Loading...

Hoja za Yanga

Suala la ukodishwaji wa klabu wa Yanga limeendelea kugonganisha vichwa vya wadau na wanachama wa klabu hiyo baadhi yao wakitoa mitazamo tofauti kuhusu mkataba huo.


Wiki iliyopita bodi ya wadhamini ya klabu hiyo iliridhia ikodishwe kwa Kampuni ya Yanga Yetu Limited kwa kipindi cha miaka kumi.



Kutokana na uamuzi huo, gazeti moja kubwa hapa nchini limeibua hoja nane za wadau ambazo wanachama na mwenyekiti wa klabu hiyo, Yusuf Manji wanatakiwa kujiuliza na kuzijibu kabla ya kuendelea na mchakato huo.

1-Mkutano wa wanachama na hasara Sh11 bilioni Yanga. 
Katiba ya Yanga inaweka wazi kuwa mkutano mkuu wa wanachama unatakwa uitishwe ndani ya siku 15, huku ajenda za mkutano huo zikitangazwa au kujulikana ndani ya siku saba.

Hata hivyo, mkutano mkuu uliopita wa wanachama, Agosti 6 ulidaiwa kukiuka katiba na uliitishwa ndani ya wiki, huku ajenda zikiibuka ndani ya mkutano.

Ajenda kubwa katika mkutano huo ilihusu mwenyekiti wa klabu hiyo (Manji) kutaka kuikodi Yanga kwa miaka 10.

“Nitaikodisha Yanga kwa miaka 10 kwa asilimia 75 na 25 inabaki kwa wanachama. Nataka kuikodisha timu na nembo, majengo ya klabu yanabaki kuwa mali ya wanachama,” alisema Manji.

Mwanachama Chris Kashililika alisema Imani Madega (aliyekuwa mwenyekiti) aliiacha Yanga ikiwa na Sh200 milioni kwenye akaunti yake, lakini miaka yote ya uongozi wa Manji, mfanyabiashara amekuwa akilalamika kapata hasara, kama kapata hasara kwanini anahitaji klabu hiyo kwa miaka kumi?

“ Kwanini mkataba ueleze Sh100 milioni kila mwaka, halafu asilimia 90 ziende kwenye matawi, kwanini iwe matawi na siyo klabu?

Mkataba una kipengele kisemacho ukivunjika mkodishwaji analipwa, ila hakuna sehemu inayoeleza analipa iwapo atauvunja,” alihoji Kashililika.

2-Mwenyekiti alisimama upande gani wakati wa kujadili mkataba?


Inajulikana kuwa Manji ni mwenyekiti wa Yanga, lakini wakati huo huo ndiye anayetaka kukodishwa klabu hiyo, swali la kujiuliza ni je, wakati majadiliano kuhusu ukodishwaji huo yakifanyika, mfanyabiashara huyo alikuwa upande upi, mwenyekiti au mkodishwaji?

Katibu mkuu wa zamani wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Fredrick Mwakalebela alibainisha kuwa ni muhimu katiba ya Yanga ikazingatiwa katika mchakato huo, huku akibainisha kuwa mkataba huo haujaanisha masilahi ya klabu hiyo.

“Hilo ni suala la kikatiba, bila katiba, process (mchakato) itakuwa na changamoto. Masilahi ya klabu ni muhimu kwa sababu Yanga ni klabu ya wanachama. Katika hili ni vyema Manji angesimamia upande mmoja. Anaingia kwa kofia ya uenyekiti au mfanyabiashara ili kuepuka mgongano wa kimasilahi,” alisema Mwakalebela.

Mchezaji wa zamani wa timu hiyo, Ally Mayay alisema mwenyekiti anaweza kusimama pande zote, lakini kubwa ni kulinda masilahi ya Yanga.

“Katiba yetu inaitambua bodi ya wadhamini kama chombo cha kusimamia mikataba. Kilicho muhimu ni kuhakikisha taratibu zote zinafuatwa ili mkodishaji na mkodishwaji wafahamu manufaa ya mchakato huo. “Ni vyema mkutano ujao utoe fursa pana kwa wanachama kujadili ili kupata undani wa masilahi ya pande zote. Jukumu kubwa la mwenyekiti ni kulinda masilahi hayo ya klabu,” alisema Mayay.

3- Ni mamlaka gani iliyo nayo bodi ya wadhamini?
Mamlaka ya bodi ya wadhamini ya Yanga yanaelezwa kuwa ni kusimamia mali za klabu na siyo kuuza. Hivyo, kama wanataka kuuza au kukodishwa ni lazima asilimia kubwa ya wanachama wa klabu hiyo waridhie jambo linalozua utata ndani ya klabu hiyo kwani baadhi ya wanachama wanaafiki na wengine wanapinga.

