Loading...

Shule zafundisha kuiba mitihani.

Hata baada ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kufikia kutangaza kuwa imefanikiwa kudhibiti wizi wa mitihani ya kuhitimu elimu ya msingi na sekondari imeelezwa kuwa kuna shule zinazofundisha mbinu za kuiba mitihani.

Wenye siri kuhusu vituo na shule hizo zinazokiuka taratibu za usiri wa mitihani ni Umoja wa Wamiliki wa Shule na Vyuo binafsi (Tamongsco) ambao wamesema baadhi ya shule hizo ni zile zinazofundisha masomo ya sekondari kwa miaka miwili kwa ajili ya kufanya mitihani ya maarifa (QT).

Habari hizo zimemshtua Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako alipoulizwa na Mwananchi kama ana taarifa hizo. Waziri huyo alisema wizara yake haina taarifa lakini ipo tayari kuzipokea na kuzifanyia kazi kwani imejizatiti kuongeza umakini zaidi katika ulinzi na usahihishaji wa mitihani hiyo hivyo ikipokea taarifa kutoka kwa raia wema itatoa ushirikiano.

“Kwa sasa tumekuwa watendaji zaidi katika kuweka ulinzi Necta wakati wa usahihishaji na wakati huo bado tunapokea ushirikiano kutoka kwa raia, kwa hivyo ikitokea kuna taarifa nyingine ya kuwapo kwa shule hizo, tunapokea na kuzishughulikia, hakuna shida kabisa tunaomba watoe hizo taarifa. Hatutaki kuona hali hiyo ikiendelea,” alisema Ndalichako.

Katibu Mkuu wa Tamongsco, Benjamin Nkonya alimwambia mwandishi wetu kuwa wanazifahamu shule 34 za binafsi zisizo na sifa kuanzia za awali hadi sekondari ambazo zinatoa elimu bila kuwa na vigezo vinavyotambuliwa kwenye usajili na miongoni mwa hizo zinafundisha mbinu za kuiba mitihani.

“Kuna shule za ovyo nyingi tu tunazifahamu. Tumewahi kuzibaini shule zinazofundisha hadi mbinu za kuiba mitihani ya mwisho, nyingi ni zile zinazofundisha masomo ya sekondari miaka miwili, wanaita QT,” alisema Nkonya.

Katibu mkuu huyo hakutaka kutaja majina ya shule hizo, bali alisema kwa sehemu kubwa, ziko katika jiji la Dar es Salaam. “Umoja wetu hautetei wala hauna masilahi na shule zinazokiuka maadili na miongozo ya Serikali,” alisema akiunga mkono hatua ya Serikali kuzifungia shule 43 na bweni moja kutokana na kukosa sifa.”

Nkonya ameiomba Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuongeza ushirikiano na umoja huo ili kudhibiti shule hizo zisiendelee kuathiri ubora wa elimu, usalama wa mwanafunzi wa kike huku wazazi wakiibiwa fedha zao kwa kutotambua au kupewa lugha za kurubuniwa.

“Huwezi kuanzisha operesheni ya kukamata samaki bila kutumia samaki (chambo). Sisi tunazifahamu na tunafahamiana wenyewe. Wazazi wanatakiwa kuilaumu wizara na siyo hao wamiliki wa shule kwa sababu wakati wa usajili wanahusika kusajili shule zisizokuwa na vigezo halafu wanapotaka kuzifungia hawataki kutushirikisha sisi wadau,” alisema Nkonya.

Alisema mwaka 2011, umoja huo ulifanikiwa kukusanya taarifa za majina ya shule 34 vimeo na kuziwasilisha kwa aliyekuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo lakini baada ya waziri huyo kuondoka wizarani hapo, shule hizo zilirudi na zinaendelea kufundisha.



Kuvuja mitihani

Maelezo haya yamekuja siku chache baada ya Wizara ya Elimu kuzifungia shule 43, nyingi zikiwa za wamiliki binafsi ambazo zilikosa vigezo vya usajili na mwandishi wetu alipotaka kujua mchango wa Tamongsco katika kuhakikisha wanachama wake wanazingatia taratibu zilizowekwa, alijibiwa kuwa ushirikiano ni mdogo.

Oktoba 27, 2014 Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) lilisema limedhibiti wizi wa mitihani na kwamba linakabiliwa na changamoto ya kudhibiti udanganyifu katika ngazi mbalimbali za elimu.

Mkuu wa Idara ya Fedha na Utawala, Necta, Daniel Mafie alisema Baraza lilifanikisha hilo kutokana na ushirikiano kati yake na kamati ya uendeshaji mitihani ya Taifa katika ngazi ya mkoa na wilaya. Idadi ya waliofutiwa matokeo kwa udanganyifu katika mitihani ya kumaliza elimu ya msingi mwaka 2013 ilikuwa wanafunzi 13 ikilinganishwa na watahiniwa 9,736 waliofutiwa mwaka 2011. Waliodanganya mtihani wa kumaliza kidato cha nne mwaka 2013 walikuwa 272 ikilinganishwa na 789 mwaka 2012 na watahiniwa 3,303 mwaka 2011.

Kutokana na udanganyifu huo, idadi ya wanaofaulu kuingia sekondari huku wakiwa hawajui kusoma na kuandika ni kubwa; mwaka 2012 walikuwa 5,000.

Kauli ya Serikali


Alipoulizwa ikiwa wanajua kuwa kuna shule zinazofundisha udanganyifu, Kaimu Mkurugenzi wa Usajili wa Shule katika wizara hiyo, Khadija Mcheka alisema hawajui lakini anakaribisha taarifa ya Tamongsco akisema uibuaji wa madudu ya shule zisizokuwa na sifa ni jukumu la Watanzania wote.

“Nimekuwa nikiwasiliana nao lakini tunaweza kuwaandikia barua rasmi. Tunahitaji ushirikiano na tumekuwa tukipata taarifa kutoka kwa wazazi, waandishi wa habari na wadau wengine watupatie taarifa ya shule hizo halafu tutazichukulia hatua haraka. Lazima tufahamu hilo ni tatizo linalowapata watoto wetu kwenye jamii,” alisema Mcheka.

Kuhusu hatua za usajili, Mcheka alikiri kuwapo kwa shule zinazotoa elimu bila kuwa na vigezo huku baadhi zikiwa zimepewa vibali kinyume cha mwongozo wa usajili na kusema baadhi ya wakaguzi walihusika. “Kuna baadhi ya wakaguzi, siyo wote, hawataki kuwajibika kwa nafasi zao. Unakuta mkaguzi wa wilaya kaandika halafu yule bosi wake kagonga mihuri tu na kusaini. Baadhi unakuta wanaleta taarifa zina mapungufu inabidi kurudisha tena sasa matokeo yake inatuchelewesha hata kutoa huduma kwa wadau,” alisema.

Hadi Septemba mwaka huu, shule za sekondari za umma 3,516 na binafsi 1,245 zilikuwa zimeshasajiliwa huku shule za msingi za umma zikiwa ni 16,087 na za binafsi 1,267. Mcheka alisema ofisi yake kwa sasa haitakubaliana na udhaifu wa shule yoyote inayojiendesha bila kuzingatia vigezo vilivyopo.

“Kwa mfano, kati ya wamiliki 49 walioleta maombi ya kibali cha ujenzi wa shule, 29 tu ndiyo walikubaliwa baada ya kujiridhisha na vigezo Agosti mwaka huu. Wakati mwingine kiongozi wa halmashauri anakuja na mapendekezo ya usajili wa shule tena anasifia kabisa shule fulani ina sifa lakini ukifuatilia hakuna kitu,” alisema.

Shule zilizofungiwa


Akizungumzia shule 43 zilizofungiwa kutokana na kukosa usajili, Mcheka alisema wamiliki watalazimika kuwasambaza wanafunzi kwenye shule nyingine kwa gharama zao.

Tayari zaidi ya shule 10 zilizofungiwa kutoa huduma ya elimu zimesambaza wanafunzi huku baadhi ya wamiliki wakilia ukata. Lakini shule ya Rose Land na Must Lead ya mkoa wa Pwani zimerekebisha makosa na zimerudishiwa vibali.

Source: Mwananchi
ZeroDegree.
Shule zafundisha kuiba mitihani. Shule zafundisha kuiba mitihani. Reviewed by Zero Degree on 10/08/2016 05:44:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.