Loading...

Pembejeo feki za kilimo zanaswa jijini Dar.

SERIKALI imekamata zaidi ya chupa 60 zenye ujazo wa mililita 100 za viuatilifu vya mimea visivyosajiliwa katika msako unaoendelea maeneo mbalimbali nchini.

Viatilifu hivyo vilikamatwa juzi katika soko la Kariakoo na maofisa wa taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu (TPRI) katika operesheni maalumu ya kukamata wafanyabiashara wanaouza bidhaa hizo ambazo hazijasajiliwa.

Mkaguzi Mwandamizi wa TPRI, Michael Sanga, aliwaambia waandishi wa habari baada ya kukamata viuatilifu hivyo aina ya Dudu-Acalamettin kuwa havijasajiliwa kuuzwa nchini kwa ajili ya matumizi ya kilimo.

Alisema dawa hizo ambazo zinatoka nje ya nchini, zilizosajiliwa zinafahamika kwa jina la Dudumetion na kwamba wakulima wameshindwa kufahamu zilizo halisi ni zipi.

Sanga alisema adhabu ya kukamatwa na dawa zisizosajiliwa ni faini ya kati ya Sh. milioni 10 hadi Sh. milioni 100, zile zisizokidhi vigezo vya lebo zake faini yake Sh. milioni mbili hadi Sh. milioni 10 au kifungo cha miaka tatu au vyote kwa pamoja.

Ofisa Mfawidhi wa TPRI Kanda ya Dar es Salaam, Solomon Mungula, alisema ukaguzi wa viatilifu hivyo ni endelevu katika maduka yote na kuwataka wananchi wanaonunua bidhaa hizo kudai risiti ili kumpata msambazaji wa bidhaa hiyo feki nchini.

Ramadhani Kambi, mmiliki wa duka la viuatilifu Kariakoo aliyekamatwa na dawa hizo, alikiri kununua kwa kampuni ya Bukoola Chemical Industries ambayo inasambaza nchini.

"Sikufahamu kama hizi dawa hazijathibitishwa kwa sababu nilinunua kwenye kampuni ambayo ni maarufu na iliyozoeleka na walinipatia risiti ambazo ninazo," alisema.

Msajili wa viatilifu hivyo kutoka Kampuni ya Biddi Enterprises, Godfrey Mchome, alisema sababu za kuamua kufanya ukaguzi huo ni kutokana na malalamiko kutoka kwa wakulima ambao walinunua viatilifu vinavyofanana na vile vilivyosajiliwa.

"Kikubwa hivi viatilifu tunaviwekea namba ya usajili ambayo ni 0709.

Hizi ambazo hazijasajiliwa hazina namba yetu na tofauti nyingine ni haya majina yametofautiana kidogo, ndiyo maana wakulima walipoona utofauti wa hizi dawa wakatoa malalamiko na leo (jana) tumeanza kuzikamata na tutafanya ukaguzi katika maduka yote ya dawa nchini," alisema.

ZeroDegree.
Pembejeo feki za kilimo zanaswa jijini Dar.  Pembejeo feki za kilimo zanaswa jijini Dar. Reviewed by Zero Degree on 10/29/2016 10:58:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.