Loading...

Hawa hapa wakurugenzi wa ufundi wanaotamba zaidi kwenye mpira wa miguu duniani

SOKA ina mambo mengi, ambapo ukiachana na muunganiko wa wachezaji, benchi la ufundi, uongozi wa klabu na mengineyo, wako watu wanaoitwa Wakurugenzi wa Ufundi ambao wana kazi kubwa katika kuhakikisha klabu zinapata mafanikio makubwa.

Mkurugenzi wa Ufundi ni mtu muhimu zaidi kwenye timu, mwenye majukumu mengi ya kiutendaji na ambaye anakuwa katikati ya bodi ya klabu, makocha na wachezaji.

Barani Ulaya, kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili majira ya baridi mwezi huu wa Januari, biashara, mipango na mikakati yote ya uhamisho wa wachezaji kutoka na kuingia katika klabu huwa chini ya Mkurugenzi wa Ufundi.

Wako wakurugenzi wengi wenye majina wanaofahamika kutokana na mipango yao wanayoifanikisha lakini makala hii leo inakuletea orodha ya wakurugenzi watano wanaofanya vizuri katika klabu mbalimbali barani Ulaya.

Txiki Begiristain (Manchester City)



Alifanya kazi kubwa katika kuhakikisha ujio wa kocha mwenye mafanikio makubwa ndani ya klabu ya Manchester City, Pep Guardiola.

Begiristain alitumia uzoefu wake mkubwa wa ushawishi kutokana na kuitambua falsafa ya Guardiola, huku pia akichagizwa na ukaribu uliokuwepo kati ya wawili hao.

Begiristain ni miongoni mwa wataalamu wachache wa sayansi ya soka waliokuwa wakiishi katika ndoto za kocha Johan Cruyff, kipindi hicho wakiwa Camp Nou, ambapo kwa sasa amekuwa na uwezo mkubwa katika utendaji kazi wake katika eneo hilo akiwa sambamba na Guardiola, aliyewahi kucheza naye pamoja katika klabu ya Barcelona.

Wakati Begiristain akiwa Barcelona, alikuwa kiungo muhimu kufanikisha ushirikiano miongoni mwa wachezaji, viongozi na benchi la ufundi kuwa imara, ikiwamo kusajili na kuwafanya baadhi ya wachezaji kuwa kama alama ya timu hiyo.

Baadhi ya nyota walioacha alama ndani ya Barcelona chini ya ushawishi wake ni pamoja na Dan Alves, Eric Abdal na Gerarlad Pique.

Na alichofanikiwa kukifanya hadi sasa kwenye kikosi cha City ni kuweka mtandao mkubwa wa wang’amua vipaji ‘scouts’ nje ya mipaka.

Hata hivyo, aliweza kuwapata wachezaji wenye majina makubwa ambao walikuwa na uwezo wa juu wakichagizwa na uzoefu wa michuano mikubwa akina Eliaquim Mangala (pauni milioni 32) na Wilfried Bony (pauni milioni 25), ingawa hawakufanya vizuri na kumpelekea Guardiola kuushawishi uongozi wa Man City kuwatoa kwa mkopo.

Marcel Brands (PSV)



Mafanikio ya kikosi cha PSV Eindhoven ya Uholanzi, kufanya vema katika Ligi Kuu ya nchi hiyo hadi kuweza kutwaa mataji na kuonekana moja ya klabu ngumu na bora barani Ulaya kwa kiasi kikubwa yametokana na juhudi za Brands ambaye husimamia kwa usahihi maeneo yote ya timu yanayomhusu.

Ufahamu wake mkubwa wa masula ya soka, ulianza kuzaa matunda akiwa na kikosi cha Waalwijk’s kama mkurugenzi na kuifufua timu hiyo ambayo ilikuwa hoi.

Brands alipowasili tu PSV mwaka 2010, kwa muda mfupi aliweza kutengeneza sera nzuri za uendeshaji wa timu hususani eneo la ufundi, akianza na suala la usajili, akiwa sambamba na kocha Phillip Cocu, kusajili wachezaji mahiri, hatua iliyowawezesha kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu 2015, baada ya ukame wa miaka saba na siku chache baadaye wakafanya biashara nzuri ya wachezaji wake, Georginio Wijnaldum na Memphis Depay, waliouzwa baadaye kwa bei ghali.

