Loading...

Shirikisho la Soka Tanzania [ TFF ], watoa zawadia ya gari kwa mwamuzi.

Rais wa TFF, Jamal Malinzi akimpongeza mwamuzi Jonesia Rukyaa kwa kuchezesha kwa mafanikio mechi za mashindano ya Afrika kwa wanawake yaliyofanyika Cameroon wiki iliyopita. TFF pia imemzawadia gari mwamuzi huyo. Kulia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Soka la Wanawake Tanzania (TWFA), Rose Kisiwa.
MWAMUZI wa soka wa kike wa Kimataifa, Jonesia Rukyaa amezawadiwa gari aina ya Toyota Vitz na Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF) kama pongezi kwa kuchezesha kwa mafanikio mechi za fainali za Afrika za Wanawake zilizofanyika Cameroon hivi karibuni.

Akizungumza wakati wa hafla ya kumpongeza Jonesia, Rais wa TFF, Jamal Malinzi alisema amefurahi kwa kiwango ambacho Jonesia amekionesha hadi kufanikiwa kuchezesha mchezo wa mshindi wa tatu kati ya Afrika Kusini na Ghana kwenye fainali hizo.

“Jonesia ameitangaza Tanzania kwa kiwango ambacho amekionesha, sasa kamati ya waamuzi mnatakiwa mfanye kazi ya kuwazalisha akina Jonesia wengi kutoka kwa wanaume na wanawake,” alisema Malinzi akimueleza mwenyekiti wa kamati ya waamuzi, Salum Chama aliyekuwa kwenye hafla hiyo.

Pia Malinzi alisema ana imani Jonesia atachezesha fainali zijazo za Afrika na fainali zijazo za dunia kwani kwa sasa ni kati ya waamuzi bora watano barani Afrika kwa wanawake.

Naye Jonesia Rukyaa aliwashukuru wadau wote wa soka kwa michango yao mbalimbali ambayo wamekuwa wakimpatia kwani imemjenga na kumfanya kuwa bora na kutoa rai wanawake kuendelezwa kwani wanaweza.

“Kiukweli sikutarajia kuchaguliwa kuchezesha fainali za wanawake barani Afrika kwani kwenye semina nilikutana na waamuzi wenye uzoefu zaidi ya miaka kumi huku mimi nikiwa na uzoefu wa miaka mitatu,” alisema Jonesia.

Pia aliishukuru TFF na Kamati ya waamuzi kwa kumpanga kuchezesha mechi za ligi hasa za Simba na Yanga kwani zimemjenga na kumpa uzoefu. Jonesia alisema katika fainali hizo walianza kuchezesha wakiwa waamuzi 11 lakini walimaliza wanane tu kwani kila mwamuzi aliyechezesha vibaya aliondolewa.

ZeroDegree.
Shirikisho la Soka Tanzania [ TFF ], watoa zawadia ya gari kwa mwamuzi. Shirikisho la Soka Tanzania [ TFF ], watoa zawadia ya gari kwa mwamuzi. Reviewed by Zero Degree on 12/09/2016 10:12:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.