Loading...

Shambulio la kigaidi lililotekelezwa na al-Shabaab Mandera, nchini Kenya lasababisha vifo vya watu 12.

Washambuliaji walirusha vilipuzi kwenye jumba hilo.
Watu 12 wameuawa baada ya watu wenye silaha kushambulia nyumba moja ya malazi mjini Mandera, kaskazini mashariki mwa Kenya.

Msemaji wa serikali ya Kenya Eric Kiraithe amesema watu sita wameokolewa kutoka kwenye hoteli hiyo ya Bishaaro.

Wanamgambo wanaoaminika kuwa wa kundi la al-Shabaab walishambulia nyumba hiyo mwendo wa saa tisa na nusu usiku. Walirusha vilipuzi kwenye nyumba hiyo kabla ya kuingia ndani na kuanza kuwafyatulia risasi waliokuwemo ndani.

"Sehemu ya jumba iliporomoka, na kuua watu 12. Watu sita wametolewa kutoka kwenye vifusi vya jengo hilo wakiwa hai kufikia sasa," ameandika Bw Kiraithe kupitia mtandao wa Twitter.

Wataalamu wa mabomu wanafanya uchunguzi kubaini ni vilipuzi vya aina gani vilitumiwa kutekeleza shambulio hilo.


Mji wa Mandera unapatikana katika mpaka wa Kenya, Somalia na Ethiopia.

Kundi la al-Shabaab limekiri kutekeleza shambulio hilo.

Mji wa Mandera umekuwa ukishambuliwa mara kwa mara na wanamgambo wa al-Shabaab, kundi linalopigana dhidi ya serikali inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa katika taifa jirani la Somalia.

Wanamgambo hao wamekuwa wakishambulia watu ambao si wa asili ya Kisomali.


Maafisa wa usalama nje ya hoteli ya Bishaaro.

Source: BBC Swahili
ZeroDegree.
Shambulio la kigaidi lililotekelezwa na al-Shabaab Mandera, nchini Kenya lasababisha vifo vya watu 12. Shambulio la kigaidi lililotekelezwa na al-Shabaab Mandera, nchini Kenya lasababisha vifo vya watu 12. Reviewed by Zero Degree on 10/25/2016 12:41:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.