Loading...

Simba na Yanga zarudishwa ‘Shamba la Bibi’.

BAADA ya Serikali kuzifungia timu za Simba na Yanga kutumia Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa muda usiojulikana kutokana na uharibifu wa miundombinu uliofanywa na mashabiki wa timu hizo katika mchezo wa Oktoba 1 mwaka huu, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limezitaka timu hizo kuutumia Uwanja wa Uhuru.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkurugenzi wa Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB), Boniface Wambura, alisema tayari wameshazijulisha timu hizo juu ya kuutumia uwanja huo ili kuziondolea mzigo wa kuendelea kutafuta sehemu ya kwenda kuchezea michezo yao.

“Tayari tumeshazitaarifu timu hizo kurudi kwenye Uwanja wa Uhuru licha ya kuwa una kasoro kidogo iliyopelekea ziukimbie na kuomba kuutumia ule wa Taifa, kimsingi timu hizi hazina viwanja na wakati Serikali ikiwa bado inaendelea na msimamo wake wa kuufungia zitakuwa zinautumia huu kwenye michezo yake inayoendelea,” alisema Wambura.


TFF ilizihamishia timu hizo Uwanja wa Taifa baada ya klabu ya Simba kuhofia usalama wa afya ya wachezaji wake kutokana na plastiki zinazoshika nyasi katika Uwanja wa Uhuru kuwaumiza katika michezo yake mitatu iliyochezea hapo.



Sababu nyingine ambayo Simba ililalamikia ni uwanja kuwa mdogo, ikitolea mfano mchezo wa Azam ambao ulipigwa dimbani hapo na baadhi ya mashabiki wake walishindwa kushuhudia.

Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara, alipotafutwa kuzungumzia suala la kurejea kwenye uwanja huo alisema kuwa viongozi watakutana kulijadili suala hilo kwa sababu ni wao walioomba kuondoka hapo na kuhamishiwa Uwanja wa Taifa.

Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Baraka Deusderit, alisema wao hawana matatizo na kurudi kwenye uwanja huo kwa sababu walioomba kuondoka hapo ni Simba na walikuwa na malengo ya kuomba kuutumia katika michezo yake hata kabla ya Bodi ya Ligi kuwaruhusu kuutumia.

ZeroDegree.
Simba na Yanga zarudishwa ‘Shamba la Bibi’. Simba na Yanga zarudishwa  ‘Shamba la Bibi’. Reviewed by Zero Degree on 10/11/2016 10:53:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.