Wabunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wakabidhiwa Rungu.
Dodoma. CCM imewataka wabunge wake kuikomalia Serikali badala ya kupongeza kila kitu kinachofanywa na mhimili huo ili kusimamia masilahi ya wananchi, habari kutoka ndani ya semina ya kuwanoa kujiandaa kwa Mkutano wa Pili wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, zimeeleza.
Hakuna taarifa rasmi iliyotolewa na chama hicho tawala kuhusu yaliyojiri kwenye kikao hicho, lakini wabunge waliozungumza na gazeti hili walidokeza kuhusu maagizo hayo ya kutoikalia kimya Serikali ya chama hicho.
Semina hiyo ya siku mbili ilifanyika kwenye ukumbi wa White House, makao makuu ya CCM mjini hapa kabla ya kamati za Bunge wa chama hicho kukutana leo.
Makamu Mwenyekiti wa CCM, Phillip Mangula aliongoza watoa mada kwenye semina hiyo akiwa na Spika wa zamani, Pius Msekwa na Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana.
Kinana ambaye alifanya ziara nchi nzima kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, alikuwa akiahidi kuwapa meno wabunge wa CCM ili waibane Serikali, huku akiponda mawaziri walioonekana kutowajibika ipasavyo.
Mbunge mmoja aliyeomba asitajwe jina gazetini alisema: “Tutafanya kazi ya kupongeza pale inapobidi tu, lakini maeneo mengine lazima tulie nayo kwa ajili ya masilahi ya wapigakura wetu. Katibu katuambia hakuna mahali popote ambako Kamati Kuu ya CCM imekuwa ikiagiza eti wabunge kuitetea Serikali isipokuwa huwa ni mbinu ya baadhi ya watu kutaka kuficha maovu yao kwa kisingizio cha maagizo ya chama.”
Habari kutoka ndani ya semina hiyo, zinaeleza kuwa suala la bomoabomoa pia lilijitokeza baada ya wabunge wengi kulalamika kuwa linawagombanisha na wapigakura wao kutokana na kasi yake kuwa zaidi ya matarajio yao.
Hata hivyo, ufafanuzi kutoka kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi pamoja na Mwanasheria Mkuu, George Masaju ilitosha kuzima moto wa wabunge. Waziri Lukuvi aliwaambia kuwa wakiachia jambo hilo, linaweza kusababisha madhara makubwa baadaye kuliko ilivyo sasa.
ZeroDegree.
Wabunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wakabidhiwa Rungu.
Reviewed by Zero Degree
on
1/20/2016 03:57:00 PM
Rating: