Loading...

Dereva wa basi mbaroni kwa ulevi.

OPERESHENI ya upimaji vilevi kwa madereva wa magari ya abiria yaendayo mikoani, imemnasa dereva wa basi la kampuni ya JM Luxury, Romanus Mponzi, akiendesha gari akiwa amelewa.


Dereva huyo wa basi lililokuwa likitoka Bukoba kwenda Dar es Salaam, alibainika kutumia kilevi katika operesheni iliyofanywa juzi kwa ushirikiano kati ya Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Morogoro na mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na nchi kavu (Sumatra).


Awali, dereva huyo alijaribu kuwakimbia askari kwa kutumia miguu, pale alipotakiwa kushuka ili kunusuru maisha ya abiria, kabla ya kukimbizwa na askari na kukamatwa.

Mkuu wa Usalama Barabarani Wilaya ya Morogoro, Victor Ayo, alisema askari huyo atachukuwa hatua za kisheria ikiwapo kutozwa faini na kuwataka madereva nchini kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za usalama barabarani.

Mponzi alipohojiwa na Nipashe, alikiri kunywa pombe kiasi kidogo kwa madai kuwa wanaruhusiwa kufanya hivyo kwa mujibu wa mafunzo aliyoyapata.

Ayo alisema operesheni ya kuwasaka madereva wanaotumia vilevi ni endelevu na inalenga kukomesha vitendo vya uvunjaji wa sheria barabarani ambavyo vimekuwa vikisababisha ajali na hata kugharimu maisha ya wananchi.

Naye Ofisa Mfawidhi wa Sumatra Mkoa wa Morogoro, Joseph Mlongo, alisema wataendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama barabarani kuhakikisha usalama wa abiria na mali zao unakuwapo, ikiwamo kudhibiti viashiria vya ajali.

Baadhi ya madereva waliozungumza na Nipashe, Pamela John, Alex Masege na Fuya Lema, waliiomba serikali kupitia Jeshi la Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani kuendelea na utaratibu huo kwa kuwa matukio ya ajali yamekithiri kiasi cha nchi kuwa na idadi kubwa ya vifo vitokanavyo na ajali za barabarani.

‘Kwanza ukinywa unachoka na kusinzia, si kweli kwamba pombe inaondoa uchovu na kwa dereva si salama," alisema Lema, dereva wa basi la Lim Safari linalofanya safari zake kati ya Morogoro na Arusha.

ZeroDegree.
Dereva wa basi mbaroni kwa ulevi. Dereva wa basi mbaroni kwa ulevi. Reviewed by Zero Degree on 11/27/2016 12:10:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.