Loading...

Mama adaiwa kutelekeza watoto 6 mkoani Arusha.

WATOTO sita wa familia moja wametelekezwa na mama yao mzazi, Tekira Ngalawa kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa na inaelezwa amekimbilia Tarakea, wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro kwa lengo la kutafuta maisha.

Kutokana na hali hiyo, wasamaria wema wameanza kujitokeza kuwasaidia watoto hao ambao tangu Julai mwaka jana walipotelekezwa na mama yao, wamekuwa wakiishi kwa fadhila za majirani. Miongoni mwa wasamaria hao ni mfanyabiashara wa jijini hapa, Philemon Mollel 'Monaban’ ambaye jana alikabidhi misaada mbalimbali.

Akikabidhi, alisema nyumbani kwa watoto hao wanaoishi katika nyumba ya kupnga yenye vyumba viwili eneo la Moshono mjini hapa, Mollel alisema familia hiyo inayoteseka, inahitaji msaada wa hali na mali.

Mollel alimkabidhi Gloria Felix (20) ambaye ni mtoto wa huyo mama ambaye pia ana watoto wawili, mmoja ana miaka mitatu na wa pili mwaka mmoja, msaada wa unga kilo 20, mafuta ya kupikia ndoo moja, maharage kilo tano, sukari kilo tano na mikate kumi.

Akipokea msaada huo huku akibubujikwa machozi, Gloria alisema hakutegemea kupata msaada wowote kwa kuwa jamii ilikuwa haina taarifa za wao kutelekezwa na mama yao ambaye aliwaaga kuwa anakwenda Tarakea kutafuta kazi, huku akiwaahidi kuwa angerejea, lakini hajaweza kufanya hivyo.

Mtoto mwingine, Victoria Msangi (15) ambaye amefaulu kujiunga na kidato cha kwanza mwakani amewaomba wasamaria wema kuwasaidia ili waweze kukabiliana na hali ngumu ya maisha.

Akizungumzia kuhusu msaada huo, Gasper Kishumbua, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM wilayani Arusha, alisema alifanikiwa kuibua familia hiyo baada ya kufanya ziara ya kukagua uhai wa chama katika Kata ya Moshono.

Kuhusu Msangi, alisema tayari Jumuiya ya Wazazi ya CCM imejitolea kumnunulia sare za shule, viatu na madaftari ila wanachongojea ni Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Fabian Daqqaro kukamilisha mipango ya kumtafutia shule ya bweni ili asome vizuri.

Johnson Erik (16) ambaye aliishia darasa la sita mwaka jana ameomba asaidiwe kurejee shuleni, kwani hana sare za shule, viatu na vitabu.

Aidha Kishumbua amemtaka Mama Tekira Ngalawa popote alipo awasiliane naye kwa simu ya mkononi namba 0713 244 994 ili wamsaidie kazi ya kufanya na aweze kuhudumia watoto wake.

Pia ametoa mwito kwa mtu yeyote atakayeguswa na ugumu wa maisha wa watoto hao afike ofisi za CCM Wilaya ya Arusha, eneo la Fire ili watoto hao waweze kusaidiwa.

Source: Habari Leo
ZeroDegree.
Mama adaiwa kutelekeza watoto 6 mkoani Arusha. Mama adaiwa kutelekeza watoto 6 mkoani Arusha. Reviewed by Zero Degree on 12/21/2016 12:35:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.