Loading...

Vita ya maneno kuisha leo Taifa, ..vigogo watakaposimamisha Nchi kwa muda wa dakika 90.

kocha wa simba Joseph Omog akiwa na wachezaji wake katika mazoezi ya mwisho kabla ya kukabiliana na yanga.
VITA ya maneno, mbwembwe, majigambo na visasi kati ya mashabiki wa Yanga na Simba, inafikia tamati leo kwenye Uwanja wa Taifa pale vigogo hao wa soka la Tanzania watakapoisimamisha nchi kwa dakika tisini katika ‘dabi’ ya kwanza msimu huu.

Kwa zaidi ya wiki mbili, karibu kila kona ya nchi hasa Dar es Salaam, mashabiki wa soka wa klabu hizo kongwe wamekuwa wakirushiana vijembe – kila mmoja akitamba kuibuka na ushindi. 

Miamba hiyo ya soka, Yanga mabingwa watetezi na Simba wakisaka taji la kwanza baada ya miaka minne, wanakutaka leo katika mchezo wa 82 Ligi Kuu Bara.

Msimu uliopita, Yanga ilikamilisha vizuri msemo wao ‘ubingwa haunogi bila kuifunga Simba’ baada ya kuwafunga mahasimu wao hao mechi zote mbili na kuzoa pointi sita.

Yanga ina rekodi za ushindi zinazosomeka vizuri dhidi ya Simba, huku pia timu hiyo ya Jangwani ikiongoza kutwaa taji la Ligi Kuu Bara.

Hata hivyo, takwimu za karibu kuanzia mwaka 2000, zinaonyesha kuwa katika mechi 33 walizokutana vigogo hao, Simba imeshinda 11, sare mara 15, huku Yanga ikishinda mechi saba tu.

Kuelekea mchezo huo, Simba walikwenda kupiga kambi Mji Kasoro Bahari, huku wapinzani wao wakivuka bahari hadi Pemba.

Kwa mujibu wa makocha wa kila upande – Yanga, Hans van der Pluijm na Simba, Joseph Omog wamedai kuwa kazi ya maandalizi kwa ajili ya mchezo huo imekamilika vizuri.

Kocha Omog atashusha uwanjani kikosi cha Simba kilicho na deni la ‘kuwainamisha’ vichwa chini mashabiki wake msimu uliopita baada ya kunyukwa na vijana hao wa Jangwani.

Katika kuhakikisha Simba wanaibuka na ushindi, aliyewahi kuwa mfadhili wa timu hiyo, Azam Dewji alitoa ahadi ya kununua kila bao litakalofungwa kwa Sh. milioni 1.

Kwa upande wa Yanga, Pluijm alisema juzi kuwa kikosi chake kitaingia uwanjani kwa tahadhari kubwa kuwakabili Simba waliopania kulipa kisasi.

Pluijm anajivunia safu yake ya ulinzi ambayo katika mechi tano imeruhusu kufungwa bao moja tu, huku wapinzani wao wakiwa na safu ya ushambuliaji iliyo kwenye kiwango kizuri msimu huu.

"Mchezo huu umewaweka mashabiki wengi kwenye presha. Wachezaji wangu wanafahamu umuhimu wa kushinda mchezo huu, naamini watafanya hivyo," alisema Pluijm.

Kocha Msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja alisema wamejiandaa vizuri kwa ajili ya mchezo huo.

“Hatutawapa nafasi wachezaji wa Yanga kucheza mpira, watakapokuwapo na wachezaji wetu watakuwa hapohapo,” alisema Mayanja.

Mechi ya mwisho kabla ya kuivaa Yanga, Wekundu wa Msimbazi wenye pointi 16 na walio katika nafasi ya kwanza, waliichapa Majimaji mabao 4-0, huku Yanga yenye pointi 10 nafasi ya tatu wakipoteza mechi yao ya kwanza msimu huu kwa kufungwa na Stand United.

Licha ya kutokuwa na makali msimu huu, Yanga ambao ni wenyeji wa mchezo wa leo wataongozwa na washambuliaji wake Donald Ngoma, Amissi Tambwe na Simon Msuva huku Msimbazi ikiwategemea Laudit Mavugo, Ibrahim Ajib na kinara wa kupachika mabao, Shiza Kichuya.

Hata hivyo, mashabiki wa soka wamekuwa na changamoto ya kutofahamu elimu ya kununua tiketi kwa mfumo mpya wa kielektroniki ambayo inaanza rasmi leo kwenye Uwanja wa Taifa.

Refa Martin Saanya wa Morogoro ndiye atapuliza filimbi katika mchezo huo akisaidiwa na Ferdinand Chacha wa Mwanza na Samuel Mpenzu kutoka Arusha.

ZeroDegree.
Vita ya maneno kuisha leo Taifa, ..vigogo watakaposimamisha Nchi kwa muda wa dakika 90. Vita ya maneno kuisha leo Taifa, ..vigogo watakaposimamisha Nchi kwa muda wa dakika 90. Reviewed by Zero Degree on 10/01/2016 09:54:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.