Balozi Seif aweka hadharani mbinu itakayotumiwa na CCM katika uchaguzi mkuu 2020
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi ameonya kwamba wembe ule ule uliotumika katika mchakato wa kumpata Mgombea wa CCM katika kinyang’anyiro cha Uchaguzi Mkuu wa Rais wa Tanzania Mwaka 2015 ndio utakautumika katika kumpata mgombea wa Chama hicho upande wa Zanzibar ifikapo uchaguzi wa mwaka 2020.
Alisema wembe huo ndio silaha pekee itayosaidia kusafisha virusi vitakavyojaribu kuibuka ndani ya chama hicho endapo yatatokea makundi yatayoashiria kutaka kukiyumbisha Chama hicho wakati utakapokaribia mchakato wa Uchaguzi huo.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa onyo hilo hapo Nyumbani kwake Kama wakati akizungumza na Viongozi wa CCM kata ya Mtoni Jimbo la Temeke Mjini Dar es salaam ambao wapo Zanzibar kwa mwaliko wa wenyeji wao Kamati ya Ujirani Mwema ya Mkoa wa Magharibi Unguja kwa ajili ya kuhudhuria sherehe za Maadhimisho ya kutimia Miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Alisema Chama cha Mapinduzi hakitawaonea haya wanachama wowote wenye sura mbili na itakapobidi italazimika chama hicho kusafisha takataka hizo hasa katika kipindi hichi cha mpito kuelekea kwenye uchaguzi ndani ya chama chenyewe.
Balozi Seif alisema inasikitisha kuona kwamba wapo baadhi ya viongozi wa chama hicho waliowahi kudiriki kununua kadi cha Chama na kuwapa baadhi ya Watu wengine wakiwemo wapinzani ili wawachague katika kura za maoni na hatimae wapinzani hao walitumia mwanya huo kuvuruga malengo na mikakati ya Chama cha Mapinduzi.
Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CCM Taifa aliwakumbusha Viongozi na wanachama wa Chama cha Mapinduzi walazimike kufanya kazi ya ziada katika kuwabaini wanafiki hao wenye sura mbili wanazozitumia katika kutoa maamuzi yao wakati wa uchaguzi ndani ya chama.
Akizungumzia Maadhimisho ya sherehe za kutimia miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar Balozi Seif alisisitiza kwamba masuala hayo yataendelea kuwa na umuhimu kwa Wazanzibari na Watanzania wote katika kujikumbusha mzizi wa fitina wa Kikolini uliokatwa na waasisi wa Mapinduzi hayo Mwaka 1964.
Balozi Seif alisema zaidi ya Miaka 200 iliyopita kabla ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar Wakwezi na Wakulima wa Visiwa vya Zanzibar walikuwa wakinyanyaswa kimaisha, madhila yaliyoamsha ari kwa Waasisi wa ASP kuandaa mipango ya kujikomboa kwa hali yoyote ile.
Aliwahakikishia Viongozi na wanacham hao wa CCM kwamba yale yote yaliyoasisiwa na Viongozi wa Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964 kuhusiana na masuala ya Elimu, Afya na Eka Tatu Tatu walizopewa Wananchi bila ya malipo kuendesha maisha yao yataendelea kutekelezwa daima.
Credits: MoDewji Blog
ZeroDegree.
Balozi Seif aweka hadharani mbinu itakayotumiwa na CCM katika uchaguzi mkuu 2020
Reviewed by Zero Degree
on
1/15/2017 12:47:00 PM
Rating: