Loading...

Kocha Mzambia, George Lwandamina kuwasili leo Jangwani.

WAKATI Kocha Mkuu wa Yanga, Hans Van der Pluijm, akipambana kikosi chake kupata matokeo mazuri leo dhidi ya Prisons Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, kwa upande mwingine Wanajangwani hao wana ugeni mzito unaotarajiwa kuwasili leo.

Taarifa za kuaminika kutoka Yanga zinadai kuwa kocha Mzambia, George Lwandamina, anaweza akawasili leo jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya kupokea kijiti cha Pluijm ambaye anaandaliwa kupewa cheo cha ukurugenzi wa ufundi.

Kuja kwa Lwandamina kunaashiria kuwa Yanga si watu wa mchezo mchezo linapokuja suala la kumwaga fedha kwani walikuwa na vita kubwa na Free State Star ya nchini Afrika Kusini ambao nao walikuwa wakimtaka Mzambia huyo.

Kigogo mmoja wa Wanajangwani hao aliwaambia waandishi wa habari kuwa kocha huyo atawasili leo ili kumalizana na uongozi ambapo anatarajiwa kuanza kazi mara moja kuhakikisha mabingwa hao watetezi wanatetea ubingwa wao.

“Kama Mungu akipenda kesho (leo) anaweza akatua hapa nchini ambapo atakutana na uongozi na kumalizia mazungumzo yao, nadhani ataanza kazi mara moja kwani lengo letu ni kupata changamoto mpya,” alisema.

Baada ya kupigiwa simu kocha huyo wa Zesco ya Zambia ambapo licha ya kukwepa kutaja siku anayokuja, alikiri kuanza kupanga nguo zake kwenye mabegi ili kuanza safari ya kuja nchini Tanzania.

“Nisingependa kuzungumza mengi sana ila kwa ufupi tu ni kwamba nipo kwenye maandalizi ya kuja huko japo siwezi kukueleza kwamba ni lini, hiyo ya kwamba ninakuja kesho (leo) mimi siwezi kuisemea,” alisema.

Kama kocha huyo atawasili leo ni wazi anaweza akaiangalia Yanga kwenye TV itakapocheza na maafande wa Tanzania Prisons katika mchezo utakaochezwa Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, au akaamua kwenda Uwanja wa Uhuru kuishuhudia Simba ikicheza na African Lyon.

Taarifa zaidi kutoka Yanga zinadai kuwa licha ya kwamba wanataka kumpa Pluijm cheo cha kuwa Mkurugenzi wa Ufundi, yeye mwenyewe hataki na huenda akatimka zake na kutafuta maisha sehemu nyingine huku taarifa nyingine zikidai kuwa Azam FC wanamvizia.

Yanga bado wanaendelea kulifanya jambo hili siri kwani hata kocha huyo alipokuja nchini mara ya kwanza kufanya nao mazungumzo na kusaini mkataba wa miaka miwili, walikataa kuliweka wazi japo inafahamika kuwa mambo yamekwenda vizuri.

Inadaiwa kwamba kilichomvutia Lwandamina kusaini mkataba na Yanga ni malipo manono ya kazi yake ambapo imedaiwa kuwa huenda akalipwa dola za Kimarekani 18,000 kwa mwezi, ambazo ni ongezeko kubwa kutoka dola 3,000 alizokuwa akilipwa katika klabu ya Zesco.

Source: Dimba
ZeroDegree.
Kocha Mzambia, George Lwandamina kuwasili leo Jangwani. Kocha Mzambia, George Lwandamina kuwasili leo Jangwani. Reviewed by Zero Degree on 11/06/2016 12:30:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.