Giuseppe Marotta (Juventus)



Moratta aliyeajiriwa na Juventus mwaka 2010 akitokea Sampdoria, amekuwa mhimili mkubwa katika viunga hivyo vya Turin kama kiungashi bora cha timu kufanya vizuri katika Ligi Kuu ya Italia, maarufu Serie A, Ligi ya Mabingwa Ulaya pamoja na kufanya uhamisho wa wachezaji kwa bei ghali zaidi.

Weledi wake katika masuala ya kisoka umeifanya Juventus kutesa zaidi katika Serie A kwa miaka ya karibuni na hivyo kunyakuwa mataji matano ya Serie A ‘Scudetto’ kati ya mwaka 2011 hadi 2016 pekee.

Hata kocha wa Chelsea wa hivi sasa, Antonio Conte, alionekana bora zaidi katika kipindi alichokuwa chini yake licha ya kwamba baadaye mikoba yake ilichukuliwa na Massimiliano Allegri.

Vile vile Mkurugenzi huyo alikuwa chachu pia ya usajili wa mafundi waliovutia ulimwengu wa soka wakiwemo akina Andrea Pirlo, Sami Khedira, Paul Pogba, Carlos Tevez, Patric Evra, Andrea Barzagli na Arturo Vidal, aliowasainisha kwa fedha kiduchu lakini hadi sasa ni wachezaji wa madaraja ya juu wakiwa na klabu tofauti tofauti baada ya kuuzwa.

Monchi (Sevilla)



Licha ya kwamba soka ya Hispania imetawaliwa na miamba kama Real Madrid, Barcelona na kufuatiwa kwa mbali na Atletico Madrid kutokana na uwezo wa kiuchumi zilizonazo klabu hizo, lakini kuna klabu nyingine kama Sevilla inayozifukuzia kwa mafanikio ndani na nje ya uwanja.

Na hii inatokana na uwezo na weledi wa hali ya juu wa Mkurugenzi wao wa ufundi aitwaye Monchi ambaye anasifika kutokana na mipango yake sahihi katika soka.

Miongoni mwa vitu vya kwanza kabisa ambavyo Monchi alitangulia kuvifanya ndani ya klabu ya Sevilla kuiwezesha iwe ya ushindani zaidi ni kusimamia shule za soka ‘academy’ ziweze kuzalisha vipaji vya kutosha mahali hapo ndani ya miaka mitatu hadi mitano, jambo ambalo aliweza kufanikiwa.

Unaweza kulithibitisha hili kwa kuviangalia vipaji alivyowahi kuviibua ambavyo vinatamba hadi hii leo kama akina Sergio Ramos wa Real Madrid, Alberto Moreno (Liverpool), Jesus Navas (Manchester City) na Jose Antonio Reyes (Espanyol).

Pia Monchi alitengeneza sera maridadi ya mtandao mkubwa wa kusajili wachezaji kwa dau dogo na baadaye kuwauza kwa mkwanja mrefu.

Miongoni mwao ni Dani Alves, Grzegorz Krychowiak, Ivan Rakitic, Carlos Bacca na Kevin Gameiro.

Michael Zorc (Borussia Dortmund)



Zorc anakumbukwa zaidi na ulimwemgu wa soka kwa kufunga idadi kubwa ya mabao akiitendea haki nafasi ya ushambuliaji, hususani ndani ya klabu ya Borussia Dortmund, kabla ya kutundika daluga mwaka 1998 na kuingia rasmi darasani kusomea masuala mazima yahusuyo soka katika eneo la ufundi kwa ujumla.

Baada ya kuhitimu mwaka 2008, akawa rasmi Mkurugenzi wa ufundi akiwa na wasifu wa juu kabisa katika ngazi hiyo akisimami hadi masula ya uchumi.

Matunda yake yalianza kuonekana kwa kumtambulisha kwenye dunia ya soka Mario Gotze, pamoja na kuendeleza vipaji vya makinda kama Mats Hummels, Ilkay Gundogan na Robert Lewandowski, wanaoking’arisha kikosi cha Bayern Munichi wakitokea Borussia Dortmund.

ZeroDegree.
Hawa hapa wakurugenzi wa ufundi wanaotamba zaidi kwenye mpira wa miguu duniani Hawa hapa wakurugenzi wa ufundi wanaotamba zaidi kwenye mpira wa miguu duniani Reviewed by Zero Degree on 1/16/2017 12:16:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.