Loading...

TFF yaifilisi Stand Utd.


Dar es Salaam. Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), chini ya makamu mwenyekiti Wakili Mandi imeitaka Stand United kulipa deni la Sh100.3 milioni inazodaiwa na wachezaji na makocha wake.

Kamati hiyo iliyokutana mwishoni mwa wiki na kupitia kesi, mashauri mbalimbali kuhusiana na usajili na mikataba ya wachezaji na viongozi na kutoa hukumu kwa klabu za ndogo za Ligi Kuu pamoja na Ligi Daraja la Kwanza.

Uamuzi huo ni pigo kwa uongozi mpya wa Stand United uliokabidhiwa madaraka hivi karibuni kwa kuwa klabu hiyo italazimika kukatwa fedha zake za udhamini wa Ligi Kuu pamoja na zile za viingilio ili kufidia malimbikizo ya madeni ya wachezaji wake sambamba na makocha wa timu hiyo.

Kamati hiyo imeitaka Stand United, ilimpe aliyekuwa mchezaji wake Mutabuzi Peter kiasi cha Sh2 milioni ikiwa ni malimbikizo ya mshahara na fedha hizo zilipwe ndani ya mechi nane zijazo za Ligi Kuu. Wengine wanaotakiwa kulipwa ni aliyekuwa kocha msaidizi wa timu hiyo Emmanuel Masawe anayedai Sh12 milioni, lakini madai yake yamewekwa kiporo kutokana na kutokuwapo kwenye kikao hicho.

Mchezaji Ndikumana Hamad anaidai Stand United, Sh11 milioni malimbikizo ya mshahara wake, malazi na chakula, kamati hiyo imemrejesha Ndikumana kuitumikia klabu hiyo.

Kocha wa timu hiyo Ben Kalama anadai pia malimbikizo ya mshahara wake Dola 1,350, imeamuriwa arudi kuendelea kuinoa timu hiyo na kwamba watalipana kwenye vyanzo vya mapato na TFF.

Naye Mathias Lule anaidai Stand mshahara, posho na bima ya afya kiasi cha Sh48.3 milioni, aliwakilishwa na Fadhil Hussein. Ilikubaliwa alipwe kiasi cha dola 4,300.00.

Stand pia imetakiwa kuilipa Jaki Footbal Academy Sh4.2 milioni kutoka kwenye vyanzo vyao vya mapato baada ya klabu hiyo kuwasilisha malalamiko dhidi ya timu hiyo yenye maskani yake mjini Shinyanga kuidai Sh7.6 milioni.

“Muhibu Kanu dhidi ya Stand United anayeidai mishahara na posho klabu ya Stand United kiasi cha Sh.16.6 milioni. Makubaliano yamefikiwa kweli Muhibu ameshaanza kulipwa kupitia Bodi ya Ligi kiasi cha Sh2.6 milioni hivyo kiasi kilichobakia cha Sh14 milioni,” ilisema sehemu ya taarifa ya TFF.

Mbali na Stand United, timu ya nyingine zilizokumbwa na balaa hilo ni Ndanda iliyotakiwa kuwalipa wachezaji wake Said Mketo (Sh2.7 milioni), Saleh Malande (Sh2 milioni) na Rajabu Isihaka (Sh3.7 milioni), Meshack Wilfredy (Sh2 milioni). Hata hivyo Ndanda haikutuma mwakilishi hivyo imeamuriwa ieleze namna ambavyo itawalipa wachezaji hao.

Polisi Dodoma itailipa Changanyikeni Sh400,000 kama fidia ya mchezaji wake Said Athumani waliomsajili bila ya kufuata utaratibu, fedha hizo zitakatwa kutoka kwenye fedha za udhamini wa Ligi Daraja la Kwanza. Pia, kamati hiyo imeamua kujiridhisha kama timu ya Polisi Tabora ilipata kibali cha rais wa TFF, Jamali Malinzi kumtumia mchezaji Michael Chinidu bila ya kulipa dola 2,000 kwa mujibu wa kanuni, huku ikitupilia mbali kesi ya Mohamed Jingo kuwa siyo raia kwa kuwa kamati hiyo haina mamlaka ya kuthibitisha au kuamua uraia wake.

“Rufaa nyingine ilikuwa ni ile ya Mawezi Market dhidi ya Burkina Faso kumsajili mchezaji Victor Mswaki kinyemela inatakiwa kulipa Sh 370,000.”


ZeroDegree.
TFF yaifilisi Stand Utd. TFF yaifilisi Stand Utd. Reviewed by Zero Degree on 1/20/2016 03:49:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.