Loading...

Vincent Angban, Ndusha kwaheri Msimbazi.

Kipa Vincent Angban.
WAKATI dirisha dogo la usajili la Ligi Kuu ya Tanzania Bara likitarajiwa kufungwa leo usiku, kipa Vincent Angban na kiungo Mussa Ndusha, hawana chao katika kikosi cha Simba.

Wawili hao wanatajwa kutemwa ili kupisha usajili wa kipa Daniel Agyei na kiungo mwenye uwezo mkubwa kwenye dimba James Koite.

Kiungo Mussa Ndusha
Taarifa kutoka kwenye kikao cha kamati ya utendaji na ile ya usajili zilizokutana wiki hii, zinadai kuwa wawili hao wanapewa mkono wa kwaheri.

Baada ya taarifa hizo kuvuja, alitafutwa Katibu wa Kamati ya Usajili ya Simba, Kasim Dewji, ambapo alisema kila kitu kitawekwa bayana leo.

“Subiri mpaka kesho (leo) ndiyo kila kitu tutakiweka wazi, kwa sasa siwezi kuzungumza chochote,” alisema Dewji.

Taarifa zaidi zinasema kuwa tayari Angban anaondoka moja kwa moja, lakini Musa Ndusha wanamfanyia mpango wa kwenda kucheza Oman.

Simba kwa sasa ina wachezaji saba wa kigeni ambao ni Method Mwanjali (Zimbabwe), Juuko Murushid (Uganda), Jarvier Bukungu (Congo), Frederick Blagnon (Ivory Coast) na Laudit Mavugo (Burundi), Agyei na Koite (Waghana).

Katika hatua nyingine, kocha msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja, amesema neno ambalo huenda lisiwafurahishe mashabiki wa Ndanda.

Mayanja alisema kikosi chake kitaanza mzunguko wa pili kwa kuhakikisha wanawaadabisha wapinzani wao hao wakiwa nyumbani kwao, kwani lengo lao ni kutwaa ubingwa msimu huu baada ya kusubiri kwa misimu minne mfululizo bila mafanikio.

“Tupo kileleni na hatutaki kabisa mtu atushushe, hivyo tunauchukulia mchezo wetu dhidi ya Ndanda kwa uzito mkubwa na tutahakikisha tunawafunga hata kama watakuwa uwanja wao wa nyumbani.

Tunafahamu kwamba utakuwa mchezo mgumu kwetu, kwani wenzetu watataka kushinda ikizingatiwa kuwa mchezo wa mzunguko wa kwanza tuliwafunga lakini yote kwa yote sisi tumejipanga kisawasawa,” alisema.

Alisema kikosi chake hadi jana kilikuwa hakina majeruhi na kiliendelea na mazoezi kujiandaa na mchezo huo ambao wanauchukulia kwa uzito mkubwa.

Source: Bingwa
ZeroDegree.
Vincent Angban, Ndusha kwaheri Msimbazi. Vincent Angban, Ndusha kwaheri Msimbazi. Reviewed by Zero Degree on 12/15/2016 01:17:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.