Loading...

Kingunge atoa ya moyoni.

Mwanasiasa mkongwe, Kingunge Ngombale-Mwiru.
BAADA ya ukimya wa muda mrefu, mwanasiasa mkongwe, Kingunge Ngombale-Mwiru, amesema nyakati hizi ni vigumu kupata viongozi wa aina ya Mwalimu Julius Nyerere, wasiotumia uongozi kwa maslahai binafsi.

Kingunge ambaye ni mwanzilishi wa CCM, aliyejiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alisema hayo juzi katika mahojiano maalumu na waandishi wa habari nyumbani kwake jijini Dar es Salaam.

“Ni vigumu kwa nchi zetu za Kiafrika kupata viongozi wa aina ya Mwalimu Nyerere na Fidel Castro wa Cuba (alifariki wiki iliyopita) hivi sasa utakuta mtu anasema anapigania wanyonge lakini badala yake anawanyanyasa,”alidai.

Alisema Nyerere na Castro walifanana kwa mambo mengi hadi kufikia hatua ya kuanzia vyama kwa lengo la kuendesha mapambano ya ukombozi.

“Castro alikuwa na kauli mbiu madaraka unayatumia kwa jambo gani, unapinga dhuluma na uonevu, hata, Mwalimu Nyerere alikuwa na kauli mbiu kama hiyo hiyo,”alisema.

Kingunge alisema enzi za Mwalimu Nyerere mambo mengi yalifanikiwa kwa sababu ya kuruhusu demokrasia japo kulikuwa na mfumo wa chama kimoja cha siasa.

“Katika Azimio la Arusha tulisema hatuwezi kuwa na nchi ya kijamaa halafu nchi yenyewe siyo ya kidemokraisa, sasa hivi tunapondaponda tu mambo, watu wanataka haki, wanataka uhuru wao,”alisema.

Aliongeza kuwa Castro alikuwa kama Mwalimu Nyerere kwa kuwa alikuwa kiongozi anayetafuta madaraka kwa ajili kutetea maslahi ya wananchi wake tofauti na sasa ambapo baadhi ya viongozi wanayataka madaraka kwa maslahi binafsi.

Kingunge alisema katika historia kuna makundi ya aina mbili, watu wanaokandamizwa na wanaonyonywa.

“Hao wanaonyonywa wanapopata mwamko kudai haki zao huanzisha harakati za mapambano na wanyonyaji na katika harakati hizo wakati mwingine waliokuwa wanaonewa hushinda au kushindwa,”alisema.

Akizungumzia mahusiano ya Cuba na Tanzania, alisema nchi hizo zilijenga mahusiano na nchi za Afrika ambazo zilikuwa katika vuguvugu za kuleta unafuu kwa wananchi wake.

Alisema Cuba chini ya Rais Castro ilikubaliana kusaidia nchi huru za Afrika afya na elimu.

“Hapa Tanzania Castro alikubaliana na Nyerere na zikajengwa sekondari maeneo mbalimbali na katika sekta ya afya madaktari kutoka Cuba waliletwa nchini kusaidia kutoa huduma,”alisema.

Source: Nipashe
ZeroDegree.
Kingunge atoa ya moyoni. Kingunge atoa ya moyoni. Reviewed by Zero Degree on 12/04/2016 07:04:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.