Loading...

Tathmini ya NEC kuelekea uchaguzi ujao ulio bora.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu, Jenista Mhagama akihutubia kwenye mkutano wa kukabidhiwa Taarifa ya Tathmini Baada ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa Mwaka 2015, kwenye ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Bungeni mjini Dodoma hivi karibuni. Kushoto ni Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Mmtaafu Damian Lubuva na Makamu Mwenyekiti wa NEC Zanzibar, Jaji mstaafu Hamid Mahmoud Hamid.
UCHAGUZI mkuu wa mwaka 2015 unatajwa kuwa wa kihistoria kutokana na kuwepo kwa ushindani mkubwa wa kisiasa nchini kulinganisha na zilizopita.

Ni wa kihistoria pia kwa kuwa kwa mara ya kwanza Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilitumia teknolojia ya Biometric Voters Registration (BVR) katika uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura. NEC imefanya tathmini kubaini mafanikio na changamoto zilizojitokeza wakati wa uandikishaji wa wapiga kura na uendeshaji wa uchaguzi na kuja na mapendekezo pamoja na mikakati itakayosaidia kuhakikisha changamoto zilizojitokeza zinashughulikiwa kwa lengo la kuboresha uchaguzi ujao.

Tathmini imefanyika katika mikoa 22 kati ya 30 iliyokuwepo wakati wa uchaguzi mkuu. Imehusisha halmashauri 64 kati ya 181, kata 192 kati ya 3,935 kwa Tanzania bara na shehia 12 kati ya 386 kwa Tanzania Zanzibar. Kwa mujibu wa mkurugenzi wa Uchaguzi Ramadhani Kailima, tathmini ililenga kupima utendaji kazi wa tume na kubainisha sababu wa uwepo wa mwitikio mdogo wa wapigakura kwa baadhi ya maeneo ikilinganishwa na idadi ya wapia kura waliojiandikisha.

Kailima anasema baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 tathmini ilifanyika kuanzia Februari 1 hadi 26, 2016 ikiwa ni hatua ya kukamilisha mzunguko wa uchaguzi. Anasema tathmini baada ya uchaguzi, ni hatua ya kwanza ya mzunguko wa uchaguzi kwa kuwa hutoa mwelekeo mzima ni nini kinahitajika kufanyika katika marekebisho na kuweka mikakati ya mifumo mipya ya utekelezaji katika kuelekea chaguzi nyingine zinazofuata.

Pia tathmini baada ya utekelezaji wa majukumu huziwezesha taasisi kujua ni kwa jinsi gani wadau wake wa ndani na nje wanavyoiona na kupima kiutendaji na hivyo kusababisha kuwa kichocheo cha matokeo chanya ya kufikia malengo ya utekelezaji.

Anataja nchi ambazo tathmini zimefanyika ni pamoja na Canada, Ghana, India, Kenya na Sierra Leone. Tanzania ambayo hufuata mzunguko wa uchaguzi unaodumu kwa miaka mitano, baada ya kutangazwa matokeo, tathmini ya mchakato wa uchaguzi hufanyika kujua hali halisi ya utekelezaji wa uchaguzi ulioisha na kutoa mwelekeo wa maandalizi ya mchakato wa uchaguzi unaofuata.

Katika uchaguzi huo jumla ya wapigakura waliojiandikisha walikuwa 23,161,440 na waliopigakura walikuwa 15,596,110 ambao ni sawa na asilimia 67.34 ya walioandikishwa. Hata hivyo inaonesha bado kuna changamoto kubwa ya watu kujitokeza kupiga kura. Takwimu zinaonesha katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, idadi ya wapigakura ambao hawakujitokeza ilipungua hadi kufikia asilimia 32.66 ikilinganishwa na mwaka 2010.

Takwimu zinaonesha mwaka 2010 wapigakura walioandikishwa walikuwa 10,088,484 waliojitokeza kupiga kura 8,517,598 sawa na asilimia 84.4, wapigakura ambao hawakujitokeza kupiga kura walikuwa 1,570,886 sawa na asilimia 15.57. Mwaka 2005 wapigakura walioandikishwa walikuwa ni 16,442,657, waliojitokeza kupiga kura ni 11,365,477 sawa na asilimia m 69.12 ambao hawakujitokeza kupiga kura walikuwa ni 5,077,180 sawa na asilimia 30.88.

