Loading...

Simba wakimbilia Shirikisho la Soka Africa [ Caf ].

Rais wa Simba, Evance Aveva.
KLABU ya Simba imesema itabisha hodi hadi Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwa ajili ya kupata waamuzi wanaochezesha mechi za kimataifa, kusudi kuchezesha mechi yao yoyote itakayowahusisha dhidi ya watani zao Yanga.

Hata hivyo, kwa mujibu wa kanuni na taratibu za Caf, klabu sio mwanachama wa shirikisho hilo ila inaweza kufanya hivyo kupitia kwa shirikisho la soka la nchi husika, ambalo kwa Tanzania ni TFF.

Aidha, Rais wa Simba, Evans Aveva anatarajia kukutana uso kwa uso na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF),Jamal Malinzi kujua sababu za malalamiko yao kutosikilizwa kwa kipindi cha miaka miwili.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, msemaji wa Simba Haji Manara alisema sababu ya kubisha hodi CAF kutaka waamuzi wa kuchezesha dabi dhidi ya Yanga, ni ili kutendewa haki.

“Hatutacheza mechi yoyote dhidi ya Yanga kwa mwamuzi wa nyumbani, tunawaheshimu sana lakini tunataka awamu hii waamuzi wa nje, na tuko tayari kulipa sehemu ya mapato yetu waje nchini na wasaidizi wao,”alisema.

Alitolea mfano waamuzi Martin Saanya na Samwel Mpenzu kutotolewa maamuzi ya kuadhibiwa mpaka sasa kwa madai kuwa eti wanaendelea kuchunguzwa, wakati wamekuwa ni sehemu ya vurugu zilizotokea katika mechi dhidi ya Yanga hali iliyosababisha Rais John Magufuli kulaumu.

Msemaji huyo alizungumzia pia, sababu ya Rais Aveva kutaka kukutana na Malinzi limeafikiwa na Kamati ya Utendaji ya Simba iliyokutana Ijumaa iliyopita, hivyo kiongozi huyo atakwenda na barua nyingine za malalamiko yao.

Alisema zipo kesi kadhaa ambazo hadi sasa hazijafanyiwa kazi kiasi kwamba wanaona kuwa huonewa, na kuhisi kuwa hakuna maelewano mazuri baina ya taasisi mbili za Simba na TFF.

Mfano, alitaja kesi ya Hassan Kessy hajaafikiana na Yanga na hakuna maamuzi yoyote yaliyotolewa, kesi ya Singano kusajili Azam FC akiwa bado ana mkataba, kesi ya Tambwe na Ngoma kutenda madhambi kwa wachezaji wao, usajili wa Mbaraka Mohamed Kagera Sugar lakini pia, suala la ratiba kubadilishwa mara kwa mara pasipo kushirikishwa.

Kiongozi huyo alikosoa ratiba ya ligi kuwa walikuwa wakibanwa kwa mechi za karibu, wakati kwa sasa wanakaa mapumziko wa muda mrefu ambayo hayastahili kwani walihitaji wiki moja au mbili tu lakini sio mwezi mzima.

Pia, alisema anashangazwa na kitendo cha TFF kutowashirikisha kwa uandaaji wa mashindano mapya ya StarTimes,na badala yake hupelekewa barua za kuwataka kuthibitisha ushiriki wao. Mashindano hayo mapya yatashirikisha klabu mbili za Simba na Yanga kwa Tanzania na klabu nyingine za nje ya nchi yanatarajiwa kufanyika Desemba 16, mwaka huu.

Alisema baada ya kukutana, wanategemea mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania bara, kutakuwa hakutoshi kwani wamedhamiria kuendeleza makali yao na kuchukua taji la ligi.

Credits: Habari Leo
ZeroDegree
Simba wakimbilia Shirikisho la Soka Africa [ Caf ]. Simba wakimbilia Shirikisho la Soka Africa [ Caf ]. Reviewed by Zero Degree on 11/24/2016 10:31:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.