu hiyo katika mechi mbalimbali zikiwemo zile za kimataifa.

Kutokana na hilo katika mechi hiyo ya kesho, inayotazamiwa kuwa na upinzani mkali unasabishwa na hali ya timu zote mbili ambazo haziko vizuri katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi, Pluijm atalazimika kuandaa mchezaji mwingine anaweza kumudu nafasi hiyo kiufasaha.

Wachezaji wanaotarajia kuongoza jahazi katika mchezo huo, hawatakuwa tofauti sana na wale waliocheza mchezo uliopita ukimuondoa mshambuliaji wao Amiss Tambwe aliyepata majeraha huku Donald Ngoma na Obrey Chirwa aliyefunga bao lake la kwanza katika mechi iliyopita tangu ametua nchini.

Wengine wanaoweza kuanza kesho ni kama vile Haruna Niyonzima, Geofrey Mwashiuya aliyerejea baada ya kuwa nje kwa muda mrefu kutokana na kusumbuliwa na majeraha, Thaban Kamusoko, Mwinyi Haji, Simon Msuva, Juma Abdul, Vicent Andrew, Deogratius Munishi ‘Dida’, na Kevin Yondan.

Yanga inashika dimbani ikiwa imetoka kupata ushindi mnono wa mabao 3-1 dhidi ya Mtibwa, huku Azam wakiwa na hasira za kupoteza mchezo waliocheza na Stand United kwa kufungwa bao 1-0.

ZeroDegree.
Mbabe wa Pluijm arejea kikosini Mbabe wa Pluijm arejea kikosini Reviewed by Zero Degree on 10/15/2016 10:43:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.