Loading...

AJALI: Nyota wa soka nchini Brazil afariki Dunia baada ya kumpigia simu mkewe.

Ulimwengu wa soka una maajabu yake. Kipa wa Chapecoense, Danilo aliyenusurika katika ajali alimpigia mkewe simu ya mwisho kabla ya mauti kumkuta akiwa hospitalini Medellin, Colombia.

Danilo ni mmoja kati ya watu sita walionusurika kifo wakati ndege waliyopanda ilipoanguka na kuua watu 75 ambao walikuwa miongoni mwa abiria 81.

Hata hivyo, Danilo (31) akiwa hospitali alimpigia simu mkewe na kuzungumza naye kwa mara ya mwisho kabla ya kifo chake.

Klabu hiyo ndogo iliyolinganishwa na Leicester City ya England iliduwaza Amerika Kusini kwa kufuzu fainali, ambayo hata hivyo ilikatishwa ghafla juzi kwa ajali ya ndege.

Waliokufa ni wanasoka wa klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Brazil, Chapecoense kwenye ajali iliyotokea anga la Colombia.

Danilo akiwa na mkewe enzi za uhai wake. Picha hizi alizirusha katika mtandao wake wa Instagram.
Ajali hiyo ilihusisha ndege ya kukodi ya Shirika la Liama la Bolivia iliyobeba wachezaji hao na maofisa wengine waliokuwa wakielekea Medellin kucheza dhidi ya Atletico Nacional ya mjini humo kwenye mchezo wa kwanza wa mashindano ya Copa Sudamericana, ambayo yanaweza kulinganishwa na yale ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF) au yale ya Ligi ya Europa barani Ulaya.

Huo , ulikuwa mchezo wa kihistoria kwa klabu hiyo inayoshika nafasi ya 21 kwa utajiri nchini Brazil kulingana na takwimu za mamlaka zinazosimamia michezo na biashara nchini humo.

Ndege hiyo iliyotengenezwa na Kampuni ya BAe, ambayo inafahamika kwa Tanzania hasa kutokana na kashfa ya rada wakati wa utawala wa awamu ya tatu chini ya Rais mstaafu Benjamin Mkapa, ilianguka na kukatika vipande viwili, sehemu ya mkia ikiwa imeharibika vibaya zaidi. Waokoaji walieleza jana kuwa mabaki ya miili yalionekana kutapakaa kwenye eneo la tukio.

Mpigapicha wa Shirika la Habari la Uingereza la Reuters aliyefika eneo la tukio, alieleza baadaye kuwa waokoaji 30 walionekana wakiendelea na kazi hiyo ngumu milimani, mahali ambako polisi na wanajeshi pia walishiriki katika uokoaji wa maisha ya abiria 81 wa ndege hiyo.

Chapecoense, klabu kutoka Ligi Kuu ya Brazil iliyokuwa ikienda Colombia kuikabili Atletico Nacional ya Medellin katika mchezo wa leo, ambao Shirikisho la Soka la Amerika Kusini (Conmebol) ulisitisha shughuli zote za michezo ilifuzu baada ya kuiondoa San Lorenzo ya Argentina inayoshabikiwa na Papa Francis kwa bao 1-1 la ugenini, ambako katika mchezo wa marudiano zilitoka suluhu.

Klabu hiyo ndogo ya Chapeco ilifuzu kimiujiza mashindano hayo makubwa ya Soka Amerika Kusini, ambako kwa England, vyombo vya habari viliifananisha na ile ya Leicester City iliyochomoza na kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu, EPL kiaina msimu uliopita, lakini inaendelea kufanya vibaya kadri ligi inavyosonga mbele.

Wachezaji wasalimika

Polisi na vyombo vya usalama viliwataja wachezaji hao kuwa ni beki Alan Luciano Ruschel, wenzake Marcos Danilo Padilha na Jakson Ragnar Follmann kama walionusurika, wakinukuu mamlaka ya majanga ya Colombia.

Salamu za rambirambi na pole zilitumwa kutoka sehemu mbalimbali duniani, ingawa klabu hiyo ilieleza kuwa haikuwa tayari kutoa taarifa yoyote hadi ipate habari kamili kutoka mamlaka za Colombia.

“Watu sita wamenusurika ni wazima, lakini kwa bahati mbaya, mmoja amekufa wakati akihudumiwa. Wengine wote wameteketea. Idadi ya vifo ni 76,” alieleza Jose Gerardo Acevedo, mkuu wa polisi wa eneo hilo akiwaeleza wanahabari.

Wanahabari pia wamo

Habari zinaeleza kuwa ndege hiyo ilibeba wanahabari 21 kutoka vyombo mbalimbali vya Brazil waliokuwa wakienda kuripoti mechi hiyo.

Polisi wa Colombia walieleza kuwa ndege hiyo ilianguka kwenye eneo la vilima, jambo ambalo lilikwamisha harakati za uokoaji.

Mtandao wa kufuatilia mienendo ya ndege wa Flightradar24 uliandika kwenye mtandao wa Twitter kwamba uchunguzi kwenye ndege hiyo iliyosafiri kwa namba 2933 ilikuwa futi 15,500 kutoka usawa wa habari, umbali wa kilomita 30 kutoka Medellin ilipotoweka kwenye rada, mahali ambako ni milima inayofikia futi 7,000.

Kampuni ya BAe 146 ambayo ni tanzu ya BAE Systems ya Uingereza ilieleza kuwa ndege yake ilikuwa na abiria 72 na watumishi tisa ilipoanguka Jumatatu asubuhi.

Salamu za rambirambi

Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) lilieleza katika salamu kuwa tukio hilo la klabu ya Chapecoense na vyombo vya habari Brazil ni la kusikitisha.

Raia wa Brazil, Michel Temer alieleza masikitiko yake, akitaka watu waungane wakati huu wa majonzi na harakati za uokoaji ziendelee ili kupata miili ya wote waliokuwa wakisafiri kwenye ndege hiyo.

Kipa wa zamani wa Hispania, Iker Casillas anayeichezea Porto ya Ureno aliandika kwenye mtandao wake kuumizwa na tukio hilo.

Klabu za Flamengo, Botafogo, pia zilituma salamu za rambrambi na kuwatakia afya njema wale waliosalimika.

Nyingine zilizotuma salamu ni Arsenal, Manchester United, Torino, huku Barcelona na Real Madrid na kusimama kwa dakika moja wakati wa mazoezi yao ya jana.

ZeroDegree.
AJALI: Nyota wa soka nchini Brazil afariki Dunia baada ya kumpigia simu mkewe. AJALI: Nyota wa soka nchini Brazil afariki Dunia baada ya kumpigia simu mkewe. Reviewed by Zero Degree on 11/30/2016 01:54:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.