4- Nini nia ya Manji ya kuikodi klabu?


Kama nia ilikuwa njema kwa nini hakusema muda mrefu ili watu wapate kuijadili na kuelimishana kiundani hadi alipoibua jambo hilo kwenye mkutano wa dharura wa wanachama?

Aliyewahi kuwa mwenyekiti wa kamati ya matawi ya klabu ya Yanga, Mohamed Msumi alisema jambo hilo ni kubwa na linapaswa kufanywa kwa kina, akisisitiza kulitolea ufafanuzi sanjari na kuonyesha vielelezo kadhaa wakati ukifika.

Sekilojo Chambua ambaye ni mchezaji wa zamani wa Yanga alisema taswira ya ukodishwaji wa klabu hiyo unaleta picha ya maendeleo siku zijazo, ingawa hajui kama utafanikiwa u la.

“Mimi naona mchakato huu ni mzuri kwa maendeleo ya klabu na soka la Tanzania, ingawa siwezi kusema kama vyote vilivyotajwa ndani ya mkataba huo vitafanikiwa au la.”

5-Yanga itabaki vipi baada ya kumaliza mkataba wa kuikodisha?
Manji aliingia Yanga muda mrefu, kwanza akiwa mfadhili na baadaye mwenyekiti. Katika kipindi chote hicho ametamka kuwa amepata hasara anayodai inafikia Sh11.6 bilioni. Hata hivyo, mtu au kampuni inayoidai klabu hiyo haijatajwa, sasa swali je kama kwa muda huo amepata hasara huku klabu ikiwa na deni, akimaliza mkataba huo wa miaka 10 wa kuikodi ataiacha katika hali gani?

6 Nini nafasi ya wanachama Yanga?
Yanga ni klabu kongwe nchini, kama ilivyo kwa watani zake, Simba zinamilikiwa na wanachama na ndiyo maana mtu akitaka atolewe macho, awakere wanachama. Sasa, Yanga inataka kuingia katika mfumo mwingine wa klabu kumilikiwa na mtu mmoja, je, nafasi ya wanachama ni ipi?

Kuhusu nafasi ya wanachama wa Yanga, Mwakalebela alisema: “Lazima iwe wazi. Maana, mkodishaji anaweza kuamua kubadiliasha jezi ya timu kuwa nyekundu, jambo linaloweza kuzua utata, kwa hivyo masilahi ya wanachama yafahamike wazi katika mkataba.”

Akizungumzia kuhusu nafasi ya wanachama endapo klabu hiyo itakodishwa kwa mmiliki mmoja, Chambua alisema bodi ya wadhamini inatakiwa kukaa na mmiliki ili kuliangalia hilo kwa ufasaha.

“Sijui bodi ya wadhamini ya Yanga ilikubaliana vipi na kampuni hiyo inayotaka kuikodi klabu, lakini nafikiri ili kuangalia nafasi ya wanachama iko wapi wanatakiwa wakae na kujadili kwa kina kwa masilahi ya pande zote mbili, mkodishwaji na wanachama, ”alisema.

7-Itakuwaje Yanga ikikodishwa na kupata mwenyekiti mpya, majukumu yake yatakuwaje?
Hivi sasa mwenyekiti ni Manji na akikodishwa atakuwa mmiliki wa Yanga, je, kama watapata mwenyekiti mpya kazi yake itakuwa nini na kamati yake ya utendaji?

8- Kwa nini Manji anataka nembo na timu pekee?
Hilo ni swali linalogonga vichwa vya wadau wengi wa soka ambao wanajiuliza, kwa nini Manji atake timu na nembo pekee huku majengo ya klabu akiyaacha kwa wanachama.

Mchezaji mwingine wa zamani wa Yanga, ambaye pia ni mwanachama wa klabu hiyo, Ramadhan Kampira alisema hakuna kitu chochote watakachonufaika nacho wanachama kupitia ukodishwaji wa klabu hiyo na kuhoji ikiwa Manji anadai kupata hasara kwanini ang’ang’anie kumiliki nembo ya klabu.

“Manji anataka kutuhadaa, huo mkutano hauna lolote unaloweza kufanya zaidi ya kuhalalisha masilahi yake. Ni kama timu haina uongozi na yeye ndiye kila kitu.

“Mikutano ya wanachama lazima ipitie kwenye kamati ya utendaji na ni kwa mujibu wa katiba, mikutano ya dharura haina mamlaka ya kutoa uamuzi mkubwa. Manji akifanikiwa kukodishwa kwa miaka kumi Yanga haitaachwa salama,” alisema Kampira.


Credits: Mwananchi
ZeroDegree.
Hoja za Yanga Hoja za Yanga Reviewed by Zero Degree on 10/11/2016 10:30:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.