Loading...

Siri ya kijana mtoboa macho Jijini Dar.

Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akiwa na kijana Said Ally aliyejeruhiwa kwa kutolewa macho na Scorpion.
MTUHUMIWA wa tukio la kumchoma kisu na kumtoa macho, Said Ally, maarufu kama ‘Scorpion’, anadaiwa kuwa ni mbabe ambaye anaogofya kila mtu mtaani kwake eneo la Buguruni kwa Mnyamani Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam.


Jina la Scorpion lilianza kusikika katika vyombo vya habari mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya Kituo cha redio cha Clouds FM kutoa siri za kijana huyo aliyemjeruhi Ally ambaye ni kinyozi kwa kumtoboa macho na kumsababishia upofu.

Mmoja wa wauza kuku (jina limehifadhiwa) ambako Ally alijeruhiwa, aliwaambia waandishi wa habari kuwa Scorpion amekuwa akiogopwa na kila mtu katika mtaa huo na hata wakati anampiga na kumjeruhi Ally, hakuna mtu aliyejitokeza kumsaidia.

Alisema kila siku ‘mbabe’ huyo wa mtaa alikuwa akifika kwenye eneo hilo saa 12 jioni na kutangaza kwamba yeye ndiye mlinzi wa eneo hilo na hakuna ruksa kwa mtu mwingine kukatiza maeneo hayo.

Katika simulizi hiyo, ilielezwa Scorpion alikuwa na utaalamu wa karate ambao aliutumia kupora watu fedha na vitu mbalimbali.

Ilielezwa kuwa baada ya hapo huwapiga na kuwajeruhi kabla ya kuwarusha barabarani wagongwe na magari au pikipiki ili kupoteza ushahidi.

“Mtaa mzima unamuogopa Scorpion ambaye alipenda kujiita ‘teacher’ kutokana na vitendo vyake vya kupiga na kupora watu bila kificho na wakati mwingine kuwasukumia barabarani wagongwe na magari kwa lengo la kupoteza ushahidi.

“Yule alikuwa mtawala wa eneo hili, hata vibaka walikuwa wanamwogopa hawakuthubutu kukaribia katika eneo lake.

“Ni ukweli kwamba hata polisi wa Kituo cha Polisi Buguruni walimlea kwa sababu taarifa zake walikuwanazo muda mrefu lakini hawakuchukua hatua hatua zozote.

“Na hata katika tukio la juzi, polisi walipofika walishindwa kumkamata huku wakiwataka wananchi ndiyo wamkamate na kumpeleka kituoni,” alisema kijana huyo kwa sharti la kutotajwa jina.

Mkazi mwingine wa mtaa huo, alisema huenda Scorpion ni miongoni mwa vijana waliopitia mafunzo ya jeshi na baadaye kuachwa mtaani hivyo alikuwa akitumia ujuzi huo kufanya uhalifu.

“Scorpion alikuwa anasema kuwa anazuia wezi na kwamba ana kibali cha kufanya kazi hiyo na askari walikuwa wakimwona na kumwacha.

“Hata lile tukio alilolifanya la kumtoboa macho yule kinyozi hakuna mtu ambaye angejitoa mhanga kwenda kumkamata kwa jinsi alivyojiweka mtaani hapa,” alisema mkazi huyo.

Mkazi huyo alisema Ally aliposhuka kwenye bajaji na kusogea apate kununua kuku kwenye kibanda cha chips, Scorpion aliyekuwa amekaa karibu na meza za kuku alinyanyuka na kwenda nyuma yake.

“Sijui alimuuliza jambo gani na Ally hakumjibu ndipo alipoanza kumchoma visu mgongoni, kisha kumtoboa macho na kumwacha pale.

“Polisi walipokuja kumchukua majeruhi Scorpion alikuwa ameketi pembeni lakini askari hawakumgusa hadi walipokuja wenzao kutoka Kituo cha Stakishari ndiyo waliweza kumkamata,” alisema.

Meneja wa baa ya Kimboka iliyosemekana kuwa Scorpion alikuwa akifanya shughuli za ulinzi, Athumani Mwambe, alisema alikuwa akimwona nyakati za usiku lakini hakuwa analinda kwenye baa yake.

“Mtu huyu hakuwahi kuwa mlinzi wa baa hii labda alikuwa akionekana mtaani na kujifanya anazuia wezi waliokuwa wakifanya matukio.

“Alishajifanya ndiye mbabe wa mtaa huu kwa hiyo watu wengi walimuogopa.

“Vibaka wote wa mtaa huu walikwishamkimbia hivyo hata angefanya jambo gani hakukuwa na mtu wa kumgusa,” alisema.

Mkazi mwingine wa eneo hilo Salome Mgaya alisema: “Tumekuwa watu wa kuishi kwa hofu kwa kipindi kirefu na inafikia mahali hata pale unapokuwa umechelewa kurejea nyumbani kutoka kwenye mihangaiko ya maisha unakuwa huna amani kwa kuhofia usalama wako.

“Kwani mtu huyu alikuwa akikukuta njiani basi utakachokuwa nacho ni halali yake… lakini shida huja pale unapokuwa huna kitu, utapigwa na kuumizwa vibaya”.

Source: Mtanzania
ZeroDegree.
Siri ya kijana mtoboa macho Jijini Dar. Siri ya kijana mtoboa macho Jijini Dar. Reviewed by Zero Degree on 10/04/2016 08:45:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.