Loading...

Serikali yatangaza Ajira za Walimu wa Sayansi.

BAADA ya kusitisha ajira za umma kwa takribani miezi tisa, hatimaye serikali imetangaza ajira kwa wahitimu wa ualimu kwa shule za sekondari.

Hata hivyo, ajira mpya zilizotangazwa na serikali jana, zinawahusu walimu wa ngazi ya stashahada na shahada ya ualimu wa masomo ya sayansi na hisabati kwa shule za sekondari.


Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Maimuna Tarish, na kuchapishwa kwenye tovuti rasmi ya wizara hiyo, serikali inatarajia kuajiri walimu wa masomo ya sayansi na hisabati kwa shule za sekondari waliohitimu mwaka jana.

Hata hivyo, idadi ya walimu wanaohitajika kwa ajili ya kufundisha masomo hayo haikuelezwa katika tangazo hilo. "Ajira hii ni kwa walimu wa stashahada na shahada za mafunzo ya ualimu wa masomo ya hisabati na sayansi waliohitimu mwaka 2015.

Wahitimu hao wanatakiwa kuwasilisha nakala za vyeti vyao vya elimu ya sekondari (kidato cha nne na sita) na taaluma ya ualimu (stashahada na shahada) kwa ajili ya uhakiki.

"Nakala hizo ziwasilishwe kupitia barua pepe ya wizara info@moe.go.tz kuanzia tarehe ya tangazo hili (jana) hadi Ijumaa Desemba 16, 2016.

Yeyote ambaye vyeti vyake havitahakikiwa, hatafikiriwa katika ajira," tangazo hilo lilieleza. Katika mwaka huu wa fedha, serikali imepanga kuajiri watumishi 71,496 kwenye sekta mbalimbali zikiwamo elimu, afya na viwanda.

Pamoja na kutaja idadi ya watumishi wapya wanaotarajiwa kuajiriwa kwenye mwaka huu wa fedha, Serikali ya Awamu ya Tano ilikuwa haijaweka bayana ni lini hasa ajira hizo zitaanza kutolewa huku ikiwa imebaki miezi sita mwaka wa fedha wa 2016/17 kumalizika.

Wiki iliyopita, akijibu maswali yaliyoulizwa na Nipashe juu ya lini Serikali itaanza kutoa ajira baada ya kuzisitisha kwa muda, Mkuu wa Mawasiliano Serikalini, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Florence Temba, alisema katika sekta ya elimu kutakuwa na ajira 28,957.

Katika majibu hayo aliyoyatoa kwa niaba ya Katibu Mkuu Utumishi, Dk. Laurean Ndumbaro, Temba alisema mbali na elimu, sekta ya afya itakuwa na ajira mpya 10,870, kilimo 1,791, mifugo 1,130, huku maeneo mengine ambayo hayakutajwa yakitarajiwa kuwa na ajira 28,748.

Wakati Utumishi ikisema hayo, hivi karibuni Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Ezekiah Oluoch, alilieleza gazeti hili kuwa kwa sasa kuna walimu 30,000 mtaani ambao hawana ajira licha ya kuhitimu masomo yao.

Alisema hao ni wale waliomaliza masomo mwaka jana na kwamba wataongezeka baada wengine kuhitimu mwaka huu.

Makamu wa Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk. Obadia Nyongela, pia aliiambia Nipashe mwishoni mwa wiki iliyopita kuwa sasa kuna madaktari 1,700 mtaani ambao wana sifa, lakini hawajaajiriwa.

"Kama mwaka huu utaisha bila vibali vya ajira kutoka, maana yake mpaka mwakani kutakuwa na madaktari 2,866 wasio na ajira licha ya kuwapo kwa upungufu wa wataalamu hao," alisema Dk. Nyongela.

Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas), Profesa Ephata Kaaya, alisema wanaendelea kuzalisha wataalamu hao kwa sababu wanajua bado Tanzania ina upungufu wa madaktari.

Machi 12, mwaka huu, Serikali ilielekeza kufanyika kwa zoezi la uhakiki wa watumishi hewa kwa kukagua vyeti vya kazi wanavyotumia kwa lengo la kuhakikisha usimamizi na uwajibikaji.

Hata hivyo, Katibu Mkuu Utumishi, Dk. Ndumbaro, Juni 12, mwaka huu, alisema sababu nyingine iliyopelekea kusitisha ajira ni kupitia upya muundo wa Serikali ya Awamu ya Tano na taasisi zake.

Kutokana na uamuzi huo, alisema nyongeza ya mishahara kwa watumishi wa Serikali na wakala zake pamoja na utoaji wa vibali vya likizo ya bila malipo ulisitishwa kwa muda hadi zoezi lilipokamilika.

Baada ya kusitishwa kwa ajira, taarifa zilisambazwa katika halmashauri zote na idara za Serikali kutekeleza maelekezo yaliyotolewa na wizara Juni 13, mwaka huu kusitisha ajira hadi pale uhakiki utakapokamilika.

Hata hivyo, katika mkutano wake na wahariri wa vyombo vya habari uliofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam mwezi uliopita, Rais John Magufuli alisema pamoja na serikali anayoiongoza kusitisha ajira hadi pale uhakiki wa watumishi hewa utakapomalizika, aliruhusu ajira zitolewe kwa askari waliokuwa kwenye mafunzo na madaktari waliokuwa wanahitajika Muhas.

ZeroDegree.
Serikali yatangaza Ajira za Walimu wa Sayansi. Serikali yatangaza Ajira za Walimu wa Sayansi. Reviewed by Zero Degree on 12/14/2016 10:40:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.