Loading...

Utata sakata la mrembo Arusha alivyobakwa hadi kufa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo.
HATIMAYE jeshi la Polisi limeeleza kilichotokea kuhusiana na utata uliokuwa ukitawala juu ya taarifa za kubakwa hadi kufa kwa msichana mmoja wa Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira jijini Arusha.

Katika taarifa rasmi jana, ambayo sasa inasaidia kuondoa utata wa taarifa tofauti zilizosamabaa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii kuhusiana na tukio hilo, zinaeleza kuwa alama za kucha zilizopatikana shingoni mwa msichana aliyekutwa amekufa juzi asubuhi eneo la Makumira, zinaonyesha alibakwa kabla ya kuuawa, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, alisema.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisi kwake jana jijini hapa, Mkumbo alisema katika kuchunguza mwili huo ambao uliokotwa ukiwa mtupu na nguo zake kuwekwa pembeni yake, wamebaini alama za kucha shingoni na uvimbe sehemu za siri, jambo linaloonyesha kwamba alibakwa.

Msanii wa nyimbo za kiutamaduni, Juliana Issa (22), anayefanya shughuli zake katika Kituo cha Utamaduni kilichopo kwenye Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira wilayani Arumeru, alikutwa amekufa na mwili wake kutupwa kwenye majaruba ya mpunga.

Mwili huo uliokotwa juzi majira ya saa 5:30 asubuhi eneo la Makumira.

Kamanda Mkumbo alisema taarifa za awali zinaeleza kuwa Jumanne muda wa saa 12:30 jioni, Juliana aliondoka nyumbani kwao akiaga kwamba anakwenda kwenye sherehe ya kuzaliwa rafiki yake.

Alisema sherehe hiyo ilipangwa kufanyika kwenye baa iliyoko eneo la Kilala, lakini Juliana hakuonekana kwenye sherehe hiyo.

Siku ya pili (juzi), polisi walipata taarifa juu ya kuwapo kwa mwili ambao umekutwa kando ya barabara na baada ya askari kufika eneo hilo, walikuta mwili huo ukiwa mtupu na pembeni yake kulikuwa na nguo zake.

Alisema hadi sasa chanzo cha kifo hicho bado hakijajulikana na hakuna mtuhumiwa yeyote aliyekamatwa licha ya msako unaoendelea ili kuwabaini wahusika wa tukio hilo.

Mwili wa marehemu ulihifadhiwa katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru, kwa ajili ya uchunguzi zaidi wa daktari.

Mratibu wa Kituo cha CAC, Randy Stubbs, aliiambia Nipashe kuwa amehuzunika na kifo cha msanii huyo ambaye kwake alikuwa ni kama mtoto aliyemuhasili.

Alisema juzi alimwomba ruhusa kuwa anakwenda kwenye sherehe ya kuzaliwa ya rafiki yake ambaye hakumtajia jina lake, lakini hakurudi nyumbani na kila alipokuwa akimpigia simu ilikuwa haipolekewi na baadaye ilikuwa haiiti kabisa.

Alisema walihangaika pamoja na wasanii wenzake zaidi ya 25 wa kituo hicho kumtafuta bila mafanikio na juzi majira ya 5:30 asubuhi, walipata taarifa kuwa mwili huo umepatikana maeneo hayo.

Alisema msiba huo ni pigo kwao na wanasubiri taarifa za polisi na hospitali ili waweze kufanya taratibu za mazishi lakini wameumizwa na kifo hicho.

Source: Nipashe
ZeroDegree.
Utata sakata la mrembo Arusha alivyobakwa hadi kufa. Utata sakata la mrembo Arusha alivyobakwa hadi kufa. Reviewed by Zero Degree on 11/04/2016 10:05:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.