Loading...

Hiki ndicho kinachoua vyama vya wafanyakazi.

MATUMIZI mabaya ya fedha, pamoja na usimamizi mbovu wa rasilimali za taasisi na vyama vya kutetea maslahi ya wafanyakazi nchini, vimetajwa kuwa ndiyo vikwazo katika maendeleo na uimara wa vyama hivyo.

Hayo yalisemwa jijini Mbeya na mwakilishi wa mwenyekiti wa kitengo cha wanawake kutoka Chama cha Walimu Tanzania (CWT) taifa, Tukapaga Mwasandele, wakati akifunga mafunzo ya watunza hazina wanawake wa chama hicho ngazi ya wilaya na mikoa kwa Kanda ya Nyanda za Juu Jusini. 

Mwasandele ambaye ni mwalimu kutoka wilayani Chunya, alisema vyama vingi vya wafanyakazi nchini vinashindwa kuendelea kutokana na matumizi mabaya ya fedha na mali za vyama hivyo na kuwataka watunza hazina wa CWT kubadilika katika suala hilo.

Alisema vyama hivyo vinatakiwa kuboresha utendaji kazi kwa kuwapatia elimu ya usimamizi wa fedha na mali wahasibu wake ili viweze kuendelea na kufanya kazi kwa ufanisi zaidi kuliko ilivyo sasa.

Alisema endapo kutakuwa na usimamizi mzuri, vyama hivyo vitakuwa imara na hata migogoro ya wafanyakazi itakwisha.

“Mlionufaika na mafunzo haya nina uhakika mtakwenda kuyafanyia kazi vizuri na kuleta mabadiliko kwa wanachama, tunatarajia kuona mnakuwa mstari wa mbele kusimamia vyema mali za vyama vyenu kwa ajili ya ustawi wake.”

“Mkitumia mbinu hizi mlizofundishwa hapa ni wazi kuwa migogoro inayotesa vyama vingi vya wafanyakazi haitaonekana tena hasa kwenye suala la fedha ndiko kunakoleta matatizo kwenye vyama vingi hivyo mkasimamie vyema,” alisisitiza Mwasandele.

Mratibu wa CWT Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Fratern Mwahison, alisema mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa chama hicho kwa mwaka 2016 yakiwa na lengo la kuongeza ufanisi kwa wahasibu wanawake kupitia kitengo hicho.

Alisema mafunzo hayo yaliyohusisha mikoa saba ya Mbeya, Rukwa, Iringa, Katavi, Songwe, Njombe na Ruvuma, yataongeza uelewa wa usimamizi wa rasilimali fedha zinazotokana na ada za wanachama wa CWT pamoja na miradi mingine ya chama.

Kwa upande wake, mkuu wa Idara ya jinsia na walimu wanawake wa CWT kutoka makao makuu, Mwandile Kigutu, alisema walionufaika na mafunzo hayo ni walimu wanawake na kwamba wana nia ya kuimarisha kitengo hicho.

Alisema walimu hao wamepewa mafunzo ya sera ya jinsia na walimu wanawake ili kuhakikisha inatekelezwa kikamilifu.

Source: Nipashe
ZeroDegree.
Hiki ndicho kinachoua vyama vya wafanyakazi.   Hiki ndicho kinachoua vyama vya wafanyakazi. Reviewed by Zero Degree on 11/04/2016 08:56:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.