Loading...

Serikali yatangaza kufuta Diploma ya ualimu.

SERIKALI imefuta diploma maalumu ya ualimu ambayo ilianzishwa kwa ajili ya kuongeza idadi ya walimu.

Itakumbukwa wakati Serikali inaanzisha diploma hiyo, ilikuwa inakabiliwa na upungufu mkubwa wa walimu wa somo la sayansi.

Diploma hiyo ilianzishwa na Serikali ya awamu ya nne, baada ya kujitokeza upungufu mkubwa kwa walimu wa masomo hayo na kutolewa kwenye vyuo mbalimbali, kikiwamo Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).

Kwa mujibu wa waraka uliotolewa na Serikali na kusainiwa na Kaimu Kamishna wa Elimu Tanzania, Nicolas Burreta, ambao umeanza kutumika mwaka wa masomo 2016/17 katika vyuo vya elimu vya Serikali na binafsi, wizara ilihusisha programu za mafunzo ya ualimu mwaka 2014/15 ili kukidhi mahitaji ya sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014.

Waraka huo, unasema hivi sasa wizara inaendelea na maandalizi ya sheria, kanuni na miongozo ya utekelezaji wa sera hii, ikiwamo uendeshaji na usimamizi wa mafunzo ya ualimu nchini.

Sehemu ya waraka huo inasema: “Kwa kuzingatia maandalizi yanaendelea, mwongozo wa utekelezaji wa programu za mafunzo ya ualimu ya mwaka 2016/17 utakuwa wa mafunzo ya ualimu kwa astashahada (cheti) na stashahada.

“Mafunzo hayo yataendeshwa kwa kutumia mtaala wa kitaifa ulioandaliwa na Taasisi ya Elimu Tanzania (TEA) wa mwaka 2009 kwa astashahada na stashahada. Kutokana na hali hiyo, wizara itakuwa inatoa maelekezo ya sifa za kujiunga na mafunzo ya ualimu.”

Pia unasema mafunzo hayo tarajali ya stashahada ya juu ya elimu ya sekondari yaliyokuwa yakitolewa kuanzia mwaka wa masomo 2014/15, yamehitimishwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (Nacte) na kutoa tuzo ya stashahada ya kawaida ya ualimu ya sekondari kwa wahitimu wa programu hiyo baada kukamilisha mwaka wa pili wa masomo.

Aidha, wanachuo wanaoendelea na mafunzo tarajali ya ualimu wa stashahada ya kawaida kwa kutumia mtaala wa Tuzo za Taifa za Elimu ya Ufundi (NTA), wataendelea na mafunzo yao na kuhitimisha kama ilivyopangwa.

“Programu ya mafunzo kazini ya stashahada ya elimu ya msingi iliyokuwa inatumia mtaala wa Tuzo za Taifa za Elimu ya Ufundi (NTA), imesitishwa ili kufanyiwa maboresho.

“Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), litatahini na kutoa tuzo ya mafunzo ya ualimu ya astashahada na stashahada kuanzia mwaka wa masomo 2016/17 na kuvitaka vyuo vya ualimu kuhusika kutoa mafunzo ya ualimu (astashahada na stashahada) pekee, bila kuchanganya kozi nyingine.

Source: Mtanzania
ZeroDegree.
Serikali yatangaza kufuta Diploma ya ualimu. Serikali yatangaza kufuta Diploma ya ualimu. Reviewed by Zero Degree on 11/15/2016 10:06:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.