Loading...

Jinsi mkosi wa majeraha unavyoanza kuimaliza Real Madrid

KUNA rekodi moja ya kushtua imewekwa na Real Madrid msimu huu kwenye La Liga. Unaijua ni ipi hiyo?

Wachezaji 19 kati ya 24 kwenye kikosi chao wameshapata majeraha yaliyowafanya wakose baadhi ya michezo msimu huu.

Tangu kuanza kwa mwaka 2017, kama wiki tatu zilizopita, beki kisiki Pepe, kiungo James Rodriguez, Daniel Carvajal, Luka Modric na Marcelo, wmepata majeraha yatakayowafanya waungane kwenye vitanda vya wagonjwa sambamba na Gareth Bale aliye nje ya kikosi tangu Novemba mwaka jana.

Mjadala umekuwa mkubwa sana hivi sasa juu ya kinachopelekea wachezaji wa Madrid kupata majeraha kwa kiwango hiki, japo asilimia kubwa ya maumivu yao yanatokana na rafu na si matatizo ya misuli.

Wako wanaoamini ushindi wa mechi 40 mfululizo uliwaondolea umakini baadhi ya wachezaji kwa kushindwa kujilinda na matukio hatarishi ya uwanjani.

Lakini wengine wametoa sababu kwa kumshutumu Zidane kwa kuhatarisha afya za nyota wake wenye historia za kuwa majeruhi mara kwa mara.

Nyota kama Modric na Marcelo hawakupaswa kucheza kwa dakika 90 kwenye michezo mitatu mfululizo kutokana na historia yao ya majeraha.

Lakini pamoja na sababu hizo, bado Zinedine Zidane ameweza kupanga vyema kikosi chake na kupata matokeo hata anapowakosa baadhi ya nyota wake muhimu kwenye kikosi cha kwanza.

Kwa mfano, msimu huu Luka Modrick amekosa michezo 12 akiwa majeruhi na katika kipindi hicho Zidane aliifumua safu yake ya kiungo na kufanikiwa kushinda mechi nane na kutoka sare 4.

Watu kama Casemiro na Toni Kroos wamekuwa wakitumika kuwasaidia kina Isco Alarcon, Marco Asensio na Lucas Vazquez kwa ajili ya kuiongezea nguvu safu ya ushambuliaji.

Uwezo wa Casemiro kucheza nafasi zaidi ya mbili, akicheza kama kiungo mkabaji na mlinzi wa kati amekuwa msaada mkubwa kwenye kikosi cha Real Madrid msimu huu.

Upande wa kushoto, mrithi wa Marcelo ni Mreno Fabio Coentrao, ambaye mara zote amekuwa kwenye kiwango bora anapopewa nafasi lakini kwa bahati mbaya naye yuko nje.

Upande wa kulia mpaka sasa ni wazi Carvajal amekuwa kwenye kiwango bora na ni msaada mkubwa kwenye sehemu ya ulinzi ya kushambulia. Ni mtu muhimu kwenye kikosi na hakika Zidane atakuwa akipasua kichwa kupata mrithi wake.

Mpaka sasa hakuna asiyejua wasiwasi wa mashabiki wa Real Madrid juu ya kiwango cha beki Mbrazil, Danilo. Hakuna anayemwamini licha ya uwezo wake wa kukaba na kupandisha mashambulizi, ni wakati wake wa kurejesha imani kwa mashabiki wake.

Kwa mabadiliko haya kazi kubwa iliyo mgongoni mwa Zidane ni kutafuta namna ya kuifanya timu yake icheze kwa kumiliki mpira kwa muda mwingi ili kupunguza presha ya wapinzani kwa walinzi wao wa pembeni.

Msimu uliopita, Real ikiwa chini ya Carlo Ancelotti, mwezi Januari na Februari ndio miezi iliyomaliza ndoto zao za ubingwa wa La Liga na kutupwa nje kwenye michezo ya Kombe la Mfalme na tatizo kubwa lililosababisha yote hayo ni majeruhi.

Ingawa Ancelotti hakuwa na uwezo mzuri wa kuwapumzisha nyota wake kama anavyofanya Zidane lakini hali ya majeruhi inafanana sana hasa kwenye sehemu ya ulinzi.

Kama Zidane atafanikiwa kuilinda timu kwenye miezi hii miwili isipate matokeo mabovu atakuwa amefanikiwa kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kutwaa mataji matatu msimu huu.

Vinginevyo, mchawi huyu wa zamani katika soka atakuwa amejiingiza kwenye mkosi unaoitafuna Real Madrid kwa misimu zaidi ya mitatu sasa kwa kukosa taji la La Liga.

Mara zote Madrid hupotea Januari na kuanza kurudi kwenye mstari Machi, hapo wanakuwa nje kwenye mbio za ubingwa wa La Liga na akili zao zote huziweka katika ligi ya mabingwa, Zidane ana jukumu zito la kupindua hali hii.

ZeroDegree.
Jinsi mkosi wa majeraha unavyoanza kuimaliza Real Madrid Jinsi mkosi wa majeraha unavyoanza kuimaliza Real Madrid Reviewed by Zero Degree on 1/27/2017 12:42:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.