Aidha mwaka 2010 wapigakura walioandikishwa ni 20,137,303, waliojitokeza kupiga kura ni 8,626,303 sawa na asilimia 42.84 ambao hawakujitokeza kupiga kura ni 11,511,000 sawa na asilimia 57.16. Katika uchaguzi wa mwaka 2015, waliojiandikisha ni 23,161,440, wapigakura waliojitokeza kupiga kura ni 15,596,110 sawa na asilimia 67.34 na ambao hawakujitokeza kupiga kura ni 7,565,330 sawa na asilimia 32.66.

Mkurugenzi huyo wa Tume ya Uchaguzi anasema pamoja na kuongezeka kwa waliojitokeza kupiga kura mwaka 2015 ikilinganishwa na mwaka 2010, bado idadi ya wapiga kura ambao hawakujitokeza ni kubwa na tume iliona umuhimu wa kujua sababu za baadhi ya wapiga kura kushindwa kujitokeza. Anasema matokeo ya tathmini yataiwezesha tume kubaini changamoto zilizojitokeza na kuweka mpango mkakati wa utekelezaji kwa ajili ya chaguzi zijazo.

Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Damian Lubuva anasema baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 Tume iliamua kufanya tathmini kupata mrejesho juu ya utekelezaji wa uchaguzi mkuu kutoka kwa wadau. Anasema lengo kuu la kufanya tathmini lilikuwa kupata taswira halisi ya tume kutoka kwa wadau na hivyo kujenga msingi bora wa utekelezaji wa uchaguzi ujao. Anasema tangu kuanzishwa kwa tume, Januari 13, 1993 ni mara ya kwanza tume kufanya tathmini baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Aidha mafanikio ya zoezi hilo yametokana na ushirikiano mkubwa uliooneshwa na wadau mbalimbali wa uchaguzi ambao kwa namna moja au nyingine walishiriki katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Anasema hata maeneo ambayo watendaji wa tume walipita kufanya mahojiano yalichaguliwa kwa kuzingatia vigezo muhimu ikiwa ni pamoja na maeneo yaliyokuwa na mwitikio mdogo wa wapiga kura, kwa maana ya asilimia 38 hadi 67 ikilinganishwa na idadi ya wapigakura waliojiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura.

Kwa kuzingatia kigezo hicho mikoa ya Tabora, majimbo ya Igalula, Nzega Vijijini na Katavi, Dar es Salaam majimbo ya Kawe, Temeke, Ubungo na Mbagala, Katavi majimbo ya Kuvuu, Mpanda vijijini na katavi yalichaguliwa. Pia maeneo yaliyokuwa na mwitikio wa wastani wa wapigakura wa asilimia 68 hadi 77 yaliyochaguliwa ni mkoa wa Mara, jimbo la Bunda Mjini na Bunda Vijijini.

Mikoa mingine na majimbo yake kwenye mabano ni Simiyu (Maswa Mashariki na Maswa Magharibi), Kilimanjaro (Moshi Mjini), Shinyanga (Shinyanga), Dodoma (Chemba), Lindi (Kilwa Kusini na Mtama) na mkoa wa Kigoma katika Jimbo la Buhigwe.

Anasema maeneo yaliyokuwa na mwitikio mkubwa wa wapiga kura asilimia 78 hadi 87 mikoa iliyoingizwa kwenye tathmini ni Kagera (Karagwe na Kyerwa), Manyara (Mbulu vijijini, Mbulu Mjini, Babati vijijini na Hanang), Mtwara (Nanyamba, Tandahimba, na Newala), Lindi (Liwale na Lindi Mjini), Arusha (Karatu), Njombe (Makete), Iringa (Kalenga) na mkoa wa Mbeya katika jimbo la Ileje.

Kigezo kingine cha tathmini kilikuwa ni ushindani mkubwa wa kisiasa na ambako vyama vingi vikisimamisha wagombea wa nafasi mbalimbali. Aidha maeneo yaliyoathiriwa na hali mbaya ya hewa hususan mvua kubwa, wakati wa uchaguzi mkuu na maeneo ambayo hayafikiki kwa urahisi kutokana hali ya kijiografia kama vile visiwa, miinuko, mabonde na maeneo ya mbuga za wanyama.

Mwenyekiti huyo anasema pamoja na kujua mtazamo wa wadau juu ya taswira ya tume, matokeo ya tathmini yataisaidia tume katika kujitathmini katika maeneo mbalimbali ya kiutendaji ikiwemo kurekebisha sheria, kanuni na masuala ya kisera na kufanya mapitio ya mpango mkakati wa tume na mkataba wa huduma kwa wateja. Aidha tathmini hiyo itasaidia kutenganisha majukumu ya utoaji elimu ya mpigakura na kutofautisha elimu ya mpigakura na elimu ya uraia katika uchaguzi.

Anasema baada ya tathmini hiyo kufanyika tume imejiridhisha kupitia maoni ya wadau waliohojiwa kwamba sheria, kanuni na maelekezo yaliyotumika wakati wa uchaguzi mkuu yalikuwa chachu ya kufanikisha uchaguzi mkuu. Pia watendaji wa uchaguzi walionesha kuwa na uelewa wa kutosha wa sheria na kanuni za uchaguzi na wadau wengi walionesha kuridhishwa na utendaji wa tume katika kusimamia uchaguzi mkuu na kutangaza matokeo kwa kufuata sheria na kanuni zilizopo.

Anataja changamoto zilizojitokeza kwa mujibu wa wadau waliohojiwa ni pamoja na mpigakura kutoruhusiwa kupiga kura katika eneo tofauti na lile alilojiandikisha. Pia wapigakura kushindwa kupiga kura siku ya uchaguzi kutokana na kugawanywa kwa mipaka ya kiutawala na majimbo ya uchaguzi baada ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura na muda mfupi uliotolewa kujiandikisha na uwekaji wazi wa daftari la awali la wapigakura.

Aidha wadau walipendekeza yafanyike mabadiliko ya kisheria kuhusu vipengele vya kisheria ili kuleta ufanisi zaidi Mwenyekiti huyo anasema matokeo kuhusu mwitikio wa wapigakura tathmini imeonesha kuwa katika baadhi ya maeneo watu waliojitokeza kupiga kura ni wachache ikilinganishwa na idadi ya wapigakura waliojiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapigakura.

“Baadhi ya sababu zilizotolewa ni pamoja na uelewa mdogo juu ya umuhimu wa kupigakura kutokana na elimu ya mpigakura kutowafikia wapigakura walio wengi, wapiga kura waliojiandisha katika daftari la kudumu la wapigakura ili kupata kadi kwa ajili ya matumizi mengine na uwepo wa hofu na vitisho na vurugu siku ya kupiga kura” anasema. Anasema mapendekezo yaliyotolewa kurekebisha changamoto hizo ni pamoja na uboreshaji endelevu wa daftari la kudumu la wapigakura.

Pia serikali ifanye mapitio ya sheria ya taifa ya uchaguzi, sura 343 na sheria ya serikali za mitaa sura 292 ili kurekebisha vifungu vinavyokinzana. Aidha serikali kubadili muundo wa NEC ili kuwa na ofisi na watumshi katika kila halmashauri nchini na ofisi Zanzibar. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana na Watu Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama anasema tume inapaswa kupongezwa kwa kukamilisha kazi nzima ya uchaguzi mkuu ambayo ilikuwa na changamoto nyingi na ushindani mkubwa wa kisiasa.

Source: Habari Leo
ZeroDegree.
Tathmini ya NEC kuelekea uchaguzi ujao ulio bora. Tathmini ya NEC kuelekea uchaguzi ujao ulio bora. Reviewed by Zero Degree on 11/22/2016 08:39:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.