Loading...

Walemavu nchini kutibiwa bure.

WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imesema inatambua na itaendelea kuhakikisha watu wenye ulemavu wasio na uwezo wa kugharimia huduma za matibabu wanapatiwa msamaha wa matibabu katika ngazi zote kuanzia zahanati, vituo vya afya, hospitali za mikoa na za rufaa.

Aidha imesema kwa kutambua umuhimu wa huduma ya afya kwa wananchi wote, serikali kupitia wizara hiyo ipo katika mchakato wa kutungwa kwa sheria itakayowezesha wananchi wote wakiwemo watu wenye ulemavu kupata kitambulisho cha bima ya afya.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu aliyasema hayo katika tamko lake kuhusu huduma za matibabu kwa walemavu wasio na uwezo na kusema hatua hiyo itawaondolea vikwazo, wananchi wote wakiwemo watu wenye ulemavu katika kuzifikia huduma za afya pasipo kikwazo cha ukosefu wa fedha.

“Wizara inapenda kutoa ufafanuzi kuhusu tamko la Shirikisho la Watu Wenye Ulemavu nchini (Shivyawata) kuhusu makundi ya wananchi wanaostahili kupata msamaha wa matibabu. Aidha, baadhi ya vyombo vya habari vimenukuu maelezo ambayo yametolewa na mwenyekiti wa Shivyawata kuhusu makundi yanayostahili kupata msamaha wa matibabu nchini,” alisema.

Alisema kutokana na maelezo hayo, Sera ya Afya ya Mwaka 2007 inatambua kuwa wapo wananchi wanakabiliwa na matatizo mbalimbali katika kuzifikia huduma za afya wakiwemo watu wenye ulemavu.

Ummy alisema kuwa Sheria ya Watu Wenye Ulemavu Namba 9 ya mwaka 2010, pamoja na mambo mengine, inabainisha kuwa watu wenye ulemavu wana haki ya kuondolewa vikwazo katika kupata huduma za afya.

Pia alisema serikali itaendelea kusimamia na kuhakikisha makundi maalumu wakiwemo watu wenye ulemavu ambao hawana uwezo wa kuchangia huduma za matibabu wanapata msamaha wa matibabu katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya.

“Natoa maelekezo kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuwatambua watu wenye ulemavu wasio na uwezo wa kuchangia huduma za matibabu na kuimarisha Kitengo cha Huduma za Ustawi wa Jamii katika vituo vya kutolea huduma za afya ili viweze kuwatambua na kutoa msamaha kwa watu hao ili waweze kupatiwa matibabu bila ya vikwazo vya ukosefu wa fedha. Ni marufuku kwa mtumishi yeyote wa sekta ya afya kuonesha vitendo vyovyote vya unyanyapaa na unyanyasaji kwa watu wenye ulemavu wanaofika katika vituo vya kutolea huduma za afya.

Alisema mtumishi atakayethibitika kuonesha kwenda kinyume cha maadili ya utumishi wa umma na taaluma za afya kwa kufanya vitendo vya unyanyapaa na unyanyasaji kwa makundi maalumu ikiwemo watu wenye ulemavu atachukuliwa hatua za kinidhamu ikiwemo kufukuzwa kazi.

“Wizara yangu inafanya jitihada kuhakikisha kuwa inaondoa vikwazo vyote vinavyowanyima watu wenye ulemavu kupata huduma za afya wanazohitaji ikiwemo kuhakikisha kuna mazingira mazuri yanayowawezesha kufika hospitali kwa kuweka miundombinu rafiki,” alisema.


ZeroDegree.
Walemavu nchini kutibiwa bure. Walemavu nchini kutibiwa bure. Reviewed by Zero Degree on 10/17/2016 05:33:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.