Loading...

Kocha Joseph Omog arejea na kipa Simba.

KOCHA Mkuu wa Simba, Joseph Omog, anatarajiwa kutua nchini leo Jumapili akitokea kwao Ivory Coast, ambapo moja ya kazi aliyopewa na viongozi ni kutafuta kipa mwenye uwezo mkubwa kama alivyopendekeza kwenye ripoti yake.


Katika ripoti yake aliyoiwasilishwa kwa uongozi, alipendekeza wasajiliwe wachezaji watatu, ikiwamo nafasi ya kipa ambapo taarifa kutoka kwa wekundu hao wa Msimbazi zinadai kuwa, viongozi walimwambia akiona mlindamlango atakayemvutia huko kwao Ivory Coast asisite kuja naye.

Wakati viongozi wakimpa kazi hiyo, wanajua kuwa anaweza afanikiwe au asifanikiwe, ambapo wenyewe waliendelea kufanya mazungumzo ya chini kwa chini na kipa wa African Lyon raia wa Cameroon, Rostand Youthe, ili kama Omog hatafanikiwa wamsajili.

Taarifa kutoka Simba zinadai kuwa, mazungumzo kati ya Simba na kipa huyo wa African Lyon yamekuwa yakiendelea vizuri na kama Omog hatafanikiwa kupata mlindamlango hodari huko kwao, basi haitakuwa tabu, kwani huyu wanayemfukuzia anaweza kugombania vizuri namba na Vincent Angban.

“Katika ripoti yake alisema anataka pia kuongezewa kipa ambapo uongozi umemwambia kama akipata huko kwao aje naye, lakini ikishindikana wapo wengi hapa nchini walioonyesha uwezo mkubwa mzunguko wa kwanza tunaweza kuwachukua.

“Uongozi hautaki kabisa kumuingilia kocha kwenye majukumu yake, ndiyo maana wakampa uhuru kama akipata kipa aje naye, lakini pia kuna mazungumzo na kipa wa African Lyon ambayo yanakwenda vizuri,” alisema kigogo mmoja.

Katika hatua nyingine, wakati Yanga chini ya kocha wao mpya, George Lwandamina wakitarajiwa kuanza tizi kesho, taarifa kutoka Simba zinadai kuwa nao wanaweza kuanza siku hiyo kujiweka sawa kwa ajili ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.

Wekundu hao wa Msimbazi wanajua kuwa mzunguko wa pili utakuwa kama vita, kutokana na wapinzani wao hao kutaka kuwang’oa kileleni na sasa wamesema jeshi lao linaanza mazoezi ya kijeshijeshi kesho.

Taarifa kutoka Simba zinadai kuwa, tayari kuna baadhi ya wachezaji wamesharejea na leo Kocha Mkuu wa kikosi hicho, Joseph Omog, anatarajiwa kutua Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Nyerere kuanza kibarua chake cha mzunguko wa pili.

Akizungumza na waandishi wa habari akiwa nchini kwao Cameroon, Omog alisema lengo la kuingia kambini mapema ni kutaka kuhakikisha kuwa wanafanya maandalizi mazuri na kuendelea kukaa kileleni hadi ligi inamalizika na hatimaye kutwaa ubingwa.

“Ligi ni ngumu na ina changamoto kubwa, hivyo tunahitaji kuanza mazoezi mapema ili kuwaweka sawa wachezaji wangu na kuhitaji ushindi kwa kila mechi,” alisema Omog.

ZeroDegree.
Kocha Joseph Omog arejea na kipa Simba. Kocha Joseph Omog arejea na kipa Simba. Reviewed by Zero Degree on 11/27/2016 11:42:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.