Loading...

Moto wa Katiba mpya waibuka tena.

JUKWAA la Katiba Tanzania (JUKATA) limemshauri Rais Dk. John Magufuli kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kuhusu kukamilisha mchakato wa Katiba mpya.

Vilevile, limeishauri Serikali kutekeleza ahadi yake iliyoitoa kwenye mkutano wa Kimataifa wa Universal Period Review Mechanism (UPR),Mei 2016 Geneva, Uswisi.

Katika mkutano huo iliahidi kupitisha Katiba Mpya mapema iwezekanavyo.

Ahadi hiyo ya serikali ilitolewa wakati wa kuwasilisha hali ya haki za binadamu Tanzania chini ya mpango huo.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mratibu wa JUKATA, Hebron Mwakagenda, alisema katika Uchaguzi Mkuu uliopita, Rais Magufuli hakuwa mgombea binafsi bali alipitia kwenye chama cha siasa cha CCM ambacho kilikuwa na Ilani yake hivyo anapaswa kuitekeleza bila vikwazo.

Alisema kwa kuwa CCM iliwaahidi wananchi ambao ndiyo waliompigia kura Rais Dk. Magufuli, litakuwa ni jambo jema kutimiza ahadi hiyo kwa faida ya Taifa.

Mratibu huyo wa JUKATA alisema katika mkutano wa Kimataifa wa UPR wa Uswisi, Serikali ya Tanzania ilipokea mapendekekezo 227 na iliahidi kutekeleza mapendekezo 130 ikiwa ni pamoja na yale yanayohusu mchakato wa Katiba.

“Kwa kuanzia,Ibara 145 inayozungumzia kuendeleza utawala bora, demokrasia na uwajibikaji katika kipindi cha miaka mitano ijayo (2015 – 2020), CCM imeahidi kuwa itahakikisha serikali inatekeleza mambo kadhaa ikiwamo kwenye kifungu cha (g) kukamilisha mchakato wa kutunga Katiba mpya na kuanza kuitekeleza kwa mujibu wa Sheria ya mabadiliko ya Katiba.

“Katika mapendekezo hayo ya kimataifa serikali ya Tanzania ilikubali kufikiria kupitisha Katiba mpya mapema iwezekanavyo, kuitisha kura ya maoni ya Katiba, kuendeleza mchakato wa Katiba mpya ambao ni lazima uwe shirikishi na wenye kupata ushauri kutoka asasi za raia,”alisema Mwakagenda.

Alisema ni vema Rais Dk. Magufuli atekeleze ahadi hiyo kuendelea kulinda heshima ya Taifa katika ngazi za kimataifa.

Itakuwa ni fedheha kwa Serikali kushindwa ama kuacha kutekeleza ahadi ilizozitoa yenyewe, alisema.

Katika ushauri huo, Mwakagenda alisema Katiba mpya pekee ndiyo itamsaidia Rais Magufuli kuinyoosha nchi na kuirudisha kwenye mstari kama ambavyo amekuwa akizungumza mara kwa mara.

Alisema katiba hiyo pia itamfanya aache kumbukumbu ya kudumu katika mioyo ya watanzania baada ya kumaliza utawala wake.

“Kama alivyoahidi wakati akipokea taarifa ya Uchaguzi Mkuu 2015, Alhamisi Juni 23 mwaka huu alipoahidi kukamilisha sehemu ya mchakato wa Katiba iliyobaki,”alisema.

Wakati huo huo, JUKATA ilizindua kitabu cha mwongozo unaoitwa ‘Mwelekeo wa Katiba mpya Tanzania, tulikotoka, tulipo na tuendako’ kikiwa na lengo la kuelimisha wananchi na watunga sera kuanza rasmi mchakato wa Katiba mpya bila kuchelewa.

ZeroDegree.
Moto wa Katiba mpya waibuka tena. Moto wa Katiba mpya waibuka tena. Reviewed by Zero Degree on 11/21/2016 11:07